Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya mpira wa kikapu duniani

Timu ya mpira wa kikapu ya Harlem Globaltrotter ilipotembelea UN kwa mara ya kwanza Novemba 21, 2019
DGC
Timu ya mpira wa kikapu ya Harlem Globaltrotter ilipotembelea UN kwa mara ya kwanza Novemba 21, 2019

Leo ni siku ya mpira wa kikapu duniani

Utamaduni na Elimu

Maadhimisho ya kwanza kabisa ya siku ya mpira wa kikapu duniani yanafanyika leo baada ya kuidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu wa 2023 kupitia azimio namba 77/324.

Tweet URL

Msingi wa azimio hilo pamoja na mambo mengine ni kutambua kuwa michezo ni moja ya viwezeshi vya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au Ajenda 2030.

Umoja wa Mataifa unasema michezo na Sanaa vina nguvu ya kubadili mitazamo, ubaguzi, ukosefu wa haki, tabia na hata kujengea hamasa watu, kuvunja mipaka ya ubaguzi wa rangi na ya kisiasa na kuondoa mivutano au mizozo.

Mpira wa kikapu una athari chanya kibiashara, kidiplomasia, amani na huumba fursa ya kipekee ya ushirikiano, mienendo ya watu n ahata huruhusu wachezaji kutegemeana na kuonana wote ni binadamu.

Zaidi ya yote Umoja wa Mataifa kupitia wavuti wake wa siku hii, unasema michezo kama vile mpira wa kikapu huvuka mipaka, tamaduni na lugha.

“Ni kiunganishi cha watu kutoka maeneo tofauti tofauti, huwaunganisha watu na kuvunja mipaka na hivyo kujenga amani,” unasema Umoja wa Mataifa.

Mpira wa kikapu ulianza lini?

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mpira wa kikapu kwa mara ya kwanza ulichezwa tarehe 21 mwezi Desemba mwaka 1891 katika shule ya kimataifa ya mafunzo ya YMCA huko Springfield jimboni Massachusetts nchini Marekani, baada ya Dkt. James Naismith, mkufunzi wa elimu ya viungo vya mwili kutoka Canada kubuni mchezo huo ili wanafunzi wake waweze kuwa imara wakati wa msimu wa baridi kali.

Hii leo, mpira wa kikapu umekua na kuwa moja ya michezo mashuhuri duniani.

Shirikisho la mpira wa kikapu, duniani, FIBA, chombo cha usimamizi wa mpira huo duniain, linakadiria kuwa takribani watu milioni 450 duniani wanacheza mchezo huo.

Mpira wa kikapu ni sehemu ya michezo ya Olimpiki na ulijumuishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1936 wakati wa michezo ya Olimpiki huko Berlin.