Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani umalize migawanyiko- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.
UN Video
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani umalize migawanyiko- Guterres

Amani na Usalama

Waislamu duniani kote wakianza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametaka kipindi hiki kitumike kujenga hamasa kumaliza migawanyiko, kusaidia wenye  uhitaji na kufanya kazi kwa pamoja kwa usalama na utu wa kila mkazi wa dunia hii.

Katika ujumbe wake wa video, Guterres amesema mwezi huu mtukufu wa Ramadhani lazima utumike kuleta amani, “na utuongoze kuelekea dunia yenye haki na huruma zaidi.”

Katibu Mkuu amesema mambo hayo ni muhimu kutekeleza kwani Ramadhani inabeba maadili ya amani, mnepo na ukarimu.

Hata hivyo amesema mwezi huu mtukufu Ramadhani unakuja wakati ambapo watu wengi watafunga huku wakikabiliwa na mizozo, ukimbizi na hofu.

“Fikra zangu na moyo wangu viko nao – kuanzia wananchi wa Afghanistan  hadi Sahel, kuanzia Pembe ya Afrika hadi Syria na kwingineko.Na ningependa kutoa ujumbe maalum wa mshikamano na usaidizi kwa wale wanaokumbwa na machungu na zahma ya Gaza,” amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema katika zama hizi za majaribu, “nia ya Ramadhani ni nguzo ya matumaini, kumbusho la utu wetu wa pamoja.”

Guterres ametuma salamu zake za dhati kwa mamilioni ya waislamu duniani kote wanaoanza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuwatakia mfungo mwema.