Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita ya Ukraine isipokoma na hatua kuchukuliwa wimbi la watoto wataaga dunia Pembe ya Afrika:UNICEF

Mtoto akipokea matibabu ya lishe katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF, Somali, Ethiopia.
© UNICEF/Zerihun Sewunet
Mtoto akipokea matibabu ya lishe katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF, Somali, Ethiopia.

Vita ya Ukraine isipokoma na hatua kuchukuliwa wimbi la watoto wataaga dunia Pembe ya Afrika:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Naibu mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Rania Dagash ameonya leo kwamba "Janga la vifo vya watoto liko karibu kutokea katika Pembe ya Afrika endapo dunia itajikita na vita ya Ukraine na kuyapa kisogo majanga mengine ikiwemo Pembe ya Afrika"

Katika tarifa yake iliyoitolewa leo mjini Geneva Uswis Dagash amesema "Takriban watoto 386,000 nchini Somalia sasa wanahitaji haraka matibabu kutokana na utapiamlo mkali au unyafuzi unaotishia maisha yao, sasa idadi hiyo ikizidi ya watoto 340,000 ambao walihitaji matibabu wakati wa njaa ya 2011. Idadi ya watoto wanaokabiliwa na aina hii hatari zaidi ya utapiamlo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 15 katika muda wa miezi mitano.”

Ameongeza kuwa kote Ethiopia, Kenya na Somalia, zaidi ya watoto milioni 1.7 wanahitaji matibabu ya haraka kutokana na utapiamlo uliokithiri.

Amesema kumekuwa na misimu duni ya minne ya mvua ndani ya miaka miwili ambayo imesababisha wanyama kufa, mimea kukauka na kukausha vyanzo vya maji, huku utabiri wa hali ya hewa ukisema mwezi Oktoba na Desemba huenda mvua ikawa dunia pia.

Kiwango cha utapiamlo

Kwa mujibu wa UNICEF nchi zote tatu zimerekodi idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo mkali ambao wamelazwa wakipatiwa matibabu katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2022 ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka 2021.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Eyhiopia watoto waliolazwa ni asilimia 27 zaidi , huku Somalia ikilinganishwa na mwaka jana ni asilimia 48 zaidi nako Kenya idadi ya watoto waliolaza ni asilimia 71 zaidi.

Shirika hilo linasema idadi ya vifo pia inatia wasiwasi mkubwa kwani mwaka huu katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ukame kwenye Pembe ya Afrika idadi ya watoto ambao wameshakufa na utapiamlo mkali katika vituo vya matibabu ikilinganishwa na mwaka jana.

Rania Dagash, naibu mkurugenzi wa UNICEF Kusini na Mashariki mwa Afrika (Kushoto) akikutana na mama wa watoto wmapacha wanaougua utapiamlo kwenye kituo cha afya cha Dollow Somalia
© UNICEF/Omid Fazel
Rania Dagash, naibu mkurugenzi wa UNICEF Kusini na Mashariki mwa Afrika (Kushoto) akikutana na mama wa watoto wmapacha wanaougua utapiamlo kwenye kituo cha afya cha Dollow Somalia

Kuhusu maji

UNICEF inasema kati ya mweszi Februari na Mei mwaka huu idadi ya kaya ambazo hazina fursa ya uhakika ya maji safi na salama imeongezeka karibu mara mbili.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi hiyo imeonhgezeka kutoka watu milioni 5.6 hadi watu milioni 10.5.

Vita ya Ukraine

Bi. Dagash amesema Maisha ya watoto wa Pembe ya afrika yanaendelea kuwa katika hatari kubwa kwa sababu ya vita ya Ukraine, mathalani amesema Somalia pekee huingiza asilimia 92 ya ngano yake kutoka Urusi na Ukraine na sasa mnyororo wa usambazaji imekwama.

Ameongeza kuwa vita hiyo pia imechochea ongezeko la bei ya chakula na mafuta kote duniani na hii ikimaanisha watu wengi nchini Ethiopia, Kenya na Somalia hawawezi tena kumudu bidhaa za msingi za chakula wanachohitaji ili kuishi.

“Shinikizo hili pia linaathiri hatua zetu za msaada . Gharama zinazotumiwa na UNICEF kununua chakula cha tiba kwa watoto wenye utapiamlo mkali zinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 16 katika miezi sita ijayo nah ii inamaanisha UNICEF itahitaji takribani dola milioni 12 zaidi kuliko ilivyotarajiwa ili kuisaidia Pembe ya afrika pekee.”

Ibrahim mtoto wa miezi 8 anayeugua utapiamlo akifanyiwa vipimo katika hospitali ya Moghadishu Somalia
© UNICEF/Omid Fazel
Ibrahim mtoto wa miezi 8 anayeugua utapiamlo akifanyiwa vipimo katika hospitali ya Moghadishu Somalia

Ufadhili

UNICEF na mashirika mengine wamekuwa wakipiga kengele ya tahadhari kuhusu mgogoro wa ufadhili. “Tunawashukuru sana wafadhili ambao wamechagia , ni msaada wao ambao umetuwezesha kuchukua hatua za msaada ambazo tumeweza kuzichukua hadi sasa . Lakini ombi letu bado halijafadhiliwa vya kutosha tulichopata ni chini ya theluthi moja ya fedha tunazohitaji.” Ameongeza kusema Bi.Dagash.

Amehitimisha taarifa yake akisema “watoto wengi hawatoweza kuhimili hali hii , tumesikia watoto wengine wameziikwa kando ya barabara wazazi waimo wakijaribu kufanya safari za kwenda kusaka usalama na uhakika wa chakula na msaada mwingine muhimu. Na hofu yetu ni kwamba hali mbaya zaidi iko njiani.”