Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa nchi 4 waonesha jinsi TB inavyoweza kutokomezwa kwa uwekezaji wa kila dola 1

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa. (Maktaba)
UN News/Daniel Dickinson
Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa. (Maktaba)

Mpango wa nchi 4 waonesha jinsi TB inavyoweza kutokomezwa kwa uwekezaji wa kila dola 1

Afya

Kenya ni miongoni mwa nchi nne duniani zilizoshiriki katika kuandaa mpango unaoonesha ni kwa kiasi gani  uwekezaji katika uchunguzi na tiba dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB unaweza kuleta mafanikio makubwa katika kutokomeza ugonjwa huo unaoendelea kuua duniani licha ya kuwa na kinga na tiba.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inataja nchi zingine kuwa ni Brazil, Georgia na Afrika Kusini ambapo kupitia huo mpango uwekezaji unaweza kuleta manufaa ya kiafya na kiuchumi katika nchi hizo nne kwani kila dola 1 inayowekezwa inaweza kuleta marejesho ya dola 39.

Mpango unaeleza nini?

Muundo huo unaeleza kuwa uchunguzi dhidi ya Kifua Kikuu sambamba na tiba ya kuzuia vinaweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa pamoja na vifo.

“Unaeleza kuwa uwekezaji huu muhimu wa afya ya umma ni muhimu katika kushughulkia mahitaji ya kukidhi mahitaij ya wananchi walio hatarini na kufanikisha malengo ya kutokomeza TB,” imesema muundo huo.

Mpango huo umetolewa ili kusaidia nchi kuchagiza na kusambaza rasilimali za kuongeza uchunguzi na tiba dhidi ya TB kuelekea kufikia malengo mapya yaliyopitishwa na wakuu wa nchi na viongozi kwenye mkutano wa mwaka 2023 kuhusu ugonjwa huo.

Dkt. Tedros azungumza

“Mpango huu uliowasilishwa na nchi 4, unaweka bayana mantiki ya kiuchumi na kiafya kwa kuzingatia ushahidi, mapendekezo yaliyotolewa na WHO kuhusu uchunguzi na tiba ambavyo vinaweza kuchangia katika huduma ya afya kwa wote,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akiongeza kuwa leo hii WHO ina ufahamu, mbinu na utashi wa kisiasa wa kutokomeza ugonjwa huu uliodumu miaka na miaka na ambao bado unasalia kuwa moja ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani.

Ingawa juhudi za kimataifa za kutokomeza Kifua Kikuu zimeshaepusha vifo milioni 750 tangu mwaka 2000, bado ugonjwa huo unasababisha vifo vya watu milioni 1.3 kila mwaka, na kuathiri mamilioni wengine huku madhara yakisalia kwa jamii na familia, imesema WHO.

Mwaka 2022, WHO iliripoti kukwamua vizuri katika kufanikisha upatikanaji wa huduma ya uchunguzi dhidi ya Kifua Kikuu na matibabu, huku kukiwa na idadi kubwa ya watu waliofikia huduma hizo tangu WHO ianze kufuatilia ugonjwa huo mwaka 1995.

Nini kifanyike kutekeleza mkakati wa kutokomeza TB

Hata hivyo sasa hivi kasi imepungua, “kuzuia maambukizi ya Kifua Kikuu na kukomesha kubadilika kutoka maambukizi kuwa ugonjwa ni muhimu katika kupunguza wagonjwa wa TB kwa mujibu wa viwango vilivyomo kwenye Mkakati wa WHO wa kutokomeza Kifua Kikuu.”

Mpango unasema kufanikisha hilo lazima kupatia huduma za tiba ya kinga dhidi ya Kifua Kikuu kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi au VVY, kaya zilizo na wagonjwa wa Kifua Kikuu na makundi mengine yaliyo hatarini.

Usugu wa dawa dhidi ya Kifua Kikuu au MDR-TB, unasalia kuwa tishio kubwa la afya ya umma. Wakati watu 410,000 walikumbwa na usugu wa dawa dhidi ya TB mwaka 2022, ni watu 2 tu kati ya 5 walipata tiba.

Ni kwa mantiki hiyo kulekea siku ya Kifua Kikuu duniani mwaka huu wa 2024, ujumbe ni ‘Ndio! Tunaweza kutokomeza Kifua Kikuu!’ na unalenga kusambaza ujumbe wa matumaini ya kurejea katika mwelekeo wa kutokomeza ugonjwa huo.