Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nje na ndani ya uwanja wanamichezo wasongesha harakati za usawa na amani

Mali (13) na Dieumerci Mbokani  wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwenye mafunzo ya haki za mtoto kupitia soka.
© UNICEF/UN0658457/Josue Mulala
Mali (13) na Dieumerci Mbokani wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwenye mafunzo ya haki za mtoto kupitia soka.

Nje na ndani ya uwanja wanamichezo wasongesha harakati za usawa na amani

Utamaduni na Elimu

Wanamichezo wanasongesha harakati ya dunia yenye usawa wakiwa ndani na nje uwanja, umesema Umoja wa Mataifa hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya michezo kwa ajili ya maendeleo na amani.

Tweet URL

Huu ni mwaka wa 10 tangu maadhimisho haya yaanze,  yakimulika dhima chanya ya michezo katik ajamii na maisha ya binadamu duniani kote.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha siku hii ambapo wanamichezo wa kulipwa na wale wa kawaida wa umri mbali mbali wameungana na wataalamu wa michezo, wanadiplomasia na maafisa wa Umoja wa Mataifa kushiriki tukio hili, la kwanza kufanyika ukumbini tangu kuanza kwa janga la coronavirus">COVID-19 mwaka 2020.

Maudhui ya mwaka huu ni Funga goli kwa ajili ya Watu na Sayari.

Kusongesha stahmala na ujumuishi

Iwe ni michezo ya ushindani au kuburudisha, michezo huleta watu pamoja na kujenga daraja la utamaduni, kabila na mgawanyiko wa kitaifa, amesema John Wilmoth kutoka Idara ya  Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Kijamii, DESA.

“Michezo inaweza pia kuwa kichocheo cha kusongesha stahmala na kuheshimiana, ujumuishi, usawa wa jinsia na kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Wilmoth.

Ni kwa mantiki hiyo anataka watu kufanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote anaachwa nyuma katika shughuli za michezo, hususan vijana, wazee, watu wenye ulemavu, watu wa jamii ya asili na makundi ya pembezoni.

Kuonesha mfano

Katika ujumbe wake kwa njia ya video iliyochezwa kwenye tukio la leo, nguli wa mpira wa miguu duniani,  Didier Drogba amerejelea dhima ya msingi ya michezo katika kuendeleza utamaduni wa amani.

“Tasnia ya michezo, wakiwemo wanamichezo, ina dhima muhimu ya kuonesha mfano, hasa kwa vijana,” amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa, ambaye pia ni Balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO.

“Wanataka kusongesha mambo muhimu ambayo yana maslahi yetu sote katika kuunga mkono hoja za usawa wa kijinsia, kutokomeza ubaguzi wa rangi na kushiriki katika kulinda mazingira.”

Tukio hilo liliambatana na msururu wa mazungumzo yaliyochambua mambo magumu kama vile haki za wanamichezo na mchango wao, kusimamia mchanganyiko wa wachezaji kutoka pande mbali mbali, uwiano na ujumuishi, jinsia na rangi, hatua kwa tabianchi na kubadilika kwa mfumo wa vyombo vya habari.

Mcheza kabumbu nguli, Javier Zanetti, ambaye sasa ni Makamu Rais wa klabu ya soka ya Inter Milan ya nchini Italia akizungumza kwenye mkutano huo.
UN /Eskinder Debebe

Kushirikishana maadili ya pamoja

Mjadala mkuu ulijikita kwa mcheza kabumbu mwingine nguli, Javier Zanetti, ambaye sasa ni Makamu Rais wa klabu ya soka ya Inter Milan ya nchini Italia.  

Klabu hiyo inaendesha miradi 30 ya kijamii ambayo inatumia maadili ya michezo na mpira wa miguu au kabumbu kama mbinu ya kuelimisha jamii, na imefikia zaidi ya vijana 10,000.

Baadhi ya wavulana na wasichana wanaoshiriki kwenye miradi hiyo walikuwemo kwenye ukumbi wa Umoja wa Mataifa wakiwa wamevalia sare zao za buluu na nyeupe.

“Lengo letu, zaidi ya kushirikishana maadili na utendaji wetu wa kazi, ni kuwakifia na kuwaeleza kuwa wana mahali kwao:kuwapatia hisia ya kuwa wana mahali kwao,” amesema Zanetti kupitia mkalimani.

Kubadili dunia

Bwana Zanetti alikuwa kwenye makazi dunia nchini Argentina lakini alijenga mapenzi yake na mpira wa miguu, yakiambatana na bidii, vyote ambavyo vilimwezesha kuwa mmoja wa wachezaji maarufu wa mpira wa miguu duniani.

Amezungumzia jinsi michezo imegusa dunia nzima, na kusisitiza nafasi yake katika kufika mbali zaidi.

“Tunachohitaji kujaribu ni kushirikishana maadili yetu ya kibinadamu na kupambana dhidi ya aina zote za ubaguzi, ubaguzi wa rangi na kutekeleza miradi inayojikita kwenye maendeleo eneo lolote duniani.  Hii ni kwa sababu hiyo ndio njia ambayo inaweza kubadili dunia.”

Halikadhalika amesema tunahitaji kuwa na fikra ya wajibu wa watu wazima kuchukua hatua mpira wa miguu uwe bora zaidi, na kufanya mustakabali uwe bora. Hata hivyo amesema “kwa mustakabali uwe bora, wavulana na wasichana duniani kote wawe na watu wa kuwaona ndio mfano kwao katika kueleza hilo, kwa hiyo wajibu mkubwa unaangukia kwetu.”

Mcheza mpira wa kikapu wa kulipwa Batouly Camara kutoka Guinea akizungumza wakati wa mkutano wa kuadhimisha siku ya michezo kwa amani na maendeleo jijini New York, Marekani.
UN /Eskinder Debebe
Mcheza mpira wa kikapu wa kulipwa Batouly Camara kutoka Guinea akizungumza wakati wa mkutano wa kuadhimisha siku ya michezo kwa amani na maendeleo jijini New York, Marekani.

Wajibu wa kimaadili 

Wakati wa mjadala kuhusu ujumuishaji zaidi, mcheza mpira wa kikapu wa kulipwa Batouly Camara alizungumzia makuzi yake yeye mtoto wa kike muislamu na kizazi cha kwanza kutoka Guinea barain Afrika kuishi jijini la New York, nchini Marekani ambako alianza kucheza mpira wa kikapu akiw ana umri wa miaka 11.

Akiwa Chuo Kikuu, alianza kuendesha kambi za mpira wa kikapu kwa watoto wa kike nchini Guinea ambako alikutana na msichana aliyebadili maisha yake.

“Aliniambia…’Nawezaje kuendelea kujenga matumaini haya ambayo umeniwekea?” anakumbuka Bi. Camara. “Na nilihisi kuwa itakuwa ni kosa mno iwapo najenga matumaini na kisha nashindwa kuweka rasilimali au vifaa au mbinu zinazohitajika kumwezesha kuwa bora zaidi na kuishi ndoto yake, kwa sababu nilikuwa na watu walionijenga na kuniwezesha kufika hapa nilipo.”