Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uongozi wa jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini waomba usaidizi zaidi wa ulinzi

Mtoto mwenye umri wa mwaka 1 anafanyiwa unchunguzi wa matibabu kama kuna dalili za utapiamlo katika kituo cha mapokezi kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.
© WFP/Hugh Rutherford
Mtoto mwenye umri wa mwaka 1 anafanyiwa unchunguzi wa matibabu kama kuna dalili za utapiamlo katika kituo cha mapokezi kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.

Uongozi wa jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini waomba usaidizi zaidi wa ulinzi

Amani na Usalama

Huku mzozo wa Sudan ukiendelea, wakimbizi na wanaorejea wanamiminika katika mipaka ya nchi jirani ya Sudan Kusini, wengi wamekuwa wakitafuta hifadhi katika jimbo la Upper Nile nchini humo na wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.  Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umefanya mazungumzo na uongozi wa jimbo hilo kuona namna ya kuwasaidia.

Kutokana na hali hiyo ya ongezeko la wakimbizi katika jimbo la Upper Nile, Anita Kiki Gbeho, Naibu Mwakilishi Maalum mpya wa Katibu Mkuu kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Sudan Kusini UNMISS, na ambaye pia ni Mratibu Mkazi wa Misaada ya Kibinadamu nchini humo amefanya ziara yake ya kwanza huko Malakal kujionea hali iliyo. 

Bi. Anita alijionea wakimbizi wakiandikishwa, aliketi chini na kusikiliza baadhi ya wakimbizi na kuwapongeza wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa kwa kazi kubwa wanayofanya na kisha kuwa na kikao na viongozi wa jimbo la Upper Nile

“Itakuwa vyema kusikia kutoka kwako, Kaimu Gavana, na baraza lako jinsi unavyoona mustakabali ulivyo na tena jinsi gani tunaweza kuwaunga mkono kwa sababu hatimaye, tunataka kuona watu wa Sudan Kusini wanaoamua kurejea wanapata usaidizi, na tunachojaribu kufanya ni kukuunga mkono katika safari ya kusonga mbele”.

Jeremiah Deng ambaye ni Kaimu Gavana wa jimbo la Upper Nile alimueleza kiongozi huyo wa UNMISS kuwa kazi ya kusimamia watu wanaorejea makwao na wakimbizi katika maeneo yenye watu wengi kama hapo ni kubwa kupita kiasi na imekuwa si rahisi kwa mamlaka za serikali.

“Tuna mpaka mrefu ambao uko wazi sana kwamba watu wanaweza kuvuka kutoka upande wowote na kufurika kwa watu kutoka Sudan kuja Sudan Kusini. Watu wengine wanatumia barabara ya mpakani na nyinginezo tofauti, vivukio haramu. Vikosi vyetu vya usalama havina uwezo wa kufunika safu nzima ya mpaka”.

UNMISS inatoa usaidizi wa kufanya doria za mara kwa mara ili kufuatilia kituo cha usalama huku mashirika ya kibinadamu yakifanya kazi ya ziada kutoa misaada inayohitajika.