Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yahimiza matumizi ya lugha mama kwenye ufundishaji

Wanafunzi wakiwa darasani nchini Colombia.
UNESCO/Ministerio de Educación, Colombia
Wanafunzi wakiwa darasani nchini Colombia.

UNESCO yahimiza matumizi ya lugha mama kwenye ufundishaji

Utamaduni na Elimu

Tarehe 21 Februari kila mwaka ulimwengu unaadhimisha siku ya lugha mama ambayo mwaka huu Kali mbiu yake ni “Elimu ya Lugha nyingi ni nguzo ya kujifunza kati ya vizazi.” 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO hivi sasa asilimia 40 ya idadi ya watu duniani hawana fursa ya kupata elimu katika lugha wanayozungumza au kuelewa. Katika baadhi ya nchi takwimu hii inaongezeka hadi zaidi ya asilimia 90. 

Bado utafiti unaonesha kuwa matumizi ya lugha za kujifunzia kwa wanafunzi shuleni hutoa msingi thabiti wa kujifunza, huongeza kujiamini na ujuzi wa kufikiri kwa kina, na kufungua mlango wa kujifunza kati ya vizazi, kuhuisha lugha, na kuhifadhi utamaduni na urithi usioonekana. 

UNESCO wanasema maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yanalenga kuangazia umuhimu wa kutekeleza sera na mazoea ya elimu kwa lugha nyingi kama nguzo ya kufikia Lengo namba 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs linalohimiza Elimu Bora. 

Lengo hili linataka elimu jumuishi, bora na kujifunza kwa maisha yote kwa wote na vile vile kwa malengo ya Muongo wa Kimataifa wa Lugha ya asili (2022 - 2032). 

Shirika hilo linawaleta pamoja wataalam wa elimu ya utotoni, kusoma na kuandika, ujifunzaji usio rasmi na lugha za kiasili ambao watajadili jinsi sera na mazoea ya elimu kwa lugha nyingi yanaweza kutekelezwa ili kuhakikisha ujifunzaji mjumuisho, bora kwa yale yote ambayo yanaboreshwa sio tu matokeo ya ujifunzaji lakini uwasilishaji wa maarifa, lugha, utamaduni kati ya vizazi na urithi usioonekana.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani maadhimisho ya siku hii yanakutanisha Mabalozi wa Kudumu wa Austria, Bahrain, Bangladesh, Bolivia, Romania, na Afrika Kusini wakishirikiana na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa na UNESCO kwenye hafla ya kujadili masuala muhimu ya lugha mama  na matangazo yake yanarushwa mubashara tarehe 21 Februari. 2024 saa 10:00 hadi 6:00 jioni katika Chumba cha Mkutano na mubashara https://webtv.un.org/en/asset/k1w/k1w2te2nrh  lugha tatu zitatumika katika hafla hiyo ambazo ni Kingereza, kifaransa na kihispania pamoja na uwepo wa watafsiri wa lugha nyingine mbalimbali ikiwemo kichina, kirusi na kiarabu.