Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Celeste Saulo wa Argentina aanza jukumu lake la uongozi WMO

Celeste Saulo, mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO. Ameanza kazi rasmi leo huko Geneva, Uswisi
National Meteorological Service
Celeste Saulo, mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO. Ameanza kazi rasmi leo huko Geneva, Uswisi

Celeste Saulo wa Argentina aanza jukumu lake la uongozi WMO

Masuala ya UM

Profesa Celeste Saulo wa Argentina hii leo ameanza rasmi jukumu lake la Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa, WMO huko jijini Geneva, nchini Uswisi.

 

Taarifa iliyotolewa leo na WMO huko Geneva uswisi inasema Profesa Saulo anakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwezi Machi mwaka 1950,  hallikadhalika mwanamke wa kwanza kutoka Amerika Kusini.

Kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Wizara ya Hali ya Hewa nchini Argentina tangu mwaka 2014 na pia aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa WMO.

Profesa Saulo katika wadhifa wake ataongoza WMO kuelekea maono yake ya dunia ambamo kwamo mataifa yote, hasa yaliyo hatarini zaidi, yataweza kuwa na mnepo kwenye hali mbaya ya hewa,  mabadiliko ya atabianchi, maji na matukio mengine ya mazingira.

Ataongoza pia shughuli za jumuiya ya WMO kubadilisha sayansi iwe na faida zaidi kwa jamii kwa kadri iwezekanavyo. Hii ni pamoja na kuimarisha huduma za ufuatiliaji na ubadilishanaji wa data unaohitajika kwa ajili ya utabiri wa mabadiliko ya tabianchi unaotegemeka na unaoweza kufikiwa, kunufaika kutokana na maendeleo makubwa ya akili mnemba, na kupanua Huduma za Maonyo ya Mapema ili kulinda kila mtu duniani.

Prof. Saulo pia atajaribu kuunganisha ufuatiliaji na utafiti wa WMO wa viashirio na athari za mabadiliko ya tabianchi ili kutoa taarifa kuhusu kufanya maamuzi juu ya kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kupitia mpango mpya wa  Ufuatiliaji duniani wa hewa chafuzi au Global Greenhouse Gas Watch. 

"Mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa la kimataifa la nyakati zetu, na kuongezeka kwa usawa kunazidisha athari zake. Tumeishi mwaka wa joto zaidi kwenye rekodi na huenda mwaka wa 2024 ukawa wa joto zaidi na uliokithiri mara tu athari kamili ya El Niño inayoendelea itakapoonyeshwa kwenye halijoto na matukio ya mabadiliko ya tabianchi. Shughuli za kibinadamu na za viwanda zinalaumiwa bila shaka, “ amenukuliwa Profesa Saulo kwenye taarifa hiyo.

Kwa kumalizia, Prof. Saulo amethibitisha kuwa moja ya vipaumbele vyake vitakuwa kuimarisha uwepo wa WMO katika ngazi ya kikanda na kuwezesha huduma za Kitaifa za mabadiliko ya tabianchi na Uhai kupitia hali kadhalika za mikoa ili kuimarisha utofauti wa kijiografia ndani ya Sekretarieti ya WMO. 

Hii ni kutokana na azma ya kudumisha uhusiano wa karibu na familia ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya maendeleo, na sekta ya kibinafsi ya Mpango wa Maonyo ya Mapema kwa Wote, ambapo uongozi halisi na matokeo madhubuti yanatokana na ushirikiano.

Profesa Saulo anamrithi Prof. Petteri Taalas wa Finland ambaye alikamilisha majukumu yake ya mihula miwili. 

Aliteuliwa tarehe 1 Juni 2023 katika mkutano wa nne wa WMO unaofanyika kila baada ya miaka minne, mkutano ambao una wanachama 193.