Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UDADAVUZI: Fahamu saratani ya shingo ya kizazi

Hospitali ya Kanda ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza kaskazini magharibi mwa Tanzania.
UN News
Hospitali ya Kanda ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza kaskazini magharibi mwa Tanzania.

UDADAVUZI: Fahamu saratani ya shingo ya kizazi

Afya

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ambayo hutokana na mabadiliko ya mfumo wa chembechembe au seli zilizoko katika shingo ya kizazi wengine wakiita mlango wa kizazi. 

Saratani hii huathiri shingo ya kizazi ambayo ni sehemu ya chini ya mfuko wa kizazi, ambapo kwa kawaida huonekana pale tu mwanamke anapolala chali na inaweza kuonekana kupitia uke. 

Kwa mujibu wa WHO ulimwenguni kote saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ya nne kwa kuathiri wanawake, ikiwa na wagonjwa wapya 604,000 mnamo 2020. 

Takriban asilimia 90 ya vifo 342,000 vilivyosababishwa na saratani ya shingo ya kizazi vilitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati. Viwango vya juu zaidi vya saratani hiyo na vifo ni kutoka Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Amerika ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia. 

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa kila mwaka Tanzania ina wagonjwa wapya wa saratani 42,000 ambapo wagonjwa hao wapya wanaofika kwenye vituo vya afya ni takribani 15, 900 tu. 

Ripoti za utafiti wa kisayansi zimeafiki kuwa saratani za shingo ya kizazi hutokana na maambukizi ya virusi vya 'Human Papillomavirus' au HPV vilivyoko katika jamii ya papilloma.  

Virusi vya Papiloma

Virusi aina ya Human Papiloma (HPV) ni maambukizi ya kawaida ya zinaa ambayo yanaweza kuathiri ngozi, sehemu za siri na koo, takriban watu wote wanaofanya ngono wataambukizwa wakati fulani wa maisha yao, kwa kawaida bila dalili.  

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na mkufunzi wa kitaifa wa saratani ya shingo ya kizazi Dkt. Amina Jumanne Yusuph, anasema “Virusi hivi huambukizwa kwa njia ya kujamiiana, kwa hiyo hatuwezi kujua uliyejamiiana naye ana maambukizi au hana”.

“Mtu yeyote ambaye amewahi kujamiiana, karibia 80% ya watu wote, wamewahi kuambukizwa mara moja au mara mbili, kwasababu kinaambukizwa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi 

Kwenda kwa mtu asiye na maambukizi”, amesema Dkt, Amina. 

Dkt, Amina anasema kwamba mwanaume anaweza akakichukua kirusi hicho kutoka kwa mwanamke mwenye tatizo hilo, lakini mwanaume hawezi kuugua saratani kwasababu wao hawana mlango wa kizazi. 

“Mwanaume anaweza kuwa amejamiiana na wanawake wengi, miongoni mwao mwanamke mmoja akiwa na kirusi kuna uwezekano wa kuwaambukiza wengine, lakini siyo lazima wote waugue saratani hii, itategemeana na kinga ya miili yao”, amesema Dkt, Amina. 

Dkt. Amina Jumanne Yussuph, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na mkufunzi wa kitaifa wa saratani ya shingo ya kizazi akizungumza wakati wa mazungumzo na UN News yaliyofanyika katika hospital ya Kanda ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza kaskazini maghar…
UN News
Dkt. Amina Jumanne Yussuph, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na mkufunzi wa kitaifa wa saratani ya shingo ya kizazi akizungumza wakati wa mazungumzo na UN News yaliyofanyika katika hospital ya Kanda ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Dalili zake ni zipi? 

Sababu za hatari zinazoweza kusababisha saratani ni pamoja na kiwango cha aina ya HPV iitwayo oncogenicity ya, hali ya kinga mwilini, uwepo wa magonjwa mengine ya zinaa, idadi ya kuzaa watoto, ujauzito wa kwanza katika umri mdogo, matumizi ya uzazi wa mpango wakutumia homoni, na kuvuta sigara. 

Dkt. Amina anasema kisababishi kikubwa ni kirusi auna ya HPV ambacho iwapo ukiambukizwa na kukaa mwilini kwa muda mrefu kinaweza kuleta shida ya saratani ambapo huanza kuonesha dalili kwa muda wa miaka 10-20. 

“Inachukua muda mrefu mfano, binti akianza kujamiiana akiwa na umri wa miaka 15, maana yake mpaka kuanza kutengeneza mabadiliko ya awali kwenye mlango wake itachukua miaka 10-20, kwahiyo binti huyu ataanza kuonesha mabadiliko ya awali akiwa na miaka 30”. 

Walioko kwenye hatari 

 Kwa mujibu wa Dkt, Amina ni watu wanaoishi na maambukizi ya VVU, wanawake waliobeba mimba na kuzaa Watoto wengi kuanzia watano, wanawake wenye mahusiano na zaidi ya mtu mmoja, anakuwa katika hatari ya kupata maradhi haya

“Mabinti wanaoanza kujamiiana mapema inawaweka katika hatari kwasababu wanakuwa na muda mrefu wa kujamiiana, lakini pia hata wale wanaoishi na maambukizi ya magonjwa ya zinaa pia wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu wa saratani” 

Shuhuda 

“Nilikuwa ninatoka damu usiku na mchana, damu ikaendelea karibia nusu mwaka, mwezi wa kumi na mbili nilipokuja Bugando wakanipima, wakatoa vinyama viwili, majibu yalipotoka wakasema ni saratani ya mlango wa kizazi,” anasema mgonjwa mmoja hapa hospitali ya Kanda Bugando mkoani Mwanza, Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania. 

Mgonjwa mwingine Husna, (si jina lake halisi) ameketi huku kichwa amekiinamisha, yeye ni mkazi wa Sikonge mkoani Tabora magharibi-kati mwa Tanzania, ilimlazimu kusafiri umbali wa kilomita 415.5 zaidi ya saa 6 kufika katika hospital hii, alikuwa tayari kuzungumza nami lakini alishindwa kutokana na kushikwa na kizunguzungu baada ya kutoka kwenye matibabu ya mionzi, hivyo alinipa ruhusa ya kuzungumza na mwanaye. 

Mwanaye huyu anakiri mama yake kupata unafuu baada ya kuanza matibabu ya mionzi “uchunguzi tulikuja kuufanyia hapa, wakampima kinyama cha ndani wakachukua majibu wakasema ana saratani ya mlango wa kizazi, tukaanzishiwa mionzi ya nje na ndani, baada ya kupata matibabu anaendelea vizuri damu imekata, maji maji yalikuwa yanatoka yakiwa na harufu lakini sasa hivi hamna” anasema Dkt. Amina.  

Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.
© UNICEF/Laurent Rusanganwa
Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.

Kujikinga 

Saratani ya shingo ya kizazi yaweza kutibika iwapo itagundulika mapema, Pap Test (Papanicolaous Test); Pap-Smear ni kipimo ambacho hutumika kuchunguza mabadiliko ya chembe zilizoko katika mlango wa kizazi ili kugundua mabadiliko yanayotokea katika chembe hizo na hivyo kuwahi kuyakabili mapema. 

“Kinga kuna chanjo, kinga pekee kabla haujaanza kujamiiana upewe chanjo, tunahamasisha watu waelewe chanjo, kwahiyo mpeleke binti akapate chanjo” anasema Dkt. Amina

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO lilitangaza kuwa mwezi Januari ni mwezi wa kuhamasisha jamii kuhusu satarani ya shingo ya kizazi.  

Wataalam wa afya katika mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania wamekuwa wakitoa elimu ya ugonjwa huo katika jamii na kuhamasisha wanawake kujitokeza katika vituo vya afya vinavyotoa huduma hiyo ili kupima afya zao kujua iwapo wana mabadiliko ya awali, au kuzaniwa kuwa na saratani ya mlango wa kizazi. 

Mkakati wa WHO ni kupunguza idadi ya wagonjwa wapya kila mwaka hadi wanne au pungufu zaidi kwa kila wanawake laki moja na kuweka malengo matatu yatakayofikiwa ifikapo mwaka 2030.