Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la kinibadamu DRC lahitaji dola bilioni 2.6 mwaka 2024: OCHA

Mvulana akiwa ameketi katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani Goma jimbo la Kivu Kaskazini
© UNICEF/Jospin Benekire
Mvulana akiwa ameketi katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani Goma jimbo la Kivu Kaskazini

Janga la kinibadamu DRC lahitaji dola bilioni 2.6 mwaka 2024: OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na jumuiya ya misaada ya kibinadamu leo ​​wamezindua ombi la dola bilioni 2.6 za kimarekani ili kufadhili mpango wa misaada ya kibinadamu wa mwaka huu wa 2024 nchini humo.

Ofisi ya Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa OCHA nchini humo imesema fedha hizo zitatumika kutoa msaada wa kuokoa maisha na huduma za ulinzi kwa watu milioni 8.7 DRC ambao maisha yao yanategemea zaidi msaada wa dharura.

OCHA inasema kwa zaidi ya mwaka mmoja, mgogoro wa kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC umefikia viwango vya kutisha.

Na mlipuko mpya wa ghasia, hasa mashariki mwa nchi, unalazimisha watu walioathiriwa kuhama mara kwa mara. 

Mama mkimbizi wa ndani akibeba kuni. anayeishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani kwenye kambi za wakimbizi Ituri, DRC.
UN News
Mama mkimbizi wa ndani akibeba kuni. anayeishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani kwenye kambi za wakimbizi Ituri, DRC.

Idadi ya wakimbizi inaongezeka

Kwa mujibu wa OCHA kwa sasa DRC ina wakimbizi wa ndani milioni 6.7, na wengine kwa mamilioni wamekimbilia nchi jirani kusaka usalama.

Wakati huo huo nchi hiyo pia inakabiliwa na mafuriko makubwa na kuibuka tena kwa magonjwa ya kuambukiza kama surua na kipindupindu, ambayo yamezidisha hatari ya watu walioathiriwa na zaidi ya miongo mitatu ya vita ya kutumia silaha.

Mbali ya changamoto zote hizo OCHA inasema mgogoro wa DRC ni miongoni mwa migogoro mikubwa duniani ambayo haijafadhiliwa vya kutosha huku mamilioni ya watu nchini humo wakitegemea msaada kuweza kuishi hali ambayo inaweza rehani sio tu Maisha ya watu hao bali pia uwezo wao wa kuishi.

Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC
© WFP/Michael Castofas
Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC

Changamoto ya ufadhili

Kwa mujibu wa Bruno Lemarquis mratibu wa masuala ya kibinadamu wa umoja wa Mataifa nchini DRC mwaka jana 2023, ombi la ufadhili kwa ajili ya nchi hiyo ilifadhiliwa kwa asilimia 40 pekee. 

Amesema “Hii imesaidia zaidi ya watu milioni 5, lakini mahitaji mengi bado hayajafikiwa. Na hali hii inasababisha mateso mengi, majanga ya kibinadamu, kupoteza maisha. Vitu vingi vya muda mfupi ambavyo athari zake hudumu kwa muda mrefu sana. Watu wanataka kurejea nyumbani na kurejea katika maisha ya kawaida.” 

Ameongeza kuwa zaidi ya watoto milioni moja hawaendi shule tena kutokana na migogoro ya kivita. 

Naye Modeste Mutinga Mutushayi, Waziri wa Masuala ya Kijamii, Misaada ya Kibinadamu na Mshikamano wa Kitaifa amesema “Hali ni mbaya sana. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuangalia upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kwa uwezo wake wa kipekee duniani katika ngazi ya mazingira, katika ngazi ya uchimbaji madini na katika ngazi ya utalii, Congo inaweza kuleta mengi duniani. Inachohitaji ni kupata Amani.”