Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania katika mwelekeo wa kutumia nishati jadidifu majumbani

Sikuzani Abdallah (kushoto) ni mkazi wa kata ya Mbagala yenye wakazi wengi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
UNCDF/Tanzania
Sikuzani Abdallah (kushoto) ni mkazi wa kata ya Mbagala yenye wakazi wengi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Tanzania katika mwelekeo wa kutumia nishati jadidifu majumbani

Tabianchi na mazingira

Nchini Tanzania kuna kaya nyingi ambazo zinatumia mkaa, kuni na mafuta ya taa kama tegemeo kuu la mapishi ya nyumbani, nishati ambazo si rafiki sio tu kwa mazingira bali pia afya ya mamilioni ya binadamu. Lakini sasa kuna mabadiliko,wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unapigia chepuo nishati jadidifu na salama; wakati huu ambapo pia wakuu wa nchi watakutana jijini New York, Marekani kutathmini hatua zipi zimechukuliwa kubadili mwelekeo wa mabadiliko ya tabianchi.  

CookFund imeleta nuru 

Shukrani kwa mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya mitaji, UNCDF uitwao CookFund unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya. Mradi huu unalenga kuchangia katika ahadi za Tanzania katika kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza idadi ya watu wanaopata nishati safi ya kupikia hadi asilimia 80 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.  

Leonardi Kushoka, wa kampuni ya Kuja na Kushoka inayotengeneza mkaa mbadala usiotumia miti ameanza kujihusisha na uzalishaji wa mkaa mbadala tangu mwaka 2016. 

. Anazungumza katika video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji, UNCDF nchini Tanzania, watekelezaji wa mradi wa CookFund. 

Alipoulizwa ni kwa nini alianza kujihusisha na utengenezaji wa mkaa mbadala Bwana anasema, “ni baada ya kuona fursa kubwa inayopatikana kutokana na changamoto kubwa ya watu kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Lakini ziko njia nyingine ambazo tunaweza kuzalisha mkaa kutokana na mabaki ya mimea na takataka nyingine zenye asili ya mimea.” 

Njia rahisi ya kupika ambayo imeboresha sio tu utaratibu wa kila siku lakini pia imechangia mazingira safi na yenye afya kwa jamii Dar es Salaam Tanzania.
UNCDF/Tanzania
Njia rahisi ya kupika ambayo imeboresha sio tu utaratibu wa kila siku lakini pia imechangia mazingira safi na yenye afya kwa jamii Dar es Salaam Tanzania.

Changamoto ni mitaji 

Tina Machibya, kutoka kampuni ya Wema Products inayosambaza gesi anasema wanakabiliwa na changamoto ya kusambaza majawabu ya kutumia nishati ya gesi kama jawabu la kukabili mabadiliko ya tabianchi. 

Bi. Machibya anasema“changamoto ya kwanza ni kwa watu wanaotaka kuanza biashara hiyo kutokuwa na mtaji wa kutosha kumudu gharama za awali za kununua vifaa husika; majiko na mitungi ya gesi. Changamoto ya pili ni  uelewa juu ya kupika kwa kutumia nishati salama.” 

Mradi unatekelezwa DSM, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mwanza 

Hapo ndipo mradi wa CookFund unapoingia ili kukabilia changamoto hizo za uwezo, upatikanaji na mitaji midogo kwa wajasiriamali. Mradi unalenga kuhakikisha nishati salama ya kupikia inapatikana, na inafikia kwa urahisi nchini Tanzania kwa kufikia kaya 580,000 katika mikoa ya mitano ambayo ni Dar es salaam, Pwani,  Morogoro, Dodoma na Mwanza. 

Mradi unapatia familia njia mbadala za kupika ambazo sio tu ni rafiki kwa mazingira bali pia zinapunguza mzigo hasa wakati wa mapishi. 

Sasa wanaume wanashangaa hata hawaombwi tena fedha 

Sylvester Mwambibe kutoka kampuni ya Envotec inayozalisha majiko sanifu ni mnufaika wa programu ya CookFund, halikadhalika shuhuda wa manufaa ya mradi huo. 

Bwana Mwambibe anasema, “kuna baadhi ya kaya ambazo zilikuwa zinatumia gunia moja la mkaa kwa mwezi. Lakini baada ya kuwapatia majiko sanifu sasa wanawake wameacha kabisa kuomba fedha za mkaa kwa waume zao, hadi wanaume wanawauliza, ‘mbona hamjaomba fedha ya mkaa?’ kwa sababu ilikuwa ni kawaida kuomba fedha za kununua mkaa baada ya muda fulani,lakini sasa mwezi mzima ulipita bila kuomba fedha na ndio wanaume wanaulizia kulikoni?.” 

Sikuzani yuko chini ya mradi wa usambazaji wa Moto Safi, kampuni tanzu ya Consumers Choice Limited na mnufaika wa programu ya CookFund.
UNCDF Tanzania
Sikuzani yuko chini ya mradi wa usambazaji wa Moto Safi, kampuni tanzu ya Consumers Choice Limited na mnufaika wa programu ya CookFund.

CookFund imepunguza gharama za majiko 

Mnufaika mwingine wa fedha kutoka CookFund ni kampuni ya Consumer Choice Limited inayotengeneza majiko yanayotumia nishati ya mafuta rafiki kwa mazingira, ambapo afisa wake Isack Danford anasema ambaye anasema, “msaada wa fedha ambao Consumer Choice Limited imepokea kutoka UNCDF, utatuwezesha kufanya gharama ya majiko kwa mtumiaji kuwa nafuu.” 

Sikuzani Abdala, mtumiaij wa jiko kutoka kampuni ya MotoSafi inayotumia nishati ya mafuta aina ya BioEthanol anazungumzia unafuu alioupata baada ya kugeukia nishati mbadala kupikia. 

Bi. Abdalla anasema, “nishati ninazopikia nina ya mkaa, gesi lakini hiyo ya mafuta  ninaiona ni nyepesi sana, kwa sababu ninaweza kuwa natazama Televisheni huku napika mboga yangu Niko hapo hapo, na watu wamelipenda. Nimewaambia watu kuwa jiko ni zuri hata ukirejea safari usiku unaweza kupika haráka".