Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC yapongezwa kwa kuanzisha Bunge la watoto na mkataba wa ulinzi kwa watoto

Meja Sherihan kutoka Misri akiwa na watoto nchini DRC. (Maktaba)
MONUSCO
Meja Sherihan kutoka Misri akiwa na watoto nchini DRC. (Maktaba)

DRC yapongezwa kwa kuanzisha Bunge la watoto na mkataba wa ulinzi kwa watoto

Haki za binadamu

Kamati ya Haki za Mtoto ya Umoja wa Mataifa CRC hii leo imetoa matokeo yake kuhusu utafiti waliofanya katika nchi sita ambazo ni Jamhuri ya kidemocrasia kongo DRC, Bulgaria, Lithuania, Urusi, Senegal na Afrika Kusini, baada ya kufanya uhakiki wanchi hizo katika kikao chake cha hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa hii leo na ofisi ya umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu OHCHR kutoka Geneva Uswisi imenukuu kamati hiyo ikiipongeza nchi ya DRC kwa kuanzisha bunge la watoto na kuidhinishwa kwa Mkataba wa The Hague wa Ulinzi wa Watoto na Ushirikiano kuhusiana na Kuasili kwa Nchi Mbalimbali. 

Kamati, kwa upande mwingine, ilikuwa na wasiwasi kwamba idadi kubwa ya watoto nchini Jamhuri ya kidemokrasia Kongo walikuwa hawajaandikishwi wakati wa kuzaliwa. 

Taarifa hiyo imesema kamati imeiomba Serikali ya DRC kufuta ada zote zisizo rasmi za usajili wa kuzaliwa, kupanua upatikanaji wa usajili, kuongeza muda wa mwisho wa kujisajili, na kuongeza ufahamu wa umuhimu wa usajili kwa wananchi wake.

Ajira za utotoni

Kamati hiyo ya haki za watoto pia imeeleza wasiwasi wake kwamba watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 wanajishughulisha na shughuli za kiuchumi licha ya mambo hayo kukatazwa na Katiba. 

Kamati ilitoa tahadhari kuhusu watoto wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi kama vile uchimbaji wa madini ya dhahabu, machimbo mengine, na maeneo ya upangaji wa taka na dampo.

Kamati hiyo imeitaka DRC kutekeleza ukomo wa umri wa kikatiba wa kuajiriwa kwa watoto na kuhakikisha inaondoa kabisa ajira za watoto katika uchimbaji wa madini, machimbo mengine, maeneo ya upangaji taka na dampo na aina nyingine za ajira za watoto.

Kusoma ripoti za nchi nyingine ambazo ni Afrika Kusini, Bulgaria, Urusi, Senegal na Lithuania bofya hapa.

Kamati ya Haki za Mtoto (CRC) ni chombo cha wataalam 18 huru ambao hufuatilia utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Mtoto na Mataifa yake. Pia kamati hiyo inafuatilia utekelezaji wa Itifaki za Chaguo za Mkataba, juu ya ushiriki wa watoto katika migogoro ya silaha na uuzaji wa watoto, ukahaba wa watoto na video za ponografia kwa watoto.