Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yanayojadiliwa mkutanoni hayana tija yasipotekelezwa kwa vitendo mashinani: Madina Kimaro

Madina Jubilate Kimaro akizungumza katika mahojiano huko Dubai.
UN News
Madina Jubilate Kimaro akizungumza katika mahojiano huko Dubai.

Yanayojadiliwa mkutanoni hayana tija yasipotekelezwa kwa vitendo mashinani: Madina Kimaro

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 unakunja jamvi mjini Dubai Falme za nchi za Kiarabu. Wakuu wa nchi na serikali, wadau wa mazingira wanazuoni, asasi za kiraia na vijana kutoka mataifa 199 wamejadili mengi ikiwemo hatma ya kuhakikisha joto halizidi juzijoto 1.5 na mustakbali wa matumizi ya mafuta kisukuku.

Miongoni mwa vijana walioshiriki ni Madina Jubilate Kimaro balozi wa skauti wa kike au Girlguide na wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Tanzania akijikita na mabadiliko ya tabianchi  amezungumza na UN News kandoni mwa mkutano huo, kwanza ameeleza kilichomhamasisha kujihusisha na masuala ya tabianchi.

“Nilianza kujihusisha na masuala ya mazingira wakati nilipokuwa nasoma shule ya msingi , napenda sana kufanya kilimo hivyo nilikuwa nafanya kilimo nyumbani . Na baada ya muda nikaanza kuona mazao yangu yanakauka hivyo nikajiuliza kwa nini nami nisianze kuchukua hatua dhidi ya madaliko ya tabianchi.? Na huo ulikuwa mwanzo wa kujihusisha katika programu nyingi katika jamii yangu kama kusafisha fukwe, kupanda miti, utengenezaji wa mbolea ambayo pia nawafundisha wnafunzi mashuleni na naisambaza kwa ajili ya programu za kupanda miti.”

Na huo ulikuwa ni mwanzo wa safari ya mafanikio ya Madina “Hivyo ndivyo nilitambulika na skauti wa kike au Girlguide na kuingia katika program ya hatua za wasichana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, hapo tumekuwa tukishirikiana na viongozi wetu kuelemisha na kuelezea kwa nini kuna umuhimu wa kutatua changamoto ya mabadiliko ya tanianchi.”

Madina Jubilate Kimaro akizungumza katika kongamano la watoto kuhusu masuala ya tabianchi yanayoathiri maisha yao.
Madina Jubilate Kimaro
Madina Jubilate Kimaro akizungumza katika kongamano la watoto kuhusu masuala ya tabianchi yanayoathiri maisha yao.

Balozi wa mazingira wa UNICEF

Kupitia harakati zake za kulinda na kutunza mazingira shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF walimuona na kumteuwa kuwa balozi wake wa mazingira.

Mpaka sasa Madina anajihusisha na shughuli mbalimbali na anajumuisha watoto mashuleni na vijana wenzie na kukusanya mawazo yao wanataka nini viongozi wao wafanye.

Anasema “Na hivi tumekuja hapa Katika COP28 tunajua mengi yatakuwa yamejadiliwa tulikusanya maoaji na watoto na vijana kabla ya kuja huku ili tuweze kuwafikishia maoni hayo kwa viongozi huku kwenye huu mkutano mkubwa wa COP28.”

Madina Jubilate Kimaro (mbele kulia) akiwa kwenye mkutano wa vijana wa COP28.
Madina Jubilate Kimaro
Madina Jubilate Kimaro (mbele kulia) akiwa kwenye mkutano wa vijana wa COP28.

Kwa nini suala la madiliko ya tabianchi ni muhimu kwako?

Madina amesema “Mabadiliko ya tabianchi yananiathiri sana mimi na jamii yangu mfano kwa Tanzania mwezi Novemba tulipata mafuriko makubwa na watu zaidi ya 12 walipoteza maisha na tarehe 2 Desemba kwenye wilaya ya Hanang mkoani Manyara kulikuwa na mafuriko makubwa na maporomoko ya udongo vilivyoathiri watu wengi.”

Ameongeza kuwa Tanzania inategemea kilimo ambacho ni uti wa mgongo  hivyo wale wakulima wadogo na wakubwa wanahisi vipi majanga kama hayo yanapozuka , kwa hakika wao ni waathirika wakubwa .

Kwani wanapanda mazo yao na wanashindwa kuvuna walichotegemea sababu ya mabadiliko ya tabianchi “Ukame ukiwa mkali mazao yanakauka na mvua ikiwa kubwa mazao yanasombwa na maji.”

Hivyo amesema “Mabadiliko ya tabianchi nayapazia sauti ili watu wafanhamu na kwa pamoja tuweze kuitatua changamoto hiyo.”

Vijana wahusishwe vipi katika mchakato huu

“Vijana tuna uwezo mkubwa , tuna uwezo mkubwa wa kufikiri kuliko wengi wanavyodhani . Tunaweza kufanya mengi zaidi mfano mimi kama kijana wa Kitanzania nimeweza kuja na mbolea ya composti ambayo nasambaza mashuleni na hii mbolea inasaidia sana pale ambapo inatokea ukame.”

Akasenda mbali zaidi na kusema “Vijana wana suluhu nyingi zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi , wakuja na mkaa mbadala badala ya kukata miti , kwa hiyo mimi ninaamini kwamba vijana wana uwezo tunachohitaji ni kushikwa mkono na kusukuma zile suluhu zetu zifikie watu wengi zaidi.”

Ameendelea kusema kwamba “Lakini pia vijana tunahitaji tuendelee kusukuma viongozi wetu mbele zaidi katika jamii kufanya yale ambayo wanapaswa kufanya .

Madina Jubilate Kimaro (wa tatu kushoto) akiwa Dubai, akipiga picha na vijana wenzake wakati wa hafla za kando za COP28.
Madina Jubilate Kimaro
Madina Jubilate Kimaro (wa tatu kushoto) akiwa Dubai, akipiga picha na vijana wenzake wakati wa hafla za kando za COP28.

Ahadi zisiishie mikutanoni zitekelezwe kwa vitendo

Mwisho amesisitiza kwamba kwa sababu kila siku tunakuwa na mikutano mikubwa kama huu wa COP28 basi “Yale ambayo tunayazungumza katika mikutano kama huu wa COP28 tunakwenda kuyatekeleza katika jamii zetu ili wote tuweze kunufaika na inabidi kuweza kuwafikia viongozi wetu kuanzia ngazi ya chini kabisa ya diwani mpaka kitaifa ili viongozi wajue vijana tupo na tunataka kuleta mabadiliko na kwa pamoja tulete mabadiliko hayo.”

Baada ya COP28 nini unatarajia

“Ninachotaka katika mkutano huu ni kuona kwamba viongozi wana mwamko wa kutekeleza yale wanayoyazungumzia wakati tutakaporekea majumbani kwetu , kwa sababu hicho ndio kitu cha msingi zaidi kuliko mengine yote. Ni kurudi katika jamii zetu na kufanya kitu ambacho sote tutanufaika.”