Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu: Umoja wa Mataifa sio tatizo

Dennis Francis, Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu, akitoa muhtasari wa vipaumbele vyake kwa 2024. (Maktaba)
UN Photo/Eskinder Debebe
Dennis Francis, Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu, akitoa muhtasari wa vipaumbele vyake kwa 2024. (Maktaba)

Rais wa Baraza Kuu: Umoja wa Mataifa sio tatizo

Amani na Usalama

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis Pamoja na mambo mengine amesema Umoja wa Mataifa "sio tatizo" bali tatizo linatokana na kwamba baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanahisi wanaweza kukiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa watakavyo na kukiuka sheria za kimataifa bila kuadhibiwa.

Akizungumza na UNTV jana Februari 26 mjini Geneva, Uswisi ambako anashiriki katika kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Kibinadamu, Balozi Dennis Francis anasema, “hadi sasa, Vita ya Tatu vya Dunia haijatokea. Na bila shaka hiyo ni kwa kiasi kikubwa kutokana na ukweli kwamba Umoja wa Mataifa unatoa jukwaa kwa nchi zote kuja na kuongea yanayowasibu, ili kutoa nafasi ya mazungumzo yanayoweza kuuokoa ulimwenu na janga la vita.

Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa anaendelea kueleza kwamba, "nchi huru lazima zitambue heshima ya eneo la majirani zao na wa nchi zote wanachama, kama njia ya kujenga uhusiano thabiti, mzuri, wa kirafiki," na akasisitiza kwamba kanuni hii "imeingiliwa katika muktadha wa kile Urusi imefanya katika Ukraine. Na hadi hapo hali hiyo itakaporekebishwa na Urusi, itasalia kuwa ajenda ya Umoja wa Mataifa.”

Kuhusu UNRWA amedokeza kwamba uchunguzi unafanyika kwa sasa kuhusu madai ya kuhusika kwa wafanyakazi wa shirika hilo katika mashambulizi ya Oktoba 7.

"Matumaini yangu ni kwamba nchi wafadhili zitaendeleza usaidizi wao na msaada kwa UNRWA. Uchunguzi unaendelea. Ripoti bado hazijatolewa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, lakini kwa vyovyote vile, Shirika lina mamlaka liliyopewa na Baraza Kuu na lazima liwekwe kwenye nafasi, lipewe uwezo, ili kutekeleza majukumu yake. Sio kwa sababu UNRWA inapendelewa, lakini kwa sababu watu wanaoitegemea, maslahi yao lazima yahifadhiwe."

Akigeukia Mkutano wa kuangazia siku zijazo, utakaofanyika Septemba mwaka huu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Balozi Francis anasema,

“Mkutano wa kuangazia siku zijazo unakusudia kuwezesha, maelewano madhubuti, maelewano madhubuti kati ya wakuu wa nchi na serikali, kufufua ushirikiano wa kimataifa, kushikilia nchi kuwajibika kwa ahadi zao ili kuhakikisha kuwa tunapata nafasi nzuri ya kuchukua uamuzi, mgumu kwa vyovyote ulivyo, ili kuleta utulivu wa mfumo."