Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa kimaasai Monduli wageukia ufugaji nyuki kwa hisani ya FAO na wadau

Wanawake wa Kimaasai Monduli nchini Tanzania wageukia ufugaji nyuki ili kujikwamua kiuchumi.
FAO Tanzania
Wanawake wa Kimaasai Monduli nchini Tanzania wageukia ufugaji nyuki ili kujikwamua kiuchumi.

Wanawake wa kimaasai Monduli wageukia ufugaji nyuki kwa hisani ya FAO na wadau

Ukuaji wa Kiuchumi

Kaskazini mwa Tanzania, ukame wa mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni umeweka shinikizo kwa jamii zilizozooea kujipatia riziki kwa kufuga ng'ombe. Kundi la wanawake wa Kimasai wamegeukia kuzalisha asali kutoka kwenye mizinga ya nyuki msituni ili kujipatia kipato cha ziada. Hii imehakikishia mustakabali wa watoto wao na inasaidia kuzalisha upya msitu unaozunguka mizinga yao.

Katika eneo moja lililo kaskazini mwa Tanzania, Maria Shinini naonekana akivaa vazi lake la ufugaji nyuki linalofunika mwili wote kwa ajili ya maandalizi ya urinaji asali nyakati za usiku. Wana kikundi cha wafugaji nyuki wenzake wa Kimasai wanachochea moshi unaohitajika ili kutuliza nyuki na kukusanya asali hiyo kwa usalama. Kikundi hiki wana mizinga 76 sasa kwenye shamba la jumuiya nje kidogo ya wilaya ya Monduli mkoani Arusha. 

Maria alianza na mizinga mitano na vitendea kazi kadhaa, pamoja na mafunzo kutoka kwa mtandao wa wakulima wadogo, wakulima na wafugaji (MVIWAARUSHA) unaofadhiliwa na Shirika la Forest and Farm Facility (FFF), ushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira, Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) na AgriCord,zote zikiwa ni taasisi za kimataifa zinazojihusisha na kilimo na mazingira. 

Maria Shinini, mwanamke wa kimaasai ambaye ni mfugaji wa nyuki Monduli nchini Tanzania.
FAO Tanzania
Maria Shinini, mwanamke wa kimaasai ambaye ni mfugaji wa nyuki Monduli nchini Tanzania.

Sasa biashara ya Maria inastawi na maisha yake yamebadilika.

Kwa upande wa mashariki wa Bonde la Ufa, karibu na Mlima Kilimanjaro, sehemu hii ya Tanzania ni ya kijani kibichi. Ni msimu wa mvua, lakini mvua mwaka huu zimekuwa kidogo kuliko kawaida. Miongo kadhaa ya ukame wa mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya tabianchi imeharibu mandhari na kupunguza malisho ya mifugo. 

Kuanzisha ufugaji nyuki ni mpango mmoja wa kuifufua upya mandhari. Ufugaji nyuki husaidia kuhifadhi misitu kwa sababu ni makazi ya mimea ambayo wafugaji wa nyuki lazima walinde kama chakula cha nyuki wao. 

Wakati wa mafunzo, Maria na kikundi chake wanasikiliza kwa makini. Wamejifunza tangu mwanzo kwamba uhifadhi wa mazingira ni kipengele muhimu cha utunzaji na usimamizi wa nyuki wao. Mkufunzi wao Majaliwa Mwashuve, kutoka mtandao mwamvuli unaofadhiliwa na FFF amewafundisha kutunza mimea karibu na mizinga yao msituni ili nyuki wao waweze kustawi.  

FFF inasaidia mitandao saba ya wakulima wadogo, wakulima na wafugaji inayoitwa “Mashirika ya Wazalishaji Misitu na Mashamba” (FFPOs), kote Tanzania, kufikia zaidi ya kaya 300,000, ili kuendeleza biashara na kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Shukrani kwa shughuli mbalimbali, karibu hekta 68,000 za misitu zimefufuliwa tangu mwaka 2020. 

Matokeo kwa jamii yamekuwa makubwa. Maria na wafugaji nyuki wenzake wamepata mafunzo ya jinsi ya kuwa wafanyabiashara mahiri, kuzalisha, kuweka lebo na kuweka chapa bidhaa zao ili kuongeza thamani yao na kuunganisha nguvu na wafugaji wengine kupata masoko mapya. 

Wanawake wa kimaasai Monduli nchini Tanzania wageukia ufugaji nyuki ili kujikwamua Kiuchumi.
FAO Tanzania
Wanawake wa kimaasai Monduli nchini Tanzania wageukia ufugaji nyuki ili kujikwamua Kiuchumi.

Bidhaa moja mpya wanayoipa nafasi, ambayo ni matokeo ya uhusiano mpya katika wilaya jirani ni "asali ya vitunguu", hiyo ni vitunguu saumu vilichochanganywa na asali, na wakati mwingine vikichanganywa na viungo mbalimbali pia.

Ingawa inaendeshwa zaidi na wakulima wadogo, nchini Tanzania, asali ni biashara kubwa. Kote nchini, kuna zaidi ya wanawake na wanaume milioni 2 katika ufugaji nyuki na kazi zinazohusiana nayo, kama vile wazalishaji, wasindikaji, wafungaji na wauzaji. Katika msimu mmoja, Maria husindika hadi chupa 300 za asali za lita moja, ambazo huuzwa kwa shilingi 10,000 za Kitanzania sawa na dola 4.5 za kimarekani kwa kila lita moja.  

Hii imehakikishia mustakabali wa watoto wake na kumpa hadhi mpya katika jamii yake. Aligombea uchaguzi wa serikali ya mtaa na akashinda, na sasa ni Mwenyekiti wa baraza lake la mkoa, lenye wapiga kura zaidi ya elfu 16.

Na kwa hakika, Maria na wafugaji nyuki wenzake wanatimiza jukumu muhimu katika kutunza familia zao na kulinda mazingira katika nyakati ngumu. 

Na si hayo tu, Maria husafiri ndani ya wilaya yake mara kwa mara akiwahimiza wanawake wengine wa Kimasai kujiunga na vikundi vya ufugaji nyuki kama yeye ili nao waweze kufaidi kama yeye.