Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau wa kiswahili washauriwa kutumia ChatGPT

Dkt. Fillipo Lubua akieleza kuhusu suala la ChatGPT katika Kongamano la 8 la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), huko jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania.
UN News/Leah Mushi
Dkt. Fillipo Lubua akieleza kuhusu suala la ChatGPT katika Kongamano la 8 la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), huko jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Wadau wa kiswahili washauriwa kutumia ChatGPT

Utamaduni na Elimu

Wadau wa Kiswahili wameshauriwa kuchangamkia maendeleo ya teknolijia na kutumia ubunifu unaoletwa na teknolojia katika utendaji kazi wao wakipewa mfano wa kutumia ChatGPT katika kuandaa kazi zao za ufundishaji na kupata mawazo mapya. 

Hayo yamesemwa na Rais wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) Dkt. Fillipo Lubua katika mahojiano maalum na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa walipokutana katika Kongamano la 8 la Kimataifa la CHAUKIDU huko jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania. 

Dkt Lubua ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Pittsburg nchini Marekani alimueleza Leah kuwa “Ninachotaka kuwaambiwa wadau wa Kiswahili ni kuwa teknolojia hairudi nyumba bali inasonga mbele, kama wanataka Kwenda na wakati basi wasiachwe nyuma na teknolojia.” 

Amewashauri waangalie ni teknolojia gani inatumika hivi sasa na inatumika kwa namna gani ili wasiachwe nyuma “Teknolojia ndio maisha na maisha ndio teknolojia tunatakiwa tu tujue ni namna gani tuitumie kwa faida yetu na ninamna gani tukabiliane na changamoto zake lakini hatuwezi kuikwepa kwahivyo walimu wa lugha ya Kiswahili msibaki nyuma.” Amesema Dkt.Lubua 

Kongamano la 8 la Kimataifa la CHAUKIDU huko jijini Arusha nchini Tanzania lilifanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 14 mpaka 16 Desemba 2023 na kuwaleta pamoja wadau wa lugha ya Kiswahili wakiwem walimu, wakalimani na watafsiri wa lugha hiyo. 

ChatGPT

Kwa mara mbili wadau hao walifundisha kuhusu ChatGPT na namna ya kuitumia na Dkt. Lubua anaeleza sababu mbili za kutoa kipaumbele kwa somo la akili mnemba (AI) 

“Mara ya kwanza ilikuwa ni warsha na tulijifunza kwa kina sana kuhusu ChatGPT vile ambavyo walimu wa kiswahili na lugha nyingine pia wanaweza wakaitumia ChatGPT kufundishia lugha. Ya pili ilikuwa ni wasilisha dogo nililofanya na mwenzangu Mwalimu Grace Mkomwa tukiwa na mada je ChatGPT inaleta baraka katika ufundishaji katika elimu ya juu au inaleta laana.”

Ameeleza katika kujadili huko walichoondoka nacho ni kuwa umuhimu wa akili mnemba katika zama hizi ni mkubwa sana kwasababu watu wanahitaji kujua kuwa dunia imehama kutoka katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – TEHAMA na kwenda katika teknolojia za kiwango cha juu zaidi, teknolojia za AI. 

Kongamano la nane la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) huko Arusha Tanzania.
UN News/Leah Mushi
Kongamano la nane la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) huko Arusha Tanzania.

Faida za ChatGPT

Rais huyo wa CHAUKIDU ametaja faida kadhaa za kutumia ChatGPT 

“kwanza nianze na walimu – mojawapo ya vitu ambavyo vimetajwa sana na watu wanaokosoa matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, wamesema Kiswahili hakina matini ya kutosha, saa ChatGPT inatupa nafasi ya kutafsiri matini yoyote ile, maudhui yoyote yale yanayopatikana katika lugha yoyote ile kuyapeleka katika lugha ya kiswahili.” 

Akitaja umuhimu mwingine wa ChatGPT amesema “inatupatia fursa ya kutafsiri matini na vitabu na maudhui yaliyo katika lugha ya Kiswahili kwenda katika lugha nyingine kwa hivyo fasihi na maandiko ya Kiswahili yanaweza kupatikana katika lugha nyingine, kwahivyo inarahisisha zaidi.”

Kwa upande wa walimu ameeleza wakitumia ChatGPT itawasaidia sana katika masuala mbalimbali ya kiualimu. “Kwa mfano inaweza kuwasaidia katika kutengeneza maudhui mbalimbali ambazo wanaweza wakazitumia darasani na huo ndio umuhimu mkubwa sana kwa walimu wa lugha.” 

Wanafunzi nao wanaweza pia kunufaika na maendeleo haya ya teknolojia. 

“Wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wanaweza kuitumia kama rafiki wa lugha. Mfano wanafunzi ambao wapo mfano Marekani au ulaya ambaye hakutani na wazawa au wasemaji wa lugha ya Kiswahili anaweza kutumia ChatGPT kama rafiki wa lugha wa kuwasiliana naye. Anaweza kuongea naye akimwambia habari na ChatGPT itamjibu nzuri na wewe je?”

Dkt. Fillipo Lubua akieleza kuhusu suala la ChatGPT katika Kongamano la 8 la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), huko jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania.
UN News/Leah Mushi
Dkt. Fillipo Lubua akieleza kuhusu suala la ChatGPT katika Kongamano la 8 la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), huko jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Changamoto za ChatGPT

Mwaka 2023 Shirika la elimu sayansi na utamaduni UNESCO lilitoa muongozo kwa serikali na watunga sera kuhakikisha wanatunga sera kuhusu matumizi ya AI mashuleni kwani ikiachwa kutumika bila miongozo inaweza kuleta changamoto. 

Dkt. Lubua ameeleza kuunga mkono suala hilo akieleza kuwa udanganyifu hasa kwa wanafunzi na hata wanaotumia AI bila kueleza wamechukua maudhui kutoka ChatGPT ni suala ambalo wahusika wanapaswa kulizingatia. 

Ameeleza uzoefu wake hapo zamani wanafunzi walikuwa wanatumia Google kutafsiri kazi zao kutoka kiingereza kwenda Kiswahili na kudanganya kama ni kazi zao halali. 

Ametolea mfano chuo chake tayari wameshaweka sera inayohamasisha wanafunzi kutumia ChatGPT lakini kwa ueledi bila kudanganya kuwa nikazi zao ilihali wamechukua maudhui kutoka sehemu nyingine.