Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapendekezo mapya kuhusu utoaji wa chanjo ya HPV dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi

Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.
© UNICEF/Laurent Rusanganwa
Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.

Mapendekezo mapya kuhusu utoaji wa chanjo ya HPV dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, limeboresha mapendekezo yake kuhusu utoaji wa chanjo ya Human Papilloma Virus, HPV inayosabisha saratani ya shingo ya kizazi, na ambapo sasa itatolewa dozi moja badala ya dozi mbili.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema mpendekezo hayo ya WHO yamo kwenye chapisho lake la wiki iliyopita, na yanatokana na mapendekezo yaliyotolewa na kundi la wataalamu huru washauri kwa WHO mwezi Aprili mwaka huu. 

Mapendekezo yanasema utoaji wa dozi moja ya chanjo unaweza kuwa na ufanisi kama dozi mbili na katika muda ule ule wa kinga dhidi ya virusi hivyo vya HPV. 

Wanafunzi wawili wa shule ya msingi nchini Rwanda wakipatiwa chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi, HPV.
© UNICEF/UN0261446/Rusanganwa
Wanafunzi wawili wa shule ya msingi nchini Rwanda wakipatiwa chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi, HPV.

Utoaji wa chanjo ya HPV umepungua duniani kote 

WHO inasema chapisho hilo na mapendekezo hayo yamekuja wakati muafaka wakati ambapo kumekuweko na shaka na hofu kuhusu kupungua kwa utoaji wa chanjo ya HVP duniani kote. 

“Kati ya mwaka 2019 na 2021, utoaji wa dozi ya kwanza ya chanjo ya HPV ulipungua kutoka 25% hadi 15%. Hii inamaanisha kuwa wasichana milioni 3.5 walikosa chanjo ya HPV mwaka 2021 ikilinganishwa na mwaka 2019,” imesema taarifa hiyo. 

Ni kwa mantiki hiyo WHO inasema ratiba bora ya utoaji wa chanjo na kupunguza dozi kutaongeza upatikanaji wa chanjo, na kutoa fursa kwa nchi kupanua wigo wa idadi ya watoto wa kike wanaopatiwa chanjo na wakati huo huo kupunguza mzigo wa gharama za fedha zinazohitajika kununua chanjo za ziada kwa awamu ya pili ya chanjo. 

Mapendekezo ya WHO 

Kwa watoto wa kike wenye umri wakati ya miaka 9 hadi 14 wapatiwe dozi moja au mbili, halikadhalika wasichana na wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 20 nao wapatiwe dozi moja au mbili. 

Hata hivyo kwa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 21 wao wapatiwe dozi mbili; ambapo akishapatiwa ya kwanza, ya pili apatiwe baada ya miezi sita. 

Walio na kinga kidogo wapatiwe kipaumbele 

Chapisho hilo linataka wale walio na kinga kidogo mwilini wapatiwe kipaumbele katika kupata chanjo hiyo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, wakiwemo wale wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, na hao wapatiwe chanjo mbili au hata ikiwezekana tatu. 

Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi
PAHO/WHO
Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi

Walengwa wakuu watoto wa kike 9-14 

Mapendekezo hayo yanaweka bayana kuwa walengwa wakuu wa chanjo ya HPV ni watoto wa kike kuanzia umri wa miaka 9 hadi 14; kabla hawajaanza kujamiiana, na kwamba utoaji chanjo kwa walengwa wengine wasio wa msingi, wakiwemo wavulana na wanawake watu wazima unapendekezwa pale ambapo inawezekana . 

Saratani ya shingo ya kizazi inashika nafasi ya nne kati saratani zinazoongoza zaidi kupata wanawake, na 95% ya maambukizi ni virusi hivyo HVP kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana. 

WHO inasema kuepusha saratani ya shingo ya kizazi kwa kuongeza upatikanaji na ufikiwaji wa chanjo ndio hatua bora zaidi ya kuondoa magonjwa na vifo vinavyozuilika.