Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Syria ni mbaya si ya kiutu, kibinadamu na haipaswi kuendelea hivyo:UN

Binti akinawa mikono katika kambi ya wakimbizi wa ndani Kaskazini mwa Syria waliotawanywa na vita
© UNICEF/Ali Almatar
Binti akinawa mikono katika kambi ya wakimbizi wa ndani Kaskazini mwa Syria waliotawanywa na vita

Hali nchini Syria ni mbaya si ya kiutu, kibinadamu na haipaswi kuendelea hivyo:UN

Amani na Usalama

Mzozo nchini Syria leo ukianza mwaka wa 13 hli imeelezwa kuwa baya zaidi, isiyovumilika na hatua zahitajika kumaliza madila kwa mamilioni wa taifa hilo walio ndani na nje ya nchi yao kwa mujibu wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa.

Mwakilishi maalum wa umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Geir O. Pedersen amesema “siku hii ambayo vita nchini Syria inaanza kuingia mwaka wa 13 tunawakumbuka kwa machungu makubwa maelfu kwa maelfu ya watu walipoteza maisha na kukumbusha ukatili na madhila kwa mamilioni ya watu wakiwemo waliolazimika kuyakimbia makazi yao na maelfu ambao bado wanashikiliwa kinyume cha sheria na wale waliotoweshwa na kutojulikana waliko.”

Ameongeza kuwa hali ya maisha nchini Syria ni haifai na kuendelea nayo ni kukiuka ubinadamu na mantiki.

Ameendelea kusema kuwa na majanga ya asili ikiwemo matetemeko ya ardhi ya hivi karibuni yameongeza madhila kwa watu hao na kuacha changamoto hali ambayo ni ukumbusho kamili kwamba hali iliyopo si endelevu na haiwezi kuendelea.

Ameahidi kwamba “Baada ya matetemeko hayo ya ardhi, tunayo dhima ya pamoja ya kibinadamu ili kuondoa siasa kwenye juhudi za misadai. Hii inamaanisha tunahitaji fursa za kuwafikia wahitaji, kupitia njia zote, tunahitaji rasilimali na tunahitaji utulivu endelevu.”

Mgao wa chakula wa kila mwezi ukisambazwa kwa familia zilizokimbia makazi yao katika eneo la Sukari huko Aleppo, Syria.
© WFP/Hussam Al Saleh
Mgao wa chakula wa kila mwezi ukisambazwa kwa familia zilizokimbia makazi yao katika eneo la Sukari huko Aleppo, Syria.

Syia inasalia kuwa mgogoro wenye changamoto kubwa duniani

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na kaimu mratibu mkazi wa Syria El-Moustafa Benlamlih na mratibu wa kikanda wa masuala ya kibinadamu Muhannad Hadi kuhusu miaka 12 ya vita hivyo inasema “Syria inasalia kuwa mojawapo ya dharura tata zaidi za kibinadamu na ulinzi duniani huku watu milioni 15.3 kote nchini wakitathminiwa kuhitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu wa 2023 ambayo ni idadi kubwa zaidi ya watu wanaohitaji msaada tangu kuanza kwa vita.”

Syria pia inasalia kuwa moja ya mizozo mikubwa zaidi ya watu kulazimika kuhama makwao duniani, kukiwa na watu milioni 6.8 wakilazimika kuwa wakimbizi wa ndani ya nchi hiyo, mara kadhaa, na angalau wengine milioni 6.6 wakiishi kama wakimbizi nje ya Syria.

Mamilioni ya Wasyria wanasukumwa kwenye njia panda ya mustakbali wao huku kukiwa na kuporomoka kwa huduma za kimsingi, mlipuko wa kipindupindu unaoendelea, kuongezeka kwa bei ya chakula na nishati na mdororo wa kiuchumi. Tetemeko kubwa la ardhi la mwezi Februari limeongeza safu nyingine ya janga na kukata tamaa, ambapo watu milioni 8.8 waliathiriwa.

Janga la utapiamlo labisha hodi

Familia zikiishi katika kambi za wakimbizi wa ndani Kusini mwa Syria zinachangamoto hata ya kukizi chakula kwa watoto wao
© UNICEF/Hasan Belal
Familia zikiishi katika kambi za wakimbizi wa ndani Kusini mwa Syria zinachangamoto hata ya kukizi chakula kwa watoto wao

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema “Miaka 12 ya vita, na matetemeko mabaya ya ardhi ya hivi karibuni, yamewaacha mamilioni ya watoto nchini Syria katika hatari kubwa ya utapiamlo,”.

Limeongeza kuwa wakati mzozo huo ukiingia mwaka wake wa 13 leo, uhasama unaendelea bila kusitishwa katika maeneo kadhaa ya nchi, hasa kaskazini magharibi.

Ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto unaendelea. UNICEF inasema “Tangu kuanza kwa vita, karibu watoto 13,000 nchini Syria wameuawa au kujeruhiwa, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Watoto wanaendelea kuishi kwa hofu ya kushambuliwa, kuhama makazi yao na viwango vya utapiamlo vinaongezeka kwa kasi.”

Kulingana na makadirio, ya shirika hilo zaidi ya watoto 609,900 walio chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa nchini Syria.

Kudumaa hutokana na utapiamlo wa muda mrefu na husababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa ya kimwili na kiakili kwa watoto.

Hii inaathiri uwezo wao wa kujifunza, tija na mapato yao baadaye katika utu uzima.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA limesema miaka hiyo 12 ya vita imekuwa “ni miaka 12 ya uharibifu, miaka 12 ya kuanguka kwa uchumi, miaka 12 ya matumaini yaliyomomonyoka, miaka 12 ya ndoto zilizovunjika na miaka 12 ya mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka kila uchao.”