Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa IFAD na wadau wanusuru Wahadzabe dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Mabadiliko ya tabianchi yameathiri mbinu za kujipatia kipato na chakula kwa jamii ya wahadzabe nchini Tanzania ambao ni wawindaji. IFAD imewapatia mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na mizinga.
IFAD Video
Mabadiliko ya tabianchi yameathiri mbinu za kujipatia kipato na chakula kwa jamii ya wahadzabe nchini Tanzania ambao ni wawindaji. IFAD imewapatia mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na mizinga.

Mradi wa IFAD na wadau wanusuru Wahadzabe dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Nchini Tanzania, mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD umeleta nuru kwa jamii ya kabila la Wahadzabe, ambao mabadiliko ya tabianchi yameathiri vibaya mfumo wao wa uwindaji ili kupata chakula.

 

Wakati wa mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa mabadiliko ya tabianchi, COP28 ulipomalizika tarehe 13 Desemba mwaka 2023 huko Dubai, Falme za kiarabu, mambo muhimu yaliyotakiwa kupatiwa kipaumbele ni pamoja na kuhakikisha jamii zinapatiwa mbinu za kuweza kuendelea kujipatia mahitaji yao kwenye mazingira yao huku zikihimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

IFAD tayari inatekeleza hilo ambapo Evarist Mapesa wa Idhaa hii amefuatilia hatua hizo kupitia video ya mfuko huo akianza na Shakwa. 

Shakwa, ni mwindaji na anasema hafahamu umri wake, ila anachojua tu ni kwamba kuna mnyama mkubwa aliuawa wakati alipozaliwa.

Mabadiliko ya tabianchi yakawa ‘mwiba’ kwa wahadzabe

Shakwa ni kabila la Wahadzabe ambao wanapatikana wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida uliopo takribani kilometa 348 kutoka mji mkuu  wa Tanzania Dodoma, kwa usafiri wa gari ni saa 5 na dakika 35 . 

Anasema sisi Wahazabe tunapata mlo kwa kuwinda, hilo ndilo tunalojua, tumeshuhudia kilimo kutoka kwa makabila mengine yanayotuzunguka walituletea mambo haya mapya.

Wahazabe wanachukuliwa kuwa baadhi ya jamii chache zilizosalia zwa wawindaji barani Afrika. Idadi yao kwa sasa kaskazini mwa Tanzania yakadiriwa kuwa 1,300. Joseph Kihaule ni Meneja wa Mradi wa udhibiti wa mmomonyoko wa ardhi na uhakika wa chakula

Bwana Kihaule anasema “jamii ya wahadzabe kwa kiasi kikubwa inategemea zaidi uwindaji,ufugaji wa nyuki pamoja na ulaji wa mizizi, mabadiliko yameanza kuonekana kwamba kama upatikanaji wa chakula kwao umeanza kuwa ni mgumu, kwahiyo kupitia mradi umewawezesha kupata mafunzo ya kilimo, taratibu wanaanza kuelewa kwamba pamoja na kutegemea msitu, lakini wategemee na kilimo kuwawezesha kupata chakula na kuweza kuendesha maisha yao.”

Mradi wa IFAD na GEF umekuwa mkombozi

Mradi wa udhibiti wa mmomonyoko wa ardhi na uhakika wa chakula unafadhiliwa na Fuko la Mazingira au Global Environment Facility (GEF) kwa msaada wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD na Serikali ya Tanzania.

Mradi huo unasaidia jamii ya Wahazabe kupata chanzo cha uhakika cha mapato huku wakihifadhi misitu. Wahadzabe wamepatiwa zaidi ya mizinga 1,000 ya nyuki, ambayo huning’inizwa mitini ili isishambuliwe na wanyama wa porini. Wamepatiwa pia mafunzo ya ufugaji nyuki. Mara mbili kwa mwaka, wao hurina asali hiyo, ambayo hutolewa kwenye mazega yake kwenye kituo kipya kinachofadhiliwa na mradi huo na kisha asali kuuzwa kwa wanunuzi wa ndani.

Maelezo zaidi anayo Azizi Ali Zombe kutoka kampuni ya ufugaji wa nyuki iitwayo Northern Tanzania Beekeeping Company Limited ambaye anasema, “lakini pia tunasambaza kwenye nyumba za kulala wageni na kampuni za utalii huwa pia tunawapelekea

Ufugaji nyuki umekuwa na faida kwa jamii na wengineo

Uzalishaji wa asali hausaidii tu wale wanaofanya kazi kama wafugaji nyuki, bali pia unanufaisha jamii nzima, Jackson Lubumba ni mwenyekiti wa jamii ya Wahazabe na anasema, “kwa upande wa watu tunaosimamia au kunufaika na mradi huu tunafika watu kama 150 na bado watu wanaendelea kuongezeka kwasababu vijana wanazidi kukua, kwahivyo idadi itazidi kuongezeka.”

Wahazabe wanaamua kwa pamoja jinsi pesa zitakavyotumika; iwe kwa miradi ya kijamii au kibinafsi. Bwana Lubumba anaendelea akisema, “kutokana na mizinga hii tunatakiwa vijana wetu tuwasomeshe, wapate elimu kama hizo kwa ajili ya kujiingizia mapato 

Shakwa alitumia faida yake kufunga umeme wa jua ili kutumia umeme. Bado anathamini mazingira yake, lakini anafurahia kukumbatia mbinu mpya za kumsaidia yeye na familia yake kuwa na maisha bora.

“Maisha yangu ni ya porini, tumezungukwa na pori, napenda kuishi katika mazingira haya. Ninashukuru kwamba tulipewa mizinga ya nyuki na sasa maisha yanakwenda vizuri,” anasema Shakwa.

IFAD inafanya kazi na watu 30,000 kote Tanzania, kuwapatia mbinu endelevu za kujipatia kipato na wakati huo huo kuhifadhi mazingira asilia.