Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 40 ya nchi za kipato cha chini zitakuwa maskini zaidi kuliko kabla ya COVID-19

Kampuni ya Yvette Amuli, (pichani) iitwayo Kiyana ni miongoni mwa wanufaika wa mradi wa kampuni ndogo na za kati, SME's unaoendeshwa kwa pamoja kati ya Benki ya Dunia na UN Women kwa ushirikiano na Sowers of New Hope, huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu…
UN/ Byobe Malenga
Kampuni ya Yvette Amuli, (pichani) iitwayo Kiyana ni miongoni mwa wanufaika wa mradi wa kampuni ndogo na za kati, SME's unaoendeshwa kwa pamoja kati ya Benki ya Dunia na UN Women kwa ushirikiano na Sowers of New Hope, huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Asilimia 40 ya nchi za kipato cha chini zitakuwa maskini zaidi kuliko kabla ya COVID-19

Ukuaji wa Kiuchumi

Benki ya Dunia kupitia ripoti ya matarajio ya uchumi kwa mwaka huu wa 2024 inaeleza kuwa baada ya uchumi wa mwaka 2023 kufanya vibaya, nchi za kipato cha chini zitakua kwa 5.5%, chini ya ilivyotarajiwa na kwamba kufikia mwisho wa 2024, karibu 25% ya nchi zinazoendelea na karibu 40% ya nchi za kipato cha chini zitakuwa maskini kuliko kabla ya janga la COVID-19.

Kwa nchi zenye uchumi wa juu, Benki ya Dunia inatabiri kushuka kwa ukuaji mwaka huu ambao unaweza kutoka asilimia 1.5 za mwaka 2023 hadi asilimia 1.2 mwaka huu 2024.

Mwanauchumi mkuu wa Benki ya Dunia Indermit Gill ameeleza kwamba ukuaji dhaifu wa muda mfupi utasababisha nchi nyingi zinazoendelea, hasa zile maskini zaidi, kufikia “viwango vya juu vya madeni na upatikanaji wa chakula usio wa kuaminika kwa karibu mtu mmoja kati ya watatu.”

"Hilo litazuia maendeleo katika vipaumbele vingi vya kimataifa," Gill anasisitiza. "Lakini bado kuna fursa za kubadili mkondo," anangeza, akitoa wito kwa serikali kote duniani kuchukua hatua sasa ili kuharakisha uwekezaji na kuimarisha mifumo ya sera za fedha.