Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Jamhuri ya Congo kwa juhudi za kukomesha kutokuwa na utaifa: UNHCR

Nenbo la kampeni ya I Belong ya kuchagiza kuhusu umuhimu wa utaifa kwa watu ambao wanakabiliwa na changamoto hiyo
UNHCR
Nenbo la kampeni ya I Belong ya kuchagiza kuhusu umuhimu wa utaifa kwa watu ambao wanakabiliwa na changamoto hiyo

Heko Jamhuri ya Congo kwa juhudi za kukomesha kutokuwa na utaifa: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

UNHCR, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, leo limeipongeza serikali na watu wa Jamhuri ya Congo Brazzaville kwa kujiunga hivi karibuni na mkataba wa mwaka 1954 wa Hali ya watu wasio na uraia na mkataba wa mwaka 1961 wa kupunguza hali ya kutokuwa na uraia.

Shirika hilo linasema katika nchi yenye wakazi karibu milioni 6, takriban watu 200,000 wametambuliwa na serikali kuwa katika hatari ya kutokuwa na utaifa. Mwaka 2019, nchi hiyo iliahidi rasmi kutia saini mikataba hii muhimu wakati wa kikao cha kamati tendaji ya UNHCR.

Kutia saini mikataba ya kutokuwa na utaifa

Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi miaka minne baadaye, Jamhuri ya Congo ilikamilisha mchakato wa kujiunga tarehe 10 Oktoba 2023, na kuifanya nchi hiyo kuwa mshiriki wa 97 katika mkataba wa 1954 na mshiriki wa 79 kwenye mkataba wa 1961.

"Kujiunga kwa Jamhuri ya Congo katika mikataba hii ni mafanikio ya kupongezwa na ushahidi wa dhamira isiyoyumba ya nchi hiyo ya kutokomeza ukosefu wa utaifa, ambao una madhara makubwa kwa maisha ya mamilioni ya watu duniani kote," amesema Gillian Triggs, Kamishna Mkuu Msaidizi wa Ulinzi wa UNHCR.

Ameongeza kuwa “Jamhuri ya Congo imetoa mfano kwa mataifa mengine barani Afrika kwani masaibu ya mamilioni ya watu wasio na utaifa yanaweza kutatuliwa kupitia utashi wa kisiasa na mabadiliko ya sheria.”

Ushirikiano na Jamhuri ya Congo

UNHCR inafanya kazi kwa karibu na serikali ya Congo Brazzaville kuzuia na kutatua masuala ya ukosefu wa utaifa na bado iko tayari kuunga mkono Jamhuri ya Congo katika kutekeleza mikataba hiyo miwili kikamilifu. 

Kama sehemu ya uungaji mkono wa UNHCR kwa juhudi za serikali za kuimarisha mifumo ya usajili wa raia ili kukabiliana na ukosefu wa utaifa nchini kote, zaidi ya vyeti vya kuzaliwa 30,300 vimekabidhiwa kwa watu walio katika hatari ya kutokuwa na utaifa tangu mwaka 2018, vikiwemo 5,300 kwa watu wa jamii za asili walio katika hatari kubwa zaidi.

Leo hii kwa mujibu wa shirika hilo, mamilioni ya watu ulimwenguni kote wananyimwa utaifa. 

UNHCR inaripoti kuwa kulikuwa na zaidi ya watu milioni 4.4 wasio na utaifa au uraia ambao haujabainishwa katika nchi 95 mwaka wa 2022.

Bila utaifa, watu wasio na utaifa wanazuiwa kupata kikamilifu haki zao za binadamu na kushiriki katika jamii , kupata elimu, huduma za afya au soko rasmi la ajira, uhuru wa kutembea au haki ya kupiga kura, miongoni mwa mengine.

Kampeni ya #IBelong

Kwa kutambua ukubwa wa changamoto ya kutokuwa na utaifa mwaka wa 2014, UNHCR ilizindua kampeni ya kimataifa ya #IBelong inayolenga kukomesha tatizo la kukosa utaifa. 

Tangu kuzinduliwa kwake, nchi 23 zimeridia mkataba mmoja au yote mawili ya ya kutokuwa na utaifa, kuashiria utashi wa kisiasa ulioimarishwa kumaliza ukosefu wa utaifa. Makumi ya maelfu ya watu kote Asia, Ulaya, Afrika na Amerika sasa wana njia ya kupata uraia kutokana na mabadiliko mapya ya sheria.