Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wingu zito limetanda juu ya uchumi wa dunia.

Urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ni moja ya mbinu za kukuza uchumi wa nchi
IFAD
Urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ni moja ya mbinu za kukuza uchumi wa nchi

Wingu zito limetanda juu ya uchumi wa dunia.

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti ya matarajio ya ukuaji wa uchumi duniani iliyotolewa Jumatatno na Benki ya Dunia imeonesha kuwa uchumi wadunia unategemewa kudorora kwa asilimia 2.9 kwa mwaka huu wa 2019 huku biashara ya kimataifa na uwekezaji vikipungua, mvutano wa biashara ukiendelea kuongezeka na madeni ya serikali kwa nchi za kipato cha chini yakiongezeka.

Taarifa ya Benki ya Dunia imesema masoko kadhaa makubwa yalikuwa na shida kubwa ya kifedha mwaka jana, na kwamba katika “kukabiliana na hali hii ya changamoto, ukuaji wa soko jipya na uchumi unaoendelea vinatarajiwa kubaki pabaya mwaka huu wa 2019. Ukuaji uchumi unaotegemea sana mauzo ya bidhaa nje una uwezekano wa kuzorota kuliko ilivyotarajiwa na ukuaji wa kiuchumi katika katika nchi nyingi unatarajiwa kupungua.”

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia Kristalina Georgieva anasema "mwanzoni mwa mwaka 2018 uchumi wa dunia ulikuwa unaenda vizuri, lakini ulipoteza kasi mwaka ulivyoendelea na safari hiyo inaweza kupata misukosuko zaidi kwa mwaka huu mpya. Ili kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi ni muhimu nchi ziwekeze katika watu, kukuza ukuaji wa pamoja na kujenga jamii sitahimilivu”

Ripoti hii inasema katika miaka ya hivi karibuni nchi za kipato cha chini zimepata vyanzo vipya vya mapato na mikopo kutoka nje ya nchi kubwa za kutoa mikopo jambo ambalo limezisaidia nchi kutekeleza mahitaji ya miradi ya maendeleo lakini suala hilo limechangia katika kukua kwa deni la taifa katika nchi hizo.

Deni la taifa kwa mujibu wa ripoti limeongezeka kwa kati ya asilimia 30 hadi 50 katika miaka minne iliyopita baadhi ya nchi zilizotajwa kukumbwa na ongezeko la deni la serikali ni Msumbiji, Zimbabwe na Benin.

Benki ya Dunia inapendekeza hatua za  kunusuru uchumi kuwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi kwa kuweka sera ambazo zitapunguza changamoto zinazokumba sekta hiyo.

Benki ya Dunia hutoa ripoti kama hii mara mbili kwa mwaka ambapo moja hutolewa mwezi Januari na nyingine mwezi Juni kama moja ya tahimini ya maendeleo ya kiuchumi na matokeo yake katika nchi wanachama.