Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan kuangaziwa jumatano hii kandoni mwa UNGA 78

Watu wanaendelea kuhama makazi yao kutokana na vita nchini Sudan.
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Watu wanaendelea kuhama makazi yao kutokana na vita nchini Sudan.

Sudan kuangaziwa jumatano hii kandoni mwa UNGA 78

Msaada wa Kibinadamu

Jumatano wiki hii Septemba 20, kutakuwa na tukio maalumu kandoni mwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kukusanya rasilimali na kuonesha uungaji mkono kwa watu wa Sudan. 

Tukio hilo linakuja wakati ambapo mapigano makali katika mji mkuu wa Sudan , Khartoum, mwishoni mwa wiki yamesababisha vifo vya raia, imeeleza Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu, OCHA

“Wadau wetu wa kibinadamu pia wanatuambia kuwa mapigano mapya huko Darfur Kusini yamewakosesha makazi watu wengi katika jiji la Nyala.” Imeeleza OCHA kupitia mkutano wa Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na waandishi wa Habari jijini New York, Marekani. 

Watu wanaendelea kuyahama makazi yao, huku zaidi ya milioni 5.1 wamekimbia makazi yao tangu katikati ya Aprili watu milioni 4.1 ndani ya Sudan na zaidi ya milioni 1 walilazimika kutafuta hifadhi nje ya nchi. 

Waandishi wa Habari wameambiwa, “familia mpya zilizokimbia makazi zinawasili katika maeneo ambayo tayari yalikuwa yanakabiliwa na changamoto kutokana na vurugu zilizopo, huku huduma za kimsingi zikiwa zimejaa.” 

OCHA inasema kulingana na wadau weke, tangu kuanza kwa mzozo wa sasa, takribani watoto 435 wameripotiwa kuuawa na wengine 500 wamekufa kutokana na njaa - ingawa idadi ya kweli inaweza kuwa kubwa zaidi. 

Mpango wa misaada ya Kibinadamu wa dola bilioni 2.6 kwa Sudan, ambao unalenga kusaidia watu milioni 18, hadi sasa umefadhiliwa kwa  asilimia 25.