Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapinduaji wa serikali ni wale wabadilio aya ya katiba ili kuendelea kuongoza- Rais Doumbouya

Rais Kanali Mamadi Doumbouya, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani.
UN Photo/Cia Pak
Rais Kanali Mamadi Doumbouya, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani.

Wapinduaji wa serikali ni wale wabadilio aya ya katiba ili kuendelea kuongoza- Rais Doumbouya

Amani na Usalama

Jamii ya kimataifa inapaswa kushungulikia mizizi ya mlipuko wa mapinduzi ya kijeshi uliokumba bara la Afrika baada ya mlipuko wa COVID-19, badala ya kulaani wale wanaofanya mapinduzi, amesema Rais Kanali Mamadi Doumbouya, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani.

Amesema maudhui ya mkutano wa sasa ni amani, ustawi, maendeleo na uendelevu, hoja ambazo zina umuhimu sana kwa nchi yao. 

“Baada ya mlipuko wa janga la coronavirus">COVID-19 sasa Afrika imegubikwa na mlipuko wa mapinduzi ya kijeshi hasa katika nchi zinazozungumza lugha ya kifaransa zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kila mtu analaani,” amesema kiongozi huyo ambaye aliapishwa kuwa Rais wa serikali ya mpito baada ya kupindua serikali iliyokuwa madarakani mwaka 2021. 

Amesema kila mtu analaani, kila mtu anaweka vikwazo nchi husika na kuchukizwa nakitendo hicho kilichodhaniwa kuwa kimekwisha. 

Hata hivyo anasema jamii ya kimataifa inapaswa kuwa mkweli na isiridhike tu kwa kulaani matokeo au kitendo bali ishughulikie mizizi ya mapinduzi ya kijeshi. 

“Kama mapinduzi yameongezeka Afrika miaka ya karibuni ni kwa sababu za kina kabisa. Na kutibu ovu hili mabibi na mabwana, lazima tuanzie kwenye mzizi. Wanaopindua serikali si wale wanaotwaa silaha na kupindua utawala. Nataka sote tutambue kuwa wapinduaji ni wale ambao kiujanja wanabadili aya kwenye katiba na kutawala kifalme,” amesema Rais huyo wa Guinea akisema yeye ni mmoja wao waliobeba jukumu la kuepusha taifa lao lisitumbukie kwenye zahma kwani ahadi zilikuwa hazitekelezwi. 

Amefafanua kuwa ni wale wenye kazi nadhifu ambao wanabadili ‘kanuni za mchezo’ ili kusongesha utawala wa nchi na hao ndio wapinduaji wa serikali. 

Rais huyo wa Guinea amesema sasa Afrika imeinuka kuliko wakati wowote ule kwani maisha ni magumu, ukosefu wa usawa umezidi na hayo ni miongoni mwa mambo yanayotishia ustawi hivyo kipaumbele chao sasa Guinea ni ustawi wa watu wake. 

Tazama video yake hapa na soma hotuba yake hapa