Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udadavuzi: Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni nini?

Mtazamo wa jumla wa mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu. (Maktaba)
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Mtazamo wa jumla wa mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu. (Maktaba)

Udadavuzi: Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni nini?

Haki za binadamu

Uhalifu wa kivita, ubaguzi wa rangi, kuwekwa kizuizini kiholela na ubakaji kutumika kama silaha ya vita haya ni masuala machache tu ya kimataifa ambayo Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa hujadili.

Kikao chake kipya kilichoanza leo Jumatatu ndicho kirefu zaidi kuwahi kutokea, kitakwenda hadi Aprili, na kina msururu wa ajenda izilizosheheni, ikiwemo vita vinavyoendelea huko Gaza, Sudan na Ukraine, hali ya watetezi wa haki za binadamu duniani kote na zaidi ya rekodi 50 za haki za binadamu za kitaifa zinazochunguzwa.

Lakini, Baraza la Haki za Binadamu linafanya nini na kwa nini kazi yake ni muhimu?

Wakati chombo hicho chenye wanachama 47 kimekuwa mada ya utata tangu kuundwa kwake mwaka 2006 ikiwa ni pamoja na kujiondoa kwa muda kwa Marekani mwaka 2018, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameangazia jukumu muhimu la Baraza katika usanifu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, ambao ni "nguzo ya amani".

Baraza la Haki za Binadamu linafanya nini hasa?

Kwa kifupi, Baraza hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva ni jukwaa la kimataifa kwa ajili ya jumuiya ya kimataifa kujadili jambo lolote linalohusiana na masuala ya haki za binadamu duniani kote.

Mbali na kuzindua operesheni ya kusaka ukweli na kuunda tume za uchunguzi katika hali mahususi zinazotia wasiwasi, hukutana mara tatu kwa mwaka katika ukumbi wa Palais des Nations nchini Uswisi ili kujadili haki mbalimbali za kisiasa, kiraia, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na Umoja wa Mataifa, maafisa, wataalam huru na wachunguzi, nchi wanachama na mashirika ya kiraia.

Linafanyaje kazi?

Kipengele cha ubunifu zaidi cha Baraza la Haki za Kibinadamu ni mapitio ya mara kwa mara ya ulimwengu wote. 

Utaratibu huu wa kipekee unahusisha kuchunguza rekodi za haki za binadamu za nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa mara moja kila baada ya miaka minne. Ni kama kadi ya ripoti ya haki za binadamu ya kitaifa.

Mapitio hayo ni mchakato wa ushirika, unaoendeshwa na serikali chini ya usimamizi wa Baraza hilo, ambao unatoa fursa kwa kila nchi kuwasilisha hatua zilizochukuliwa na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi ili kuboresha hali ya haki za binadamu nchini na kutimiza wajibu wao wa kimataifa.

Baraza pia huunda majopo ya uchunguzi ili kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi na maeneo mahususi, kwa mfano, utaratibu wa kitaalamu wa kuendeleza haki ya rangi na usawa katika utekelezaji wa sheria.

Ili kuchunguza na kufuatilia ukiukaji, Baraza huteua wataalam huru ikiwa ni pamoja na wawakilishi maalum, ambao hufanya kazi kwa nafasi zao binafsi na hawapati malipo yoyote kutoka kwa Umoja wa Mataifa kwa kazi yao. Wakati mwingine huitwa "macho na masikio" ya Baraza hilo.

Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu linasema kila mtu ana haki ya kupata elimu
© UNICEF/Ahmed Haleem
Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu linasema kila mtu ana haki ya kupata elimu

Je, HRC inaleta mabadiliko gani kwa haki za binadamu duniani?

Ingawa haki za binadamu daima zimekuwa suala nyeti sana kwa nchi wanachama, Baraza la Haki za Binadamu linasalia kuwa sehemu muhimu ya usanifu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Baraza lina uwezo wa kupitisha maazimio, kuzindua operesheni za kutafuta ukweli na uchunguzi na kuunda tume za uchunguzi.

Hasa, Baraza linaweza kuteua wataalam wa huru kwa ajili ya masuala maalum. Kwa mfano, mwaka 2023, Baraza lilimteua Mmwakilishi maalum wa kwanza kabisa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Urusi na mnamo 2021, lilitambua kwa mara ya kwanza haki ya mazingira safi na salama kama haki ya binadamu.

Taratibu hizi zote zinaruhusu ukiukwaji mkubwa kuangaziwa na kuletwa kwenye jukwaa la kimataifa kwa ajili ya uchunguzi, majadiliano na, wakati wowote inapowezekana, hatua. 

Kitendo kama hicho kinaweza kubadilisha mwendo wa matukio.

Mjumbe akipigia kura nchi yake wakati wa upigaji kura kuchagua wanachama wapya 18 wa Baraza la Haki za Binadamu, HRC. (Maktaba)
UN /Manuel Elias
Mjumbe akipigia kura nchi yake wakati wa upigaji kura kuchagua wanachama wapya 18 wa Baraza la Haki za Binadamu, HRC. (Maktaba)

Nani anaweza kuhudumu katika Baraza la Haki za Binadamu?

Uchaguzi wa Baraza hufanyika kila mwaka kwa kura ya siri. Nchi zinahudumu kwa miaka mitatu kwa mzunguko, kwani baadhi ya viti huisha tarehe 31 Disemba kila mwaka. Kuna viti 47, vilivyogawanywa kwa usawa kulingana na kanda tano.

Kwa vile inaeleweka kwamba Baraza linaweza kuwa na ufanisi sawa na nchi wanachama wake, mchakato wake wa uchaguzi uliwekwa moja kwa moja mikononi mwa Baraza Kuu, chombo pekee cha Umoja wa Mataifa ambapo kila moja ya nchi 193 wanachama ina uzito sawa wa kupiga kura.

Mgawanyiko wa vikundi vya kijiografia na ugawaji wa viti unakusudiwa kuzuia mwelekeo usio na uwiano katika kanda na nchi chache tu na kuhakikisha kuwa kila nchi inatathminiwa kwa haki.

Ni juu ya nchi wanachama wenyewe kuchagua nchi zinazohudumu, kupitia uchaguzi, kinyume na kuzingatia rekodi za haki za binadamu za nchi yoyote.

Nani anahudumia sasa?

Kwa kura ya siri tarehe 10 Oktoba 2023, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilizichagua Albania, Brazil, Bulgaria, Burundi, China, Côte d’Ivoire, Cuba, Jamhuri ya Dominika, Ufaransa, Ghana, Indonesia, Japan, Kuwait, Malawi na Uholanzi.

Kufikia tarehe 1 Januari, nchi 15 zilizochaguliwa hivi karibuni zilianza kutumikia mihula ya miaka mitatu.

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, akizungumza katika Baraza la Haki za Kibinadamu mnamo 2018.
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, akizungumza katika Baraza la Haki za Kibinadamu mnamo 2018.

Hiki ndicho kinachoendelea katika Baraza la Haki za Kibinadamu sasa

Kikao cha 55 cha HRC kimefunguliwa Jumatatu na kitaendelea hadi 5 Aprili. Kikiongozwa na rais Omar Zniber, kitahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, rais wa Baraza Kuu Dennis Francis na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Volker Türk pamoja na maafisa wakuu kutoka nchi wanachama wakati wa sehemu yake ya ngazi ya juu.

Haya ndio unahitaji kujua:

• Tarehe 4 Machi, Kamishna Mkuu atatoa taarifa yake ya kimataifa, akiangazia hali ya haki za binadamu katika nchi mbalimbali, akizingatia hasa maeneo muhimu.

• Katika kipindi chote, wajumbe watajadili ripoti nyingi za mada na za nchi.

• Mada za majadiliano zitashughulikia hali ya Ukraine na ukiukaji unaosababishwa na uvamizi wa kijeshi wa Urusi.

• Pia nchi zitakazotathiminiwa ni Venezuela, Iran, Colombia, na hali katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.

Huku kikao kikiahidi majadiliano na vitendo vikali vinavyolenga kushughulikia masuala ya haki za binadamu duniani kote.