Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNRWA alaumu kampeni ya Israel ya kulisambaratisha shirika analoliongoza

Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Wapalestina.
UN Photo/Evan Schneider
Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Wapalestina.

Mkuu wa UNRWA alaumu kampeni ya Israel ya kulisambaratisha shirika analoliongoza

Amani na Usalama

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kuwasaidia Wapalestina, UNRWA, leo Aprili 17 mbele ya Wajumbe wa Baraza la Usalama amelaumu vikali, kampeni ya Israel ya kulisambaratisha UNRWA.

"Leo hii, kampeni ya hila ya kuzima operesheni za UNRWA inaendelea, ikiwa na athari kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa," Philippe Lazzarini amewaeleza wajumbe.

Shinikizo kubwa

Ingawa hali ya kibinadamu huko Gaza ni mbaya baada ya miezi sita ya mzozo uliochochewa na shambulio la umwagaji damu la Hamas kusini mwa Israeli mnamo Oktoba na kufuatiwa na ulipizaji kisasi wa jeshi la Israeli, Bwana Lazzarini alibainisha kuwa UNRWA inajiona hivyo kutokana na mamlaka ya Israeli kuinyima nafasi ya kutoa msaada kaskazini mwa Palestina licha ya amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuongeza mtiririko wa misaada Gaza.

Mkuu huyo wa UNRWA ameeleza kuwa mamlaka ya shirika lake yanaungwa mkono na mataifa mengi wanachama wa Baraza la Usalama, "Hata hivyo shirika hilo liko chini ya shinikizo kubwa. Wanakabiliwa na kampeni ya kufukuzwa kutoka ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Huko Gaza, serikali ya Israel inataka kukomesha shughuli za UNRWA,” ameshutumu, akibainisha kuwa majengo na wafanyakazi wa UNRWA yalilengwa tangu kuanza kwa vita, huku wafanyakazi 178 wa UNRWA wakiuawa.

Philippe Lazzarini pia amesisitiza kuwa hali katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu ni "wa kutia wasiwasi sana". Nafasi ya kazi ya UNRWA inapungua, na hatua za kiholela zilizowekwa na Israeli kuzuia uwepo na harakati za wafanyakazi. "Inazidi kuwa vigumu kuweka wazi na ufikiaji shule zetu na vituo vya afya. Hatua za kisheria na kiutawala zinazolenga kuwafukuza UNRWA kutoka makao makuu yake huko Jerusalem Mashariki na kupiga marufuku shughuli zake katika eneo la Israel zinaendelea,” akasema.

Kubakiza jukumu muhimu la UNRWA

Kwa kumalizia, mkuu wa UNRWA ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza "kuhifadhi jukumu muhimu la UNRWA," kwa msaada wa kisiasa kutoka kwa Nchi Wanachama unaolingana na ufadhili.

Pia amewataka kujihusisha "katika mchakato halisi wa kisiasa unaoelekea kwenye suluhu inaloweza kuleta amani kwa Wapalestina na Waisraeli." Hatimaye akasema kwamba ilikuwa muhimu kutambua "kwamba mchakato wa kisiasa pekee hautahakikisha amani ya kudumu".

“Lazima tukatae kuchagua kati ya kuwahurumia Wapalestina au Waisraeli; au kuwaonea huruma Wagaza au mateka wa Israel na familia zao, badala yake, lazima tutambue na kutafakari kwa maneno na matendo yetu kwamba Wapalestina na Waisraeli wanashiriki uzoefu wa muda mrefu na wa kina wa huzuni na hasara. Na wastahili pia maisha yajayo yenye amani na usalama.” Amesisitiza Mkuu huyo wa UNRWA.