Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ndio njia pekee ya kuwa na dunia yenye haki na bora kwa wote:Guterres 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres  akigonga kengele ya amani kwenye hafla iliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akigonga kengele ya amani kwenye hafla iliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani

Amani ndio njia pekee ya kuwa na dunia yenye haki na bora kwa wote:Guterres 

Amani na Usalama

Kusaka amani ni mchakato mzuri na wa lazima, na njia pekee ya vitendo kuelekea ulimwengu bora na wa haki kwa watu wote amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Kupitia ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya amani Antonio Guterres amesema “Lakini bado katika maeneo mengi, katika mazingira mengi sana, tunashindwa katika suala la amani.” 

 Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya amani ya mwaka huu siku ambayo kila mwaka huadhimishwa Septemba 21 ni "Komesha ubaguzi wa rangi, jenga amani" ikikumbusha njia nyingi za ubaguzi wa rangi hutia sumu mioyo na akili za watu na kuharibu amani ambayo sote tunaitafuta. 

 Katibu Mkuu ameongerza kuwa “Ubaguzi wa rangi unawanyima watu haki na utu wao. Unachochea ukosefu wa usawa na kutoaminiana. Na unawatenganisha watukatika wakati ambapo tunapaswa kuwa tunashikamana pamoja, kama familia moja ya kibinadamu, kurekebisha ulimwengu wetu uliopasuka.” 

 Tusipigane wenyewe kwa wenyewe tupigane na adui 

Ujumbe huo wa Guterres umeendelea kusisistiza kwamba “Badala ya kupigana sisi kwa sisi, tunapaswa kufanya kazi ili kuwashinda maadui wetu wa kweli ambao ni ubaguzi wa rangi, umaskini, ukosefu wa usawa, migogoro, changamoto za tabianchi na janga la COVID-19. Tunapaswa kubomoa miundo inayoendeleza ubaguzi wa rangi, na kuinua harakati za kupigania haki za binadamu kila mahali.” 

Pia amesema dunia inapaswa kuzima sauti mbaya za kauli za chuki kwa kilio endelevu cha pamoja kwa ajili ya ukweli, kuelewana na kuheshimiana. 

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kuwa “Katika siku hii muhimu, wakati wa kuzingatia saa 24 za kutokuwa na vurugu na kusitisha uhasama tunasisitiza wito wetu kwa watu wote kufanya juhudi zaidi zaidi ya kuweka chini silaha zao. 

Tunatoa wito kwao kuthibitisha tena vifungu vya mshikamano tunaoshiriki kama binadamu na kufikia mchakato wa kujenga ulimwengu bora na wa amani zaidi.”