Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: “Hali si hali” katika hospitali, wagonjwa wanakufa kwa maambukizi

Hospitali ya Kimataifa ya Kikosi cha Medical Corps huko Rafah, Gaza
WFP
Hospitali ya Kimataifa ya Kikosi cha Medical Corps huko Rafah, Gaza

Gaza: “Hali si hali” katika hospitali, wagonjwa wanakufa kwa maambukizi

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina (UNRWA) leo Machi 28 limetahadharisha kuhusu ujio wa baa la njaa katika Ukanda wa Gaza.

UNRWA imesema yenyewe ni uti wa mgongo wa misaada ya kibinadamu Gaza lakini bado misafara yao iliyosheheni vyakula imezuiwa kufika kaskazini, ambako baa la njaa linajongea.

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema kati ya hospitali 36 katika Ukanda wa Gaza, ni 10 tu ambazo zimesalia zikifanya kazi japo nazo kwa kiasi kidogo.

Kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, UNRWA  inasema muda unayoyoma, vikwazo lazima viondolewe sasa.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilal Nyekundu, IFRC, linaonya kuwa huduma za afya kaskazini mwa Gaza zimeharibiwa kwa kiasi kikubwa, na kwamba mfumo wa afya kusini mwa Ukanda wa Gaza uko hatarini kusambaratika.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu OCHA imesema hayo hiii leo kupitia ripoti yake ya hivi karibuni zaidi.

Theluthi mbili ya hospitali 36 Gaza hazitoi tena huduma

OCHA inasema mfumo wa afya Gaza unasambaratika kutokana na kuendelea kwa mapigano na ukosefu wa njia za kupitisha huduma, na hivyo kusababisha hospitali nyingi kushindwa kutoa huduma.

Wakati hospitali 24 kati ya 36 huko Gaza haziwezi kutoa huduma, hospitali mbili zinatoa huduma kwa kiwango kdigo, na 10 zinafanya kazi kidogo ambapo nne ziko kaskazini na sita ziko kusini. Takwimu hizi zinafuatia hesabu iliyofanywa jumatano.

Kwa siku kadhaa, mapigano kati ya jeshi la Israeli na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas kwenye eneo lililozingirwa na Israeli, yamejikita kwenye maeneo ya hospitali, hasa zile zilizoko mji wa Gaza na Khan  Younis.

Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yanasema kasi ya mashambulizi haijapungua licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa Jumatatu  Machi 25 likitaka “sitisho la mara moja” la mapigano.

Hali si hali Gaza

Yaliyomo ndani ya ripoti mpya ya OCHA yanatia hofu kubwa. Nyaraka inaelezea mazingira katika hospitali ya European Gaza au (HEG) iliyoko Khan Younis. Mazingira si ya kufikirika na hayawezi kueleweka.

Wagonjwa wanakufa kutokana na maambukizi, madaktari wamezidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa. Hospitali hiyo ina uwezo wa kuwa na vitanda 200 pekee, lakini imepanuliwa ili kuwa na vitanda 1,000. Hata hivyo bado haikidhi mahitaji kutokana na uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu, kuharibiwa kwa miundombinu na vikwazo vya kufikiwa na misaada.

Takribani wakimbizi 22,000 hadi sasa wamesaka hifadhi kwenye hospitali hiyo, wakijihifadhi kwenye shoroba za hospitali na kwenye mahema yaliyo nje ya hospitali.

Hospitali ya Al-Shifa imezingirwa kwa siku 10 sasa

Hospitali ya Al-Shifa imekuwa imezingirwa  na jeshi la Israeli kwa siku 10 sasa ambamo wagonjwa na wahudumu wa afya wamefungiwa kwenye jengo lililokuwa linatumiwa na ofisi ya rasilimali watu ambayo haijaundwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya.

Huko Khan Younis, operesheni nzito za kijeshi, wanajeshi wa Israeli walilazimisha watumishi wa hospitali na majeruhi kuondoka hospitali ya Al Amal na kufunga lango kuu kwa kuweka vizuizi.

Juzi Jumanne, hospitali na jengo la jirani la makao makuu ya Chama cha Hilal Nyekundu cha Palestina vilikoma kufanya kazi.

"IFRC imedokeza kuwa kufungwa kwa hospitali ya Al Amal, moja ya vituo vichache vya afya vilivyosalia vikifanya kazi huko Kusini kutakuwa na madhara makubwa,” imesema OCHA.