Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasheria mnaoshauri Israeli muwe makini na ushauri wenu- Wataalamu

Majengo yaliyosambaratishwa Al-Kass Gaza
© WFP
Majengo yaliyosambaratishwa Al-Kass Gaza

Wanasheria mnaoshauri Israeli muwe makini na ushauri wenu- Wataalamu

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wamesihi wanasheria wanaoishauri serikali ya Israeli inayoendelea na mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kipalestina Hamas huko Ukanda wa Gaza, wakatae kuidhinisha kisheria vitendo ambavyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita. 

Msingi wa kauli ya wataalamu hao ni kwamba tangu tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba wanamgambo wa Hamas waliposhambulia Israeli, jeshi la ulinzi la Israeli, IDF limekuwa likiripotiwa kuwa linajipanga kuanza uvamizi wa ardhini baada ya kutekeleza mashambulizi ya angani huko Kaskazini mwa Gaza yaliyosababisha vifo vya wapalestina zaidi ya 3,400 na majeruhi 12,000 wakiwemo watoto.  

Uvamizi huo wa ardhini inaelezwa ni kulipiza kisasi cha mashambulizi yaliyofanywa na Hamas na wanamgambo wengine wa kipalestina nchini Israeli na kuua raia, halikadhalika  kuteka na kushikilia wengine mateka hadi leo hii.  

Wataalamu hao kupitia taarifa yao waliyoitoa hii leo mjini Geneva, Uswisi wanasema bila shaka vitendo vya Hamas dhidi ya raia wa Israeli vilikuwa mauaji.  

Lakini sasa mashambulizi ya Israeli yamekuwa yakielekezwa kwenye maeneo yenye makazi ya watu wengi, yakiharibu makazi, hospitali, masoko huku ikizidi kuweka vizuizi na kuzingira Gaza, imekata usambazaji wa vyakula, maji, umeme na mafuta.  

Sasa wataalamu wanasema kadri ambavyo Israeli inajibu kitendo cha Hamas na kuendesha operesheni zake Gaza, wanasheria wote wanaoshauri kijeshi serikali ya Israeli lazima wabainishe na wasake ushauri ambao utaepusha vitendo ambavyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita.  

Wamesema wanasheria wana wajibu kwa mujibu wa kazi yao kukataa kuidhinisha kisheria vitendo vya kihalifu, vitendo ambavyo vitakiuka sheria ya kimataifa.  

Ifahamike kuwa sheria ya kimataifa pamoja na mambo mengine inataka pande kinzani kulinda raia kwenye mapigano na kuepuka kushambulia miundombinu ya kiraia kama vile mifumo ya maji, hospitali na shule.