Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jazz ni ladha ya uhuru wetu, utofauti wetu na utu wetu:Guterres 

Kutoka Maktaba: Hugh Masekela akitumbuiza katika uzinduzi wa siku ya kimataifa ya Jazz kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa New York, 30 Aprili 2012
UN Photo/JC McIlwaine
Kutoka Maktaba: Hugh Masekela akitumbuiza katika uzinduzi wa siku ya kimataifa ya Jazz kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa New York, 30 Aprili 2012

Jazz ni ladha ya uhuru wetu, utofauti wetu na utu wetu:Guterres 

Utamaduni na Elimu

Siku ya kimataifa ya Jazz ikiadhimishwa leo kote duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maadhimisho hayo yamekuwa faraja na furaha sio tu kwa kuenzi muziki huo bali kwa uhuru, utofauti wetu na utu wa binadamu.

 Kupitia ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu amesema “Haya ni maadili ambayo Umoja wa Mataifa unafanyakazi kuyalinda na kuyachagiza duniani kote. Tangu kuzinduliwa kwake muziki wa Jazz umekuwa daraja la kuunganisha wengi na jukumu lake la kihistoria la kupambana na ubaguzi na ubaguzi wa rangi linaendelea kuunganisha tamaduni mbalimbali kote duniani.” 

Bwana Guterres ameongeza kuwa mirindimo na miondoko yake inaonyesha utu wa kibinadamu usiyoweza kushindwa na ambao unaweza kuvuka mipaka iliyowekwa na umaskini na uonevu. 

Mkazo wake wa kuhusu masuala ya usawa huwapa wanamuziki uhuru wa ubunifu kama watu binafsi wakati wa kufanya matamasha na maonyesho kama sehemu ya sauti ya jamii. 

Ni wajibu wa kila mtu kudumisha amani na utangamano 

 Hivyo amesisitiza kwamba “Sote tunaweza kushiriki katika furaha na changamoto ya aina hii ya kipekee ya sanaa. Leo hii wakati wa janga la kimataifa la CVOVID-19 wasanii na wafanyikazi wanaotegemea sanaa ya ubunifu wanateseka. Ni muhimu turejeshe jamii zetu mahiri kuwa salama, zenye usawa na haraka iwezekanavyo.” 

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema katika “Siku hii, tunakumbushwa jinsi jazz inavyoweza kutoa tumaini, uponyaji na nguvu tunapofanya kazi ya kuujenga ulimwengu bora na wenye amani.” 

 Kwa muongo mmoja uliopita, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, limekuwa likitangaza ujumbe huu wa siku ya Jazz kote duniani. 

 Guterres amehitimisha ujumbe kwake kwa kusema “Katika maadhimisho haya ya miaka kumi, hebu tuungane tena kusherehekea ari na maadili ya jazz.”