Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumekwama wapi kutekeleza Tamko la kimataifa la Haki za Binadamu? - Balozi Francis

Mkutano wa maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko ya Kimataifa la Haki za Binadamu sambamba na utoaji wa tuzo kwa washindi wa TUzo ya UN ya Haki za Binadamu 2023
UN /Eskinder Debebe
Mkutano wa maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko ya Kimataifa la Haki za Binadamu sambamba na utoaji wa tuzo kwa washindi wa TUzo ya UN ya Haki za Binadamu 2023

Tumekwama wapi kutekeleza Tamko la kimataifa la Haki za Binadamu? - Balozi Francis

Haki za binadamu

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika maadhimisho ya miaka 75 ya kupitishwa kwa Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, (UDHR), sambamba na utoaji wa tuzo kwa washindi watano wa Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu.

 

Tweet URL

“Tumekwama wapi katika kuzingatia na kutekeleza Tamko la Kimataifala Haki za binadamu?” amehoji Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Dennis Francis wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo. Na zaidi ya yote akauliza ni kwa vipi kwenda mrama huko kumeathiri wale walio hatarini zaidi?

Amesema kauli yake hiyo inazingatia ukweli kwamba miaka 75 tangu kupitishwa kwa Tamko hilo, bado dunia iko njiapanda.

“Huu ni wakati wa kuchukua hatua kuhakikisha kila haki ya binadamu haisalii tu kwenye mabango, bali inawezesha kila mtu kudai haki na maslahi yake ambavyo ni lazima apatiwe,” amesema Balozi Francis.

Balozi Francis amekumbusha kuwa kwa sababu sote ni binadamu, kila uhai una umuhimu bila ubaguzi wowote.

Haki za binadamu zinazidi kushambuliwa- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye tukio hilo lililofanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani amesema Tamko hilo lililopitishwa miaka 75 iliyopita ni wito wa kuchukua hatua kwa mujibu wa msingi wa ukweli kwamba kila mmoja wetu ni mwanachama mwenye haki sawa kwenye familia ya kibinadamu.

Hata hivyo wito huo unaendelea kushambuliwa duniani kote, kwani mizozo imeshamiri ikiwa na madhara kwa raia kama inavyoshuhudiwa na idadi kubwa ya vifo na machungu huko Gaza baada ya shambulio la kikatili tarehe 7 mwezi Oktoba.

Amesema ukosefu wa usawa unazidi kuota mizizi, njaa na umaskini vinaongezeka, wanawake wanazidi kutwamishwa na kwingineko ambako maendeleo yamepatiakana, yanarudishwa nyuma. Vile vile fursa za kiraia zinabinywa, halikadhalika uhuru wa vyombo vya habari.

Ametumia fursa hiyo kupongeza watetezi wa haki za binadamu duniani kote ambao amesema “wanabadilisha maisha. Wanapambana, wanaelimisha, wanawajibisha walio madarakani na kufanya haki za binadamu kuwa haki inayoishi na halisia.”

Hata hivyo amesema wanafanya hivyo wakikabiliwa na vitisho na visasi. 

Watetezi wa Haki za Binadamu wanatakia mema jamii zetu - Türk

Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Bindamu wa Umoja wa Mataifa alitumia tukio hilo tuzo hii ni fursa ya kusherehekea watetezi wa haki za binadamu na mchango wao wa thamani kwa jamii mbali mbali duniani kote. 

“Wanaona mustakabali bora kwa ajili yetu sote, na wanafahamu jinsi ya kugeuza mustakabali wetu uwe wa uhalisia. Lakini katika kuhoji mifumo iliyoko, au kufanya kazi kwenye mazingira ya ghasia na vurugu, wanakabiliwa na changamoto nyingi, kuanzia kutukanwa, kunyanyaswa, kukamatwa, kuswekwa korokoroni na hata kutoweshwa,” amesema Bwana Türk. 

Amemtolea mfano Julienne Lusenge, Rais wa SOFEPADI kutoka DRC kuwa ni kiongozi asiyeogopa katika kutetea haki za binadamu. Yeye anafahamika zaidi kwa kusaidia manusura wa ukatili wa kingono kwenye mizozo. 

Mkuu huyo wa Ofisi ya Umoja wa MAtaifa ya Haki za binadamu amesihi nchi wanachama ziwapatie watetezi wa haki mazingira salama ya kufanyia kazi, pamoja na ulinzi pale inapohitajika. 

“Kule mnakosaidiwa na kulindwa, uwezo wa kazi yenu kuwa na manufaa makubwa ni dhahiri. Katika siku hii ya miaka 75 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, hebu na tuimarishe ahadi yetu ya kuwalinda,” amesema Bwana Türk, huku akiwashukuru washindi wote watano kwa mchango wao katika kujenga upya jamii na yenye mustakabali bora kwa kila mtu duniani kote. 

“Ni kwa mantiki hiyo Tuzo ya Haki za Binadamu ni muhimu zaidi. Napongeza kila mmoja aliyesihnda tuzo hii kwa kazi yao ya kipekee, utu na ujasiri,” amesema Guterres.

Washindi wa Tuzo

Washindi hao ni Julienne Lusenge kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC,  Julio Pereyra kutoka Uruguay;  

Kituo cha Amman cha Masomo ya Haki za Binadamu; Kituo cha Haki za Binadamu “Viasna”, nchini Belarus; na Ushirikiano wa kimataifa wa mashirika ya kiraia, watu wa jamii ya asili, vuguvugu la kijamii na jamii za mashinani kwa aijli ya kutambuliwa kwa haki za mazingira safi, yenye afya na endelevu.

Pamoja na kuwapongeza, ametambua pia maelfu ya watetezi wa haki za binadamu wasiotambulika duniani kote.