Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNITAMS kufunga pazia lake Sudan kuanzia Desemba 3

Wajumbe wa Baraza wakipiga kura kuhusu UNITAMS
UN/Eskinder Debebe
Wajumbe wa Baraza wakipiga kura kuhusu UNITAMS

UNITAMS kufunga pazia lake Sudan kuanzia Desemba 3

Amani na Usalama
  • Baraza laridhia ombi la mamlaka nchini Sudan
  • UNITAMS ilianzishwa baada ya UNAMID kuondoka
  • Uingereza yasema “hatukuwa na jinsi, zaidi ya kukubali”

Baada ya kutekeleza majukumu yake kwa takribani miaka mitatu, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia kipindi cha mpito nchini Sudan, UNITAMS unafunga virago baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kusitisha shughuli zake kuanzia tarehe 3 mwezi huu wa Desemba.

Wajumbe 14 walipiga kura ya ndio huku Urusi haikupiga kura.

Uingereza ndio iliyoandaa rasimu ya azimio

Azimio la kusitisha kazi ya UNITAMS liliandaliwa na Uingereza ambapo Mwakilishi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi James Kariuki amesema kwamba Uingereza isingalichagua kufungwa kwa UNITAMS hasa wakati huu.

“Hata hivyo kulingana na matakwa ya mara kwa mara ya mamlaka nchini Sudan ya kutaka kufungwa mara moja kwa shughuli za UNITAMS imebidi kama waandishi wa rasimu ya azimio hili tukubali kulegeza msimamo ili kuruhusu kuondoka kwa UNITAMS kwa utaratibu na mpito mzuri,” amesema Balozi Kariuki.

Raia wa Sudan Kusini waliorejea nchini kutoka Sudan wakiwasili katika mpaka wa Joda katika Jimbo la Upper Nile.
© WFP/Eulalia Berlanga
Raia wa Sudan Kusini waliorejea nchini kutoka Sudan wakiwasili katika mpaka wa Joda katika Jimbo la Upper Nile.

Amesema wanashukuru UNITAMS kwa kazi nzuri iliyofanya kabla na baada ya kuzuka kwa mapigano mwezi Aprili mwaka huu, huku akisisitiza kuwa mamlaka za Sudan ziwajibike na usalama wa wafanyakazi wa UNITAMS na mali za ujmbe huu wakati huu wa kipindi cha mpito.

Hakuna suluhu ya kijeshi

Nchini Sudan mapigano yanaendelea kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa kikundi cha RSF, pande zote mbili zikiongozwa na majenerali wa kijeshi.

“Hakutakuweko na suluhu ya kijeshi kwenye huu mzozo,” amesema Balozi Kariuki, akiongeza, “pande mbili zinazokinzana zinapaswa kushiriki kwenye mazungumzo ya kina na ya dhati ya kuwezesha kupatikana kwa sitisho la kudumu la mapigano na kuhamishia madaraka kwa utawala wa kiraia.”

Nchi za Afrika barazani zazungumza

Mwakilishi wa Kudumu wa Ghana kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Harold Adlai Agyeman, akizungumza kwa niaba ya nchi tatu za Afrika kwenye Baraza hilo ambazo ni Gabon, Msumbiji na Ghana amesema,  “Hali Darfur na maeneo mengine ya Sudan inachukiza. Na lazima tuchukue hatua kuitikia wito wa wananchi wa Sudan ambao wanataka sitisho la mapigano, ulinzi wa raia na kupata msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani.”

Amesema wao wakiwa ni nchi kutoka Afrika wana hofu na hali ilivyo sasa na kwamba wataendelea kutoa ushirikiano ndani ya Baraza na katika maeneno mengine kwenye michakato inayohusiana na kukomeshwa kwa mapigano.

Asante Baraza kwa kukubali ombi letu

Kwa upande wake Dafalla Al-Haj Ali Osman, ambaye ni Mjumbe Maalum wa Mwenyekiti wa Baraza la Mpito nchini Sudan ameshukuru Baraza kwa kuitikia wito wa serikali ya Sudan wa kutisishwa kwa majukumu ya UNITAMS.

“Tunatoa hakikisho la utayari wa serikali kuendelea na mazungumzo ya kina na Umoja wa Mataifa kwa kuimarisha ushirikiano na ofisi ya Umoja huo nchini Sudan ili kushughulikia masuala ya kujikwamua tena, ujenzi mpya na usaidizi wa kimaendeleo,” amesema Bwana Osman.

Mwanamke akirudi kutoka kwa kinu kipya cha unga kilichojengwa huko Shanisha, Jimbo la Blue Nile. Wanawake na wasichana nchini Sudan wanakabiliwa na vitisho vya mara kwa mara vya unyanyasaji na mashashambulizi wanaposafiri umbali mrefu, mara nyingi peke y…
© UNFPA Sudan
Mwanamke akirudi kutoka kwa kinu kipya cha unga kilichojengwa huko Shanisha, Jimbo la Blue Nile. Wanawake na wasichana nchini Sudan wanakabiliwa na vitisho vya mara kwa mara vya unyanyasaji na mashashambulizi wanaposafiri umbali mrefu, mara nyingi peke yao, kufikia huduma muhimu.

UNAMID kwenda UNITAMS

Tarehe 3 mwezi Juni mwaka 2020 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuanzisha UNITAMS baada ya kuondoka kwa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, wa kulinda amani Darfur, Sudan, UNAMID.

UNAMID ilianzishwa tarehe 31 Julai mwaka 2007 wakati Baraza lilipoidhinisha azimio namba 1769 la mwaka 2007 kuhusu hali ya Sudan ikiwemo Darfur, kuwalinda raia likiwa kitovu cha shughuli zake.