Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sayansi yathibitisha kutwama kwa tabianchi; viongozi COP28 chukueni hatua

Mwanamume akivuka shamba lililokauka katika Mkoa wa Nusa Tenggara Mashariki, Indonesia
© UNICEF/Ulet Ifansasti
Mwanamume akivuka shamba lililokauka katika Mkoa wa Nusa Tenggara Mashariki, Indonesia

Sayansi yathibitisha kutwama kwa tabianchi; viongozi COP28 chukueni hatua

Tabianchi na mazingira

Dunia inazidi kuwa na joto kila uchao katika kasi isiyo ya kawaida, zinaonesha takwimumpya huku viongozi wanoakutana kwenye COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia leo Alhamisi wakitakiwa kuchukua hatua kuondoa binadamu kwenye “tatizo kubwa” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Ingawa mwaka huu wa 2023 bado haujatamatika, ripoti tangulizi ya shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa, WMO inathibitisha kuwa mwaka huu unelekea kuwa mwaka wenye kiwango cha juu zaidi cha joto na kuvunja rekodi, huku kiwango cha joto kikiongezeka kwa nyuzi joto 1.4 katika kipimo cha Selsiyasi, juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Tabianchi inasambaratika mbele ya macho yetu- Guterres

Bwana Guterres anasema mbio zinaendelea ili kutimiza lengo la kutovuka nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kama ilivyokubaliwa na viongozi wa dunia huko Paris, Ufaransa mwaka 2015.

“Tunaishi katika kipindi tukishuhudia tabianchi ikisambaratika –na madhara yake yanasikitisha,” ameonya Katibu Mkuu kupitia ujumbe wake kwa njia ya video,  ujumbe aliotoa wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, katika siku ya kwanza ya mkutano wa kila mwaka wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi,  UNFCCC, mwaka huu ukiwa ni mkutano wa 28 au COP28  ukifanyika Dubai, Falme za Kiarabu.

Barafu zinayeyuka, viwango vya maji baharini vinaongezeka

Katibu Mkuu Guterres hivi karibuni alitembelea Antarctica na Nepa ambako alikuwa shuhuda wa kupungua kwa kiasi kikubwa kwa barafu baharini, na alishtushwa na kasi ya kupungua kwa kiwango cha barafu.

Kwa mujibu wa ripoti ya WMO, kiwango cha barafu baharini huko ncha ya kusini mwa dunia, kilikuwa na ukubwa wa kilometa za mraba milioni 1, ikiwa ni pungufu kupindukia kwa kiwango kinachotakiwa mwishoni mwa msimu wa baridi kali kwenye eneo hilo.

Barafu huko magharibi mwa Amerika ya Kaskazini na milima ya Alps huko Ulay imekumbwa na msimu mkubwa wa kuyeyuka.

Kwa sababu ya kuendelea kwa mkondo joto baharini, na kuyeyuka kwa barafu, ongezeko la kuvunja rekodi la maji ya bahari nalo lilishuhudiwa.

 

Viwango vya hewa chafuzi vinaongezeka

Wakati huo huo, viwango vya hewa chafuzi kama vile hewa ya ukaa, methani na nitrous oksaidi mwaka jana vilifikia viwango vya juu vya kuvunja rekodi, hali kadhalika vimeendelea kuongezeka mwaka huu.

Barafu zinazidi kumeguka na kupungua kutoka eneo la barafu la Patagonian huko merika ya kusini
UN News/Nargiz Shekinskaya
Barafu zinazidi kumeguka na kupungua kutoka eneo la barafu la Patagonian huko merika ya kusini

WMO imesisitiza kuwa viwango vya hewa ya ukaa kwenye anga ni juu kwa asilimia 50 ikilinganishwa na kabla ya kipindi cha mapinduzi ya viwanda, “hii ikimaanisha joto litaendelea kuongezeka miaka mingi ijayo.”

“Hizi ni zaidi ya takwimu,” amesema Petteri Taalas, Katibu Mkuu wa WMO na hivyo kutaka hatua zaidi kudhibiti ongezeko la tabianchi isiyo rafiki kwa karne hii na zijazo.”

Soma taarifa nzima hapa