Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani haiji moja kwa moja ni lazima ifanyiwe kazi: Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa kwenye sherehe ya kila mwaka ya kugonga kengele ya amani kwenye makao makuu ya UN jijini New York. Marekani.
UN /Manuel Elias
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa kwenye sherehe ya kila mwaka ya kugonga kengele ya amani kwenye makao makuu ya UN jijini New York. Marekani.

Amani haiji moja kwa moja ni lazima ifanyiwe kazi: Guterres

Amani na Usalama

Leo ni siku ya kimataifa ya Amani inayoadhimishwa kila mwaka 21 Septemba. Na mwaka huu siku hii inaadhimishwa dunia ikiwa imeghubikwa na majanga mbalimbali kwa mujibu wa ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa siku hii.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuanzia moto wa nyika, mafuriko, vita, kutoaminiana, umasikini, ukiukwaji wa haki za binadamu na pengo la usawa vimetawala kila kona na kuchangia kutokuwepo kwa utulivu na Amani.

Ameikumbusha dunia kwamba, "amani haiji moja kwa moja ni lazima hatua zichukuliwe kusongesha malengo ya maendeleo endelevu na kutomwacha yeyeto nyuma, lakini pia hatua zichukuliwe kumaliza vita na mizozo ambacho ni chanzo kikuvbwa cha uvunjifu wa amani."

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria ya usiku huko Bentiu, Sudan Kusini.
UNMISS/Gregório Cunha
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria ya usiku huko Bentiu, Sudan Kusini.

Kulinda haki za binadamu

Bwana Guterres amehimiza kuwa suala lingine la msingi ni Hatua ya kudumisha na kulinda haki za binadamu na utu wa kila mtu  hasa tunapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 ya azimio la kimataifa la Haki za Kibinadamu.

Pia hatua ya kutumia zana za kidiplomasia zisizo na ukomo wa wakati, mazungumzo na ushirikiano ili kutuliza mivutano na kumaliza migogoro.

Na mwisho kabisa amesema hatua kwa wale mamilioni ya watu wanaoishi katika jinamizi la vitisho vya vita kwani “Amani sio tu maono bora kwa wanadamu."

"Amani ni wito wa kuchukua hatua, hebu tujitolee kujenga, kuendesha na kudumisha amani kwa wote.”