Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha uamuzi wa Kenya wa kumaliza tatizo la utaifa kwa watu wa jamii ya Pemba

Laila Rashidi, mama wa watoto 10 mwenye umri wa miaka 48 kutoka jamii ya Pemba nchini Kenya akipokea cheti cha kuzaliwa kwa mwanawe.
Picha: UNHCR
Laila Rashidi, mama wa watoto 10 mwenye umri wa miaka 48 kutoka jamii ya Pemba nchini Kenya akipokea cheti cha kuzaliwa kwa mwanawe.

UNHCR yakaribisha uamuzi wa Kenya wa kumaliza tatizo la utaifa kwa watu wa jamii ya Pemba

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limepongeza hatua zinazochukuliwa na serikali ya Kenya kutatua tatizo la muda mrefu la kutokuwa na utaifa kwa watu wa jamii ya Pemba wanaoishi nchini humo.

Kwa mujibu wa UNHCR wakati wa maadhimisho ya 59 ya siku ya Jamhuri wiki hii nchini Kenya Rais Willim Ruto alitangaza kwamba serikali itaanza mipango ya mkakati wa kuwatambua watu wa jamii ya Pemba kama rai awa Kenya. 

Caroline van Buren mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya amesema “Kwa mara nyingine Kenya imedhihirisha uongozi bora katika lengo la kutokomeza kutokuwa na utaifa kote duniani.Uamuzi huu utahakikisha watu wa jamii ya Pemba wanapata fursa ya haki wanazostahili. UNHCR ipo tayari kusaidia katika mchakato huu “ 

Ameongeza kuwa usajili na kupewa nyaraka za uraia utawawezesha Wapemba kuchangia kikamilifu kwa jamii ya Kenya na kupata haki zao za msingi saw ana raia wengine wa taifa hilo la Agfrika Mashariki. 

Haki hizo amesema “zinajumuisha fursa ya kupata elimu, huduma za afya, ulinzi wa hifadhi ya jamii, huduma za fedha na kuingia kwenye mfumo rasmi wa siko la ajira.” 

UNHCR  kwa kushirikiana na wadau wengine imesema wataendelea kutoa msaada wa kiufundi na uendeshaji kwa serikali ya Kenya ili kuhakikisha watu wote wasio na utaifa nchini humo wanasajiliwa kama rai awa Kenya na wanaweza kupata nyaraka muhimu ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya susajili na vitambulisho vya kitaifa. 

Zoezi la usajili wa kuzaliwa ili kupambana na ukosefu wa utaifa miongoni mwa jamii ya pwani ya Pemba nchini Kenya
Picha: UNHCR Kenya
Zoezi la usajili wa kuzaliwa ili kupambana na ukosefu wa utaifa miongoni mwa jamii ya pwani ya Pemba nchini Kenya

Kenya imefanya maamuzi muhimu

Kwa mujibu wa UNHCR hivi karibuni Kenya imefanya maamuzi makubwa muhimu katika juhudi za kutatua changamoto ya kutokuwa na uraia nchini mwake "kwa kuwatambua maelfu ya watu wengine wasiokuwa na uraia kama raia wa taifa hilo wakiwemo jamii ya Wamakonde kutoka Msumbiji, Washona kutoka Zimbabwe na watu wengine wenye asili ya India". 

UNHCR imesema uamuzi huu wa karibuni unatilia mkazo dhamira ya serikali ya Kenya ya kutimiza ahadi zake ilizotoa katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu changamoto ya kutokuwa na utaifa uliofanyika Oktoba 2019.  

UNHCR inaihimiza Kenya kutekeleza ahadi zilizosalia, ikiwa ni pamoja na kutimiza mikataba miwili ya Umoja wa Mataifa ya kutokuwa na utaifa na kufanya mageuzi ya kisheria kutokomeza ukosefu wa utaifa nchini Kenya. 

Marekebisho muhimu pia yanahitajika katika sheria ya uraia na uhamiaji ya Kenya ili kuwa na mfumo wa kisheria wa usajili wa watu wasio na utaifa na kuongeza muda wa kikosi kazi cha kukabiliana na changamoto ya kutokuwa na uraia.  

Kikosi kazi kitasimamia taratibu za utambuzi na usajili wa watu wasio na utaifa ambao wanastahili kupata uraia wa Kenya.