Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usitishaji uhasama ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres akigonga kengele ya amani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres akigonga kengele ya amani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York

Usitishaji uhasama ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote:Guterres

Amani na Usalama

Usitishaji uhasama wakati huu janga la corona au COVID-19 likiendelea kuighubika dunia ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Katika halfa maalum iliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hii leo kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani ambayo kila mwaka hufanyika Septemba 21 Guterres amesema lengo kuu la siku hiyo ni kuzichagiza pande kinzani kila mahali duniani kuweka chini silaha zao na kuishi na kufanyakazi pamoja kwa amani. 

Ameongeza kuwa wito huo mwaka huu una uzito mkubwa zaidi kutokana na janga la COVID-19 linaloikabili dunia na ndio maana alitoa ombi la kimataifa la usitishaji uhasama mwezi Machi mwaka huu. 

"Dunia yetu inakabiliwa na adui wa pamoja, virusi hatari ambavyo vinasababisha madhila makubwa na kusambaratisha maisha na hivyo kuchangia katika mivutano ya kimataifa na kuongeza shinikizo kwa changamoto zilizopo za upatikanaji wa amani na usalama.” 

Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya amani mwaka huu ni “kuunda amani kwa pamoja” hivyo Katibu Mkuu amesema “kwa dhamira hiyo na maadhimisho ya miaka 75, Umoja wa Mataifa unawaleta watu pamoja kwa ajili ya majadiliano ya kimataifa kuhusu kuunda mustakabali na kudumisha amani katika nyakati za majaribu.” 

Amesema katika siku hizi ambazo hatua za kujitenga kupambana na COVID-19 zikiendelea inaweza kuwa vigumu watu kukutanika kwa pamoja lakini ni lazima kuendelea kushikamana kwa ajili ya amani. 

“Na kwa pamoja najua tunaweza na tutweza kujenga dunia ambayo ina haki, endelevu na yenye usawa.” amesisitiza bwana. Guterres.