Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya Umoja wa Mataifa ni heshima kwangu na nchi yangu-Rebeca Gyumi

Rebeca Gyumi kutoka Tanzania, mwanaharakati wa haki za wanawake na wasichana na mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu 2018.
UNIC Dar es salaam
Rebeca Gyumi kutoka Tanzania, mwanaharakati wa haki za wanawake na wasichana na mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu 2018.

Tuzo ya Umoja wa Mataifa ni heshima kwangu na nchi yangu-Rebeca Gyumi

Haki za binadamu

Leo washindi wa tuzo ya mwaka huu ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa akiwemo Rebeca Gyumi kutoka Tanzania wanakabidhiwa tuzo hizo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Mjini New York Marekani.

Rebeca Gyumi mshindi kutoka Tanzania anaanza kwa kueleza alivyoupokea ushindi huu:

“Ni heshima kubwa sana kwangu lakini pia kwa nchi yangu kwamba nimeweza kuwa mmoja wa washindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa wa Mataifa ya haki za binadamu. Kazi ambazo tumekuwa tunafanya hasa lile shauri ambalo tulipeleka katika mahakama kuu mwaka 2016 ambalo lilikuwa na lengo la kupinga ile sheria ya ndoa ambayo iliyokuwa inaruhusu watoto wa Kike kuolewa wakiwa chini ya miaka 14 ndiyo imechangia sana Umoja wa Mataifa kuona kuwa mimi ni mmoja wa watu ambao wanastahili  kupokea (tuzo) kwa mwaka huu ”

Rebeca ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya ‘Msichana Initiative’ nchini Tanzania kwa miaka 8 amekuwa akihoji uhalali wa ibara ya 13 na 17 ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 nchini humo ambayo inahurusu watoto wa kike kuolewa wakiwa na umri mdogo kwa ridhaa ya wazazi au mahakama. Lakini je! Jitihada za kumtetea mtoto wa kike zinafanikiwa?

“Nafikiri pamoja na kwamba kuna jitihada nyingi tunazifanya, vado Tanzania yetu ni kubwa sana, hata sisi hatujafika maeneo mengi  sana lakini naweza nikasema kwa wale ambao tunawafikia wanaanza kupata ile hamasa kwamba mtoto wa kike katika jamii ya leo ni zaidi ya kuwa kusema atakuja kuwa mke au mama. Lazima na wao wawe na ndoto kubwa, wasome wajiendeleze halafu pia watakuja wake wazuri na mama wazuri baadaye ”

Na ana ujumbe gani kwa wale ambao wanamtizama yeye kama mfano na wangependa kufuata nyayo zake?

“Ni muhimu sana tuweze kuwa sauti ya kubeba masuala ambayo yako katika jamii yetu. Kwamba yale ambayo tunayafanya yaweze kugusa maisha ya watu wa kawaida. Na hatuwezi kufanya hivyo kama harakati zetu hazitajikita kwenda moja kwa moja kwa watu hisika, tujue masuala yao kutoka kwao halafu sisi tutumie majukwaa yetu kupaza zaidi sauti na nafikiri hapo ndipo tutakuwa na harakati ambazo hata sisi ambapo hatutakuwepo kuna watu ambao watakuja na kuziendeleza kwa kuwa kila mtu anaona haya yanagusa maisha yetu”

Mwezi Oktoba mwaka huu wa 2018, Rebeca Gyumi alitangazwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo ya mwaka huu ya haki za binadamu ikitanguliwa na tuzo nyingine ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa mchango wake wa kukomesha ndoa za utotoni nchini Tanzania aliyoitwaa mwezi septemba mwaka 2016.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.