Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chini ya operesheni 1 kati ya 2 za misaada za UN ndizo zimeweza kuingia Gaza Kaskazini mwezi huu

Watoto katika Ukanda wa Gaza wanapokea chakula huku mahitaji yakiendelea kupungua.
© UNRWA
Watoto katika Ukanda wa Gaza wanapokea chakula huku mahitaji yakiendelea kupungua.

Chini ya operesheni 1 kati ya 2 za misaada za UN ndizo zimeweza kuingia Gaza Kaskazini mwezi huu

Msaada wa Kibinadamu

Wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamesema chini ya nusu ya misafara ya misaada ya Umoja wa Mataifa iliyopangwa kuelekea kaskazini mwa Gaza eneo lililokumbwa na njaa ndiyo iliyofanikiwa kufikia sasa kwa mwezi huu, licha ya wito wa mara kwa mara kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza misaada kwa zaidi ya watu milioni moja wanaokabiliwa na njaa.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, imesema wiki mbili za kwanza za mwezi Machi zilishuhudia operesheni 11 tu kati ya 24 "zilizowezeshwa na mamlaka ya Israeli. Nyingine zilikataliwa au kuahirishwa."

OCHA imeendelea kubainisha kuwa misafara mitano ilikataliwa kuingia na minane iliahirishwa.

"Operesheni zilizowezeshwa kimsingi zilihusisha usambazaji wa chakula, tathmini za lishe na afya, na usambazaji wa vifaa hospitalini," imesema OCHA ikirejea kuonya kwamba "vikwazo vya ufikiaji wa kibinadamu vinaendelea kuathiri sana utoaji wa msaada wa kuokoa maisha kwa wakati, haswa kwa mamia. ya maelfu ya watu kaskazini mwa Gaza”.

Akiunga mkono wito huo leo Jumatano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezitaka mamlaka za Israel "kuhakikisha upatikanaji kamili na usio na vikwazo wa ufikishaji bidhaa za kibinadamu kote Gaza na kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono kikamilifu juhudi zetu za kibinadamu".

Akizungumza kutoka Brussels Ubeligiji ambako anafanya mikutano na wawakilishi wa Muungano wa Ulaya, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amerejea wito wake wa "kuendelea kufanya kila liwezekanalo kukomesha mauaji, kufikia usitishaji mapigano kwa minajili ya kibinadamu na kuhakikisha kuachiliwa huru bila masharti kwa mateka wote waliosalia".

Kivuko cha Wadi Gaza

OCHA imesema kupeleka misaada kaskazini mwa Gaza kunahitaji "idhini za siku hadi siku kutoka kwa mamlaka ya Israeli, lakini licha ya jitihada zote za kuratibu mchakato huo, mara nyingi misafara ya malori inarudishwa na kuzuiliwa hata baada ya kusubiri kwa muda mrefu katika kituo cha ukaguzi cha Wadi Gaza ambayo ni lango la kaskazini mwa Ukanda huo.”

Misafara ya misaada pia imekuwa lengo la "watu waliokata tamaa", OCHA imeendelea kusema kuwa kwenye kituo cha ukaguzi au kwenye njia ngumu ya kaskazini wanapopitia ndio njia pekee ya kuhakikisha kwamba misaada ya kutosha inaweza kutolewa kwa misingi ya kutegemewa.

Katika kipindi kama hicho cha wiki mbili mwezi Machi, mamlaka ya Israel ilitoa fursa kwa operesheni tatu kati ya nne za misaada katika maeneo ya kusini mwa Wadi Gaza operesheni 78 kati ya 103 zimefanyika , huku 15 zikizuiliwa na 10 zikiahirishwa au kufutwa, kulingana na OCHA.

Njaa inakaribia

Kwa muda sasa njaa imekaribia katika sehemu za eneo hilo, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNWRA, huku kukiwa na ripoti za usiku kucha kwamba watu 24 walikufa katika shambulio la msafara wa misaada kaskazini mwa mji wa Gaza.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X UNRWA ilisema "Kwa wastani, malori 159 ya misaada kwa siku yalivuka hadi Ukanda wa Gaza kufikia sasa Machi. Idadi hiyo iko chini ya mahitaji,” 

Kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia inasalia kuwa njia pekee ya kuhakikisha kwamba misaada ya kutosha inafika Gaza kwa njia ya nchi kavu na yenye ufanisi zaidi kuliko matone tu yanayodondoshwa kwa njia ya anga au usafirishaji wa baharini wamesisitiza kwa muda mrefu maafisa wa misaada ya kibinadamu.

Wakati huohuo, kwa mujibu wa duru za habari mazungumzo yameingia siku ya tatu nchini Qatar siku leo kati ya wajumbe wakiwemo Israel, Marekani na Misri.

Takwimu za hivi karibuni kutoka kwa mamlaka ya afya ya eneo linalokaliwa la Ukanda wa Gaza zinaonyesha kuwa idadi ya vifo tangu tarehe 7 Oktoba imeongezeka hadi 31,923 huku watu 74,096 wakijeruhiwa.