Asante Kenya kwa kutupa utaifa sasa hofu hatuna tena:Washona
Asante Kenya kwa kutupa utaifa sasa hofu hatuna tena:Washona
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR lilipitisha azimio la kumaliza tatizo la watu wasiokuwa na utaifa ifikapo mwaka 2024. Miaka 2 kabla ya lengo hilo kutimizwa, Kenya imepiga hatua katika harakati za kuwatambua rasmi na kuwapa utaifa Washona walio na asili ya Zimbabwe.
UNHCR imekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Kenya kupitia kampeni yake ya kimataifa ya #IBelong kampeni ya kumaliza tatizo la kutokuwa na utaifa iliyozinduliwa miaka michache iliyopita.
Kabila la washona kutoka Zimbabwe ambao hivi sasa wamepatiwa utaifa nchini Kenya, ndio wamefanikiwa kupiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu tangu kutambulika rasmi na serikali. Washona waliingia Kenya miaka 1960 wakieneza dini halikadhalika kufanya kazi kama vijakazi wa Waingereza.
Tangu watambuliwe rasmi mwaka jana wa 2021, wameweza kupokea vitambulisho na hata hati za kuzaliwa kwa baadhi yao.
UNHCR inapinga hali ya kukosa utaifa
Hatua ya washona kupatiwa utaifa wa Kenya inaenda sanjari na kampeni ya shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi UNHCR ya kuondoa hali ya kutokuwa na utaifa ifikapo mwaka 2024.
Kampeni ilianza mwaka 2014 na inaunga mkono azimio la kupunguza idadi ya watu wasiokuwa na utaifa duniani azimio ambalo lililopitishwa mwaka 1961 kwenye kongamano la UNHCR mjini New York Marekani na kuanza kutekelezwa rasmi mwaka 1975.
Tangu jamii ya Washona kuanza kupatiwa utaifa wa Kenya takribani washona 5000 waliomba na kupokea vitambulisho rasmi vya Kenya. Wengine wapatao 1600 ambao hawakuwa na uraia walipokea hati za kuwatambua kisheria.
Marian Mungani alizaliwa Kenya na anaamini kuwa,” Sasa maisha ya wanangu yatabadilika sio kama ilivyokuwa kwangu mimi.Watoto wangu watasoma vizuri na kupata mambo mazuri zaidi maishani.Mimi nilizaliwa hapa lakini sikuweza kusoma.”
Mwaka 2019 Kenya iliitambua jamii ya Washona na kuifanya kuwa kabila la 45 lililo na watu wasiopungua Elfu 4.
Faida Gawasa ni mmoja ya wakongwe wa jamii hiyo iliyowasili miaka ya 1960 na akielezea hisia zake tangu wapate sauti ya kuwa Wakenya anasema kabla ya kupata hati za uraia, Washona wamekuwa wakiishi katika hali yenye changamoto kwani hawakuweza kutimiza vigezo vya kufanya biashara halali au hata kupata elimu kamili.
Robert Mungani anaunga mkono hilo akisema,”Awali sikuweza kuwa na uhuru wa hata kununua kadi ya simu.Nililazimika kuomba usaidizi kwa wengine kabla ya kupata kitambulisho rasmi.Kwa sasa natembea bila hofu ya kushikwa na ninaweza kufanya nikitakacho kwani niko huru.”
Watoto wa Kishona walishindwa kufanya mitihani ya kitaifa kwa kukosa hati za kuzaliwa ijapokuwa ni wazaliwa wa Kenya. Jacob Thamini alipata tabu alipojitahidi kumaliza shule na kwa mtazamo wake anasema ,”Sasa nitasoma vizuri na kuweza kujipangia maisha.Nilitatizika awali lakini kuna nuru ya yajayo mbele ya safari.Niliweza kupiga kura na kuwachagua niwatakao.Nafurahi sana.”
Madhila ya kutokuwa na utraifa
Washona walishindwa kutembea na kuwa huru kwa kukosa hati muhimu za uraia. Walipowasili Kenya walikuwa na hati za kusafiria za Uingereza.
Baada ya Kenya kupata uhuru mwaka 1963 walipewa nafasi kusajiliwa kuwa wakenya lakini wengi wao waliipoteza fursa hiyo baada ya kupitwa na wakati.
Hilo liliwafanya kukosa utaifa kwani hawakutambulika Zimbabwe, Kenya au hata Uingereza.
Jamii ya Washona aghalabu wanapatikana Githurai,Kinoo,Kiambaa, Hurligham katika kaunti za Nairobi na Kiambu na hata nje ya maeneo ya pwani.
Na uamuzi wa Kenya kuwapatia uraia umebadilidi maisha yao na vizazi vyao vijavyo.