Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani: Kinachotuunganisha kiimarike kuliko kinachotugawa

Nchini Jordan wakimbizi wakiwa pamoja kwa futari wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
© UNHCR/Benoit Almeras
Nchini Jordan wakimbizi wakiwa pamoja kwa futari wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani: Kinachotuunganisha kiimarike kuliko kinachotugawa

Utamaduni na Elimu

Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ukianza tarehe 5 mwezi huu, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,UNHCR Filippo Grandi ametoa salamu za kuwatakia waumini wa dini ya kiislamu mfungo mwema akisema kuwa mwezi huu mtukufu unakuja wakati ambao kunashuhudiwa mazingira magumu zaidi.

Katika salamu zake alizotoa kutoka kambi ya wakimbizi ya Kutupalong huko Bangladesh ambako ni makazi ya takribani wakimbizi milioni moja wa kabila la warohingya kutoka Myanmar, Bwana Grandi ametaja mazingira hayo magumu kuwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya watu walio kwenye nyumba za ibada, chuki dhidi ya wageni na hata hisia ngumu za kisiasa dhidi ya wale wanaohitaji msaada zaidi.

Hata hivyo amesema licha ya mazingira hayo magumu, bado anaguswa zaidi na ukarimu unaoonyesha na biandamu tena wale walio na uwezo mdogo.

Nchini Uingereza wapishi wakuu ambao ni wakimbizi wakibadilishana uzoefu wa mapishi ya futari.
© UNHCR/Kim Nelson
Nchini Uingereza wapishi wakuu ambao ni wakimbizi wakibadilishana uzoefu wa mapishi ya futari.

“Nasalia kuvutiwa na watu na viongozi ambao wanachagua ujasiri dhidi ya mgawanyiko na upendo dhidi ya uoga,” amesema Bwana Grandi akiongeza kuwa “katika dunia ambayo kila uchao tunashuhudia machungu na mateso ya binadamu pamoja na kukata tamaa, huku watu takribani milioni 70 wakiwa wamefurushwa makwao, uvumilivu na huruma ambavyo ni maadili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.”

Kwa mantiki hiyo Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR amesema, “hebu na tutumie mwezi huu wa kujitafakari kwa kukumbuka watu waliopoteza maisha wakati wakisaka usalama na hifadhi na tuonyeshe uungwaji mkono kwa mamilioni ambao wamefurushwa makwao kwa sababu ya ghaia au mateso.”

Bwana Grandi amesema “hebu na tuwakumbuke kwa mnepo wao na tuonyeshe mshikamano nao wao leo na siku zote,” na kwamba mwezi huu mtukufu wa Ramadhani unatuma ujumbe muhimu zaidi hii leo ya kwamba, “kile kinachotuunganisha kiimarike kuliko kile kinachotugawa.”