Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP28: "Hatma ya ubinadamu inaning'inia kwenye mizani."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Hali ya Hewa wa COP28 kwenye Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Walaa Alshaer
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Hali ya Hewa wa COP28 kwenye Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.

COP28: "Hatma ya ubinadamu inaning'inia kwenye mizani."

Tabianchi na mazingira

Kuzuia ajali na kuungua kwa sayari, "tunahitaji...ushirikiano na utashi wa kisiasa", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema leo Ijumaa, akiwapa changamoto viongozi wa dunia waliokusanyika Dubai kwa ajili ya COP28.  

Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wake wa kusisimua katika ufunguzi wa Mkutano huo wa Kimataifa wa Tabianchi, ambao utashuhudia viongozi wa dunia na Wakuu wa Nchi na Serikali wakijadiliana kwa siku mbili zijazo katika Ukumbi wa Al Waha katika Jiji la Maonesho la Dubai. 

Akionya kwamba "hatma ya ubinadamu inaning'inia kwenye mizani", Katibu Mkuu amesema viongozi wa ulimwengu lazima wachukue hatua sasa kumaliza janga la tabianchi. 

Watu wanaohudhuria mkutano wa COP28 katika Banda la Indonesia katika Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Walaa Alshaer
Watu wanaohudhuria mkutano wa COP28 katika Banda la Indonesia katika Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.

"Huu ni ugonjwa ambao ni nyinyi tu, viongozi wa kimataifa, mnaoweza kuuponya," amesema, akitoa wito kwa viongozi kukomesha utegemezi wa ulimwengu kwa nishati ya mafuta na kutimiza ahadi ya muda mrefu ya haki ya tabianchi. 

Bwana Guterres pia amekaribisha mafanikio yaliyopatikana jana Alhamis ya Novemba 30, 2023 katika siku ya ufunguzi wa COP28 baada ya wajumbe kufikia makubaliano juu ya uendeshaji wa mfuko wa hasara na uharibifu ili kusaidia nchi zilizo hatarini zaidi duniani kulipia athari mbaya za maafa ya tabianchi. 

Umoja katika janga 

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbushia safari zake za hivi karibuni huko Antarctica na Nepal, akionesha jinsi alivyoshuhudia kwa macho kiwango cha kuyeyuka kwa barafu. 

"Maeneo haya mawili yako mbali sana, lakini yameungana katika janga," anasema Guterres. 

Ametahadharisha ingawa hii ni dalili moja tu ya ugonjwa unaoipeleka tabianchi yetu  kwenye anguko. 

Mfalme Charles III akihutubia katika Mkutano wa Kilele wa Hatua za Hali ya Hewa Duniani wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, kwenye Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Christophe Viseux
Mfalme Charles III akihutubia katika Mkutano wa Kilele wa Hatua za Hali ya Hewa Duniani wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, kwenye Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Mfalme Charles III  

Miongoni mwa wazungumzaji wengine wa ngazi ya juu leo Ijumaa, Mfalme Charles III wa Uingereza amekumbuka wakati ambapo alialikwa kuzungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kihistoria wa COP21 mjini Paris miaka minane iliyopita, "ambapo mataifa yaliweka tofauti kando kwa manufaa ya wote". 

"Ninasali kwa moyo wangu wote kwamba COP28 iwe hatua nyingine ya mabadiliko," amesema Mfalme Charles.  

Alichukizwa na ukweli kwamba maendeleo kuelekea malengo ya tabianchi yameporomoka, kama takwimu za kiamatifa zinavyoonesha. 

"Kukabiliana na hili ni kazi yetu sote," amesisitiza katika hotuba yake kwa niaba ya Uingereza kwenye Mkutano huo. 

Mfalme Charles ameendelea kutaja athari za mabadiliko ya tabianchi duniani kote, ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa nchini India na Pakistani na moto mkali huko Marekani, Canada na Ugiriki. 

"Isipokuwa kwa haraka tukarabati na kurejesha uchumi wa kipekee wa asili, kwa kuzingatia maelewano na usawa, ambayo ni tegemeo letu la mwisho, uchumi wetu wenyewe na kuendelea kutakuwa hatarini," amesema Mfalme wa Uingereza. 

Rais wa Baraza Kuu la UN na "Mkakati wa Watu kwanza" 

"Mimi mwenyewe kama raia wa Kisiwa kidogo kinachoendelea, ninafahamu kabisa kwamba katika mwelekeo wetu wa sasa visiwa hivyo na utajiri wa utamaduni na historia wanazowakilisha ziko hatarini kutoweka," amesema Dennis Francis, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambaye anatoka Trinidad na Tobago, eneo linalotishiwa na kupanda kwa kina cha bahari kinachoendelea kwa kasi. 

"Ulimwengu wa nyuzi tatu sio maigizo ya kisayansi lakini ni njia tuliyomo sasa," amesema, akimaanisha ukweli kwamba ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea, ulimwengu unaweza kukabiliwa na ongezeko la joto la nyuzi tatu za Selsiasi juu ya enzi ya kabla ya viwanda, badala yake ya shabaha au lengo la nyuzi joto 1.5 iliyowekwa mjini Paris. 

Mwanajamii wa watu wa asili anahudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 katika Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Anthony Fleyhan
Mwanajamii wa watu wa asili anahudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 katika Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Hapa na pale  

Jiji la maonesho, mahali kunakofanyika mazungumzo kuhusu tabianchi, kumejaa shughuli huku kukiwa na ulinzi mkali katika siku ya pili ya COP28, wakati viongozi wa dunia walipoanza kuwasili kwa ajili ya Mkutano wa Utekelezaji. 

Katika siku mbili zijazo, viongozi kutoka zaidi ya nchi 160 wanatarajiwa kuelezea maono yao ya kukabiliana na janga la tabia nchi. 

Dubai, jiji kubwa zaidi katika Umoja wa Falme za Kiarabu, linajulikana sana kwa hali ya hewa ya joto kali sana. Ingawa Desemba kwa kawaida huwa mwezi wa kupendeza, mamia ya waandishi wa habari, wapiga picha na wajumbe wa mashirika ya kiraia wamekuwa wakishindana kutafuta nafasi katika maeneo yenye kivuli ili kupata mapumziko kutokana na jua kali. 

Watu wa jamii za asili wako kwenye mstari wa mbele wa athari za mabadiliko ya tabianchi na wawakilishi wao wanafanya kazi sana - na wanazungumza - katika COP28. Mapema leo Ijumaa ‘Habari za UN’ imekutana na Jacob Johns, ambaye anasema anafanya kazi kueleza sera ya tabianchi kwa maarifa ya kiasili. 

"Tuko hapa kuhamisha mioyo na akili za wahudhuriaji wa mkutano na timu za mazungumzo ili tuishi kwa mshikamano na maisha bora ya baadaye," amesema Bwana Johns, ambaye ni kutoka jamii ya Akimel O'odham, ambao ni watu wa asili wa Marekani. 

"Tunataka kuona hatua halisi dhidi ya tabianchi... Tunataka kuona ufadhili ukienda katika haki ya tabianchi na hazina ya hasara na uharibifu. Tunataka fedha hizi zote zipatikane kwa watu wa asili ambao wanateseka kutokana na kuporomoka kwa tabianchi kunakokaribia, kutokana na upotevu wa ardhi na matukio ya hali mbaya ya hewa,” amesema.