Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Wanaodhaniwa waasi wa M23 washambulia helikopta ya Umoja wa Mataifa jimboni Kivu Kaskazini

Picha kutoka maktaba: Helikopta ya MONUSCO ikitua Beni katika eneo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
UN Photo/Michael Ali
Picha kutoka maktaba: Helikopta ya MONUSCO ikitua Beni katika eneo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

DRC: Wanaodhaniwa waasi wa M23 washambulia helikopta ya Umoja wa Mataifa jimboni Kivu Kaskazini

Amani na Usalama

Mapema leo Februari pili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wa kundi lenye silaha la M23 wameishambulia moja ya helikopta za Umoja wa Mataifa, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umeeleza.

Kwa mujibu wa maelezo kwa waandishi wa Habari, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric hii leo jijini New York, Marekani, tukio hilo la kushambuliwa kwa helikopta ya Umoja wa Mataifa limefanyika katika eneo la Karuba katika jimbo la Kivu Kaskazini, katika eneo la Masisi, mashariki mwa nchi. 

Majeruhi

Tukio hilo limesababisha majeraha kwa walinda amani wawili wa Afrika Kusini, akiwemo mmoja aliyejeruhiwa vibaya. Helikopta hiyo iliweza kutua salama mjini Goma, na walinda amani hao kwa sasa wanapokea matibabu.

Nembo ya Umoja wa Mataifa

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambaye pia ni Mkuu MONUSCO, Bintou Keita, amelaani vikali shambulio dhidi ya ndege yenye nembo ya Umoja wa Mataifa, ambalo linakuja karibu mwaka mmoja baada ya shambulio kama hilo lililosababisha kifo cha askari wa kulinda amani wa Afrika Kusini.

Bi.Keita amekumbushia kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa uhalifu wa kivita. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa hautaacha juhudi zozote, kwa ushirikiano na mamlaka ya DRC, kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Wakuu wengine wa UN wako DRC

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Dujarric akiendelea kuzungumza na waandishi wa Habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, amesema, “wakati huo huo, mkuu wa idara yetu ya ulinzi wa amani, “Jean-Pierre Lacroix, akiungana na Catherine Pollard, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Mkakati wa Usimamizi, Sera na Uzingatiaji, pamoja na Christian Saunders, Mratibu Maalum wa Kuboresha Mwitikio wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Unyanyasaji wa kingono na Kijinsia wote wako DRC. Wamefika Beni, Kivu Kaskazini, leo, ambapo wataendelea na ziara yao katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.