Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katu hedhi isiwe mwiko, mnahatarisha afya ya wanawake na wasichana- Wataalamu

Wanawake wahubiri wa dini ya kiislamu nchini Chad wakiwafundisha wasichana kuhusu hedhi kupitia mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa huko mjini Bol. (Picha hii ni ya Februari 2019)
UN/Eskinder Debebe
Wanawake wahubiri wa dini ya kiislamu nchini Chad wakiwafundisha wasichana kuhusu hedhi kupitia mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa huko mjini Bol. (Picha hii ni ya Februari 2019)

Katu hedhi isiwe mwiko, mnahatarisha afya ya wanawake na wasichana- Wataalamu

Wanawake

Wataalamu 7 wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa jamii ya kimataifa iondokane na mwiko unaozingira suala la afya ya hedhi na badala yake ichukue hatua kuhakikisha fikra baguzi dhidi ya suala hilo zinabadilishwa na afya ya hedhi kwa wanawake na wasichana inalindwa.

Kilio cha wataalamu hao kuhusu masuala ya wanawake kimo kwenye taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, kuelekea siku ya wanawake duniani tarehe 8 mwezi huu wa Machi, wakisema kuwa mila, unyanyapaa, miiko na fikra potofu kuhusu hedhi vimeendelea kuwatenga na kuwabagua wanawake.

Wamesema unyanyapaa na fikra potofu dhidi ya hedhi vimekuwa na madhara kwa haki za binadamu za wanawake na wasichana  ikiwemo usawa, afya,  makazi, malazi, huduma za kujisafi, elimu, Imani ya dini, kufanya kazi na kushiriki kwenye shughuli za umma.

Katika baadhi ya nchi, wanawake na wasichana walio kwenye hedhi wanaonekana kuwa ni wachafu, hawana udhu na wanawekewa vikwazo kama vile kushika maji, kupika au hata kushiriki kwenye sherehe za kidini, kijamii au kitamaduni,” wamesema wataalamu hao.

Wameendelea kusema kuwa, “wasichana walio kwenye hedhi wanaweza hata kufungiwa nje ya nyumba na kuishi kwenye upweke na uhai wao unakuwa uko mashakani n ahata wanaweza kushambuliwa na Wanyama hatari. Inapochanganywa na unyanyapaa na aibu, wanawake na wasichana wakati wa kipindi hicho wanapata hisia ya kwamba wao hawana thamani yoyote.”

Pamoja na mazingira hayo ya kutengwa, wanawake na wasichana bado wanakumbwa na shida nyingine, ambapo wataalamu hao wamesema ni taulo za kike sambamba na mazingira bora ya kuweza kujihudumia iwe shuleni au kazini na hivyo kusababisha kuongeza pengo la usawa wa jinsia.

Wataalamu hao wamesema wakati baadhi ya nchi zimeshaharamisha vitendo baguzi dhidi ya masuala ya hedhi na kutunga sera rafiki za kulinda wanawake na wasichana wakati wa hedhi, bado kwenye maeneo mengi ya nchi duniani wanawake wanapuuzwa.

Wametaka hatua zaidi zichukuliwe kushughulikie afya ya hedhi kwa wanawake na wasichana na kwamba kwa kutofanya hivyo kutaathiri kundi hilo hasa wale wanaoishi vijijini.

Wataalamu hao ni Ivana Radačić, Karima Bennoune, Dainius Pūras, Koumbou Boly Barry, Léo Heller, Dubravka Šimonovic na Surya Dev