Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Huku wanakimbia vita wanawake wa Gaza inakuwaje wakiwa katika hedhi?

UNFPA na wadau waendelea kutoa baadhi ya huduma za kuokoa maisha kwa wanawake wajawazito
© PMRS Gaza
UNFPA na wadau waendelea kutoa baadhi ya huduma za kuokoa maisha kwa wanawake wajawazito

Gaza: Huku wanakimbia vita wanawake wa Gaza inakuwaje wakiwa katika hedhi?

Wanawake

Kunapozuka mizozo na machafuko wananchi wote wanaathirika kwasababu maisha yao yanaparanganyika kabisa tofauti na walivyokuwa wamezoea. Watoto waliokuwa wakienda shule sasa hawaendi, si wafanyabiashara, wakulima wala viongozi wa dini wanaotekeleza majukumu yao ya kila siku na suala moja lililo kweli kwa kila mtu ni kuwa wanatafuta kila namna ya kuokoa maisha yao na wengi njia hiyo huwa ni kukusanya virango vyao kidogo wanavyoweza kubeba na kukimbia kuokoa nafsi zao. 

Kwa wananchi wa Gaza hususan wanawake wa Gaza, mwezi Oktoba mwaka 2023 mpaka leo wamekuwa wakikimbia mara kusini, mara kaskazini na sasa wapo Rafah karibu na mpaka wa nchi yao na Misri huku wengine wakiwa wamekwama maeneo mbalimbali ya ukanda huo kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya wanamgambo wa kipalestina wa Hamas na jeshi la Israel IDF. Lakini ki baiolojia kila mwezi wanawake na wasichana waliovunja ungo huona siku zao au huingia katika hedhi , je wanawezaje kujihifadhi wakati huo huo wakiwa leo hapa kesho pale kuokoa nafsi zao? 

Takwimu zilizotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, katika Ukanda wa Gaza kuna zaidi ya wanake na wasichana walio balehe ambao wapo kwenye hedhi 690,000. Watu wote hawa mbali na kukabiliwa na changamoto za wananchi wote za uhaba wa maji safi na kujisafi, huduma za choo na faragha juu ya yote hayo wana ufikiaji mdogo wa taulo za kike. 

Bi Bakiza Mohammed Rahman Nasrallah anatuambia yeye na mtoto wake wakike wanafanyaje kujisitiri kila mwezi.“Nina binti, ana miaka 16, nikitaka kumnunulia taulo za kike ilinigharimu Shekels 10 mpaka 15 ambazo ni zaidi ya dola 4, nawakati hapo awali taulo za kike zilikuwa takriban dola senti 50 embu angalia bei ilivyopanda.? Kwahiyo tunapokuwa na mahitaji inabidi tukate kipande cha nguo na kutumia, maana tutafanya nini sasa? Lipi bora tunaloweza kufanya? Mimi ni mjane, sina mtoto wa kiume na nina binti ambaye mume wake amefariki. Kwahiyo ninararua vipande vya kitambaa ili kujihifadhi mie na binti yangu. Binti yangu aliniambia, "Mama, siwezi kufanya hivi!" Lakini sasa mie nitafanya nini?”

UNFPA imejitahidi kufikia maelfu ya wanawake na wasichana na kuwapatia mahitaji hayo muhimu.

Video ya UNFPA inaonesha makazi ya wakimbizi ya Al- mawasi, wafanyakazi wa ‘Chama cha Utamaduni na Mawazo Huru’ (CFTA) ambao ni washirika wa UNFPA wakiwa na mabegi ya buluu wakipita katika mahema na kukabidhi mabegi hayo kwa wanawake. 

Fahima Ebeid ni mratibu wa mradi wa UNFPA wanaoshirikiana na CFTA na anaeleza nini kimo kwenye begi “Kama unataka kujua yaliyomo basi tuanzie na nguo kwa ajili ya kuswali, alafu kuna nguo za ndani maana kupatikana sasa hivi ni bei kubwa na wanawake hawawezi tena kumudu. Kuna taulo za kike ambazo nazo ni gharama kwelikweli na ni bidhaa muhimu kwa wanawake kila mwezi. Pia tumewawekea sabuni na ndala maana wengi tuliwaona wakitembea na viatu vya wanaume au peku peku. Sabuni za kuosha nywele pia tumeweka maana hazipatikana katika maeneo yote ya ukanda wa Gaza.”

Video ya UNFPA iliendelea kuonesha ugawaji wa mabegi ya buluu ukiendelea kambini hapo. Msichana Farah mwenye umri wa miaka 18 anapewa begi na anashukuru.

“Namshukuru Mola, Kidogo kidogo mambo yanakuwa bora, wanatupa huduma, chakula kidogo, na hivi vitu vinavyohusiana na afya zetu. Kwa mfano kwenye hili begi kuna shampoo sabuni ya kuosha nywele, tuna suruali za kusaidia kutupa mwili joto maana tupo karibu na baharí na tunaishi katika mahela kuna muda kuna upepo mkali na baridi Kali. Hivi ni vitu ambavyo havipatikani kwa kila mtu. Na vitu kama ndala kwa mfano, hazipatikani kamwe, hata ukitaka kuzipata, zitakuwa ghali, na unaweza usizipate kabisa”, amesema Farah.

Mbali na vifaa hivyo UNFPA pia inatoa Msaada wa kuwahamisha na kuwapatia fedha wanawake walio katika mazingira magumu, wakiwemo wajawazito na wanaonyonyesha. UNFPA inawafikia maelfu ya wanawake walio katika hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na kuwapatia Msaada wa kisaikolojia na kijamii, afya, ulinzi, na usafi katika makazi, pamoja na kuwezesha huduma ya kwanza kupitia vijana wa kujitolea. 

Lakini yote haya ni tone tu katika baharí ya hamitaji ya wananchi wa Gaza ambao kubwa wanaloliomba ni usitishaji wa mapigano kwa sababu za kibinadamu.