Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasoka wakongwe duniani kusukuma ‘gozi la SDGs’ Rwanda 2024

Balozi wa Rwanda Claver Gatete (katikati) akiwa na Mkuu wa JMU wa Ofisi ya UN_RC Rwanda Josephine Marealle-Ulimwengu(kushoto), na Mwenyekiti wa VCWC, Fred Siewe(kulia) dakika chache kabla ya Balozi Gatete kuongoza kampeni ya VCWC2024.
VCWC Rwanda
Balozi wa Rwanda Claver Gatete (katikati) akiwa na Mkuu wa JMU wa Ofisi ya UN_RC Rwanda Josephine Marealle-Ulimwengu(kushoto), na Mwenyekiti wa VCWC, Fred Siewe(kulia) dakika chache kabla ya Balozi Gatete kuongoza kampeni ya VCWC2024.

Wanasoka wakongwe duniani kusukuma ‘gozi la SDGs’ Rwanda 2024

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mwakani 2024 macho na masikio yataelekezwa nchini Rwanda ambako huko wanasoka wakongwe duniani watarejelea daluga zao na kutumia kile walichokipenda zaidi, yaani kabumbu au kandanda kusaidia Umoja wa Mataifa kusongesha masuala ya afya, utalii, amani, biashara na elimu.

Ni kupitia mashindano ya kwanza kabisa duniani yatakayoleta wakongwe wa soka ulimwenguni ambao tayari wamestaafu, ambapo kampeni ya kuelekea mashinano hayo imezinduliwa rasmi hii leo jijini New York, Marekani baina ya Umoja wa Mataifa nchini Rwanda, serikali ya Rwanda na Mashindano ya vilabu vya mpira vya wakongwe duniani, VCWC.

Uzinduzi umefanywa na Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Claver Gatete ambapo Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda Ozonnia Ojielo amesema ubia huo unazidi hata hamasa ya soka au kandanda kwa kuwa una manufaa makubwa yanayogusa pande zote.

Jiji la New York, ni moja ya maeneo ambako kunafanyika ziara za kimataifa za kuelezea mashindano hayo ya kimataifa 2024 ambapo nguli wa soka wa kimataifa mkongwe aliyeshiriki ni Edmilson de Moraes wa Brazil.

Nguvu ya michezo katika amani na maendeleo ni ya kipekee

Akizungumza katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yakena Mkuu wa Ofisi yake, Josephine Marealle-Ulimwenguni, Mratibu huyo Mkazi amesema azma ya pamoja inaakisi kujitoa kwetu kusikotetereka kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs  na Imani yetu juu ya nguvu ya michezo na mvuto michezo iliyo nayo duniani wa kuwa kichocheo cha maendeleo.

Mapema akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Bi. Marealle-Ulimwengu alisema kuwa mashindano hayo yataleta pamoja wachezaji wakongwe wa kimataifa wa soka 150 kutoka mabara yote duniani.

Alieleza kuwa VCWC walifika ofisini UN Rwanda na kueleza lengo la kuanzisha mashindano hayo kimataifa yakihusisha wachezaji wakongwe wa kimataifa kwamba “lengo lao sio tu kuanzisha mashindano, lakini pia kutumia wachezaji wakongwe ambao wengine bado wako kwenye biashara, wengine wanaheshimika sana, wengine wana ushawishi mkubwa kwa vijana na nchi zao. Kwa hiyo ni kwa jinsi gani tutatumia wachezaji hawa wakongwe katika kuchangia SDGs.”

Josephine Marealle-Ulimwengu, Head- UN Resident Coordinator Office Rwanda.
UN RWANDA
Josephine Marealle-Ulimwengu, Head- UN Resident Coordinator Office Rwanda.

Muundo wa #VCWC2024 – Soka na Majukwaa

Kwa mujibu wa Bi. Marealle-Ulimwengu, mashindano hayo yataambatana na majukwaa matano pamoja na maonesho ya kando yakihusisha vijana na kwamba yatafanyika kwa takribani wiki kwa tarehe ambayo itatangazwa.

“Sisi kama Umoja wa Mataifa tutashirikiana na wataalamu wetu na washauri wa VCWC kuandaa majukwaa yatakayozungumzia masuala ya maendeleo na amani. Wao VCWC watatafuta wachezaji wakongwe kutoka mabara mbalimbali, sisi tutajikita na majukwaa.”

Jukwaa la kwanza litamulika biashara isiyo na mipaka, “ni kwa jinsi gani tutatumia wachezaji wa mpira wa miguu kupata wawezekaji kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza Rwanda na nchi zingine, na hili litaibua kazi kwa vijana. 

Jukwaa la pili utalii wa michezo, likimulika ni kwa jinsi gai utalii unaweza kutengeneza ajira kwa vijana na pia kukuza uchumi.

Jukwaa la tatu litakuwa ni amani ikumbukwe kuwa mwakani ni miaka 30 tangu mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda. Kwa hiyo na sisi tunatumia nafasi hilo kuonesha ni kwa jinsi gani Rwanda imeweza kuendelea miaka 30 baada ya mauaji hayo ya kimbari.

Jukwaa la nne litazungumzia elimu, ni kwa jinsi gani serikali zetu zinaweza kutumia teknolojia katika kuboresha elimu, na hii teknolojia iweze kuwafikia watu wa kila mahali hata wale wa kipato cha chini. Wakati wa coronavirus">COVID-19 baadhi ya wanafunzi walikosa elimu kwa sababu hawakuwa na teknolojia ya kuwafikishia masomo.

Jukwaa la tano ni afya likimulika magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs na mimba za utotoni, kuona ni kwa jinsi gani zinaathiri hasa wanafunzi wa kike.

Kwa mujibu wa UN Rwanda, Mashindano hayo yanabeba mada kuu ambayo ni Watu , Miradi na Ushirikiano ambapo Bi. Marealle-Ulimwengu amesema mwisho wa siku wanamichezo hao wakongwe wa soka duniani wawe mabalozi wa kusongesha utekelezaji wa miradi itakayoibuliwa wakati wa mashindano hayo.

Soundcloud

Soka ilimnusuru Eric Eugene Murangwa

Hotuba ya Mratibu Mkazi wa UN nchini Rwanda ilimulika ni kwa jinsi gani simulizi ya mwanasoka wa zamani wa kulipwa nchini Rwanda Eric Eugene Murangwa alivyoweza kunusurika kuuawa wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994 .

Murangwa ambaye alikuwa golikipa wa timu ya taifa ya soka ya Rwanda, halikadhalika timu maarufu ya Rayon Sport alinusurika baada ya mmoja wa wauaji kumtambua, hali ambayo ilifanya kitendo walichotarajia kufanya kusitishwa na ndipo Murangwa akatumia fursa hiyo kuanzisha mazungumzo ya mechi za soka alizocheza na umoja uibukao katika kuunga mkono timu ya taifa.

Simulizi hizo zilivunja mipaka ya ukabila ambayo iliibua mauaji ya kimbari na hatimaye wauaji walimwachia huru.

Fred Siewe, Makamu Rais wa VCWC akizungumza jijini New York, wakati wa ziara ya kimataifa ya uzinduzi na upigiaji kampeni mashindano ya VCWC2024 nchini Rwanda yanayoratibiwa kwa pamoja na UN Rwanda, serikali ya Rwanda na VCWC.
UN RWANDA
Fred Siewe, Makamu Rais wa VCWC akizungumza jijini New York, wakati wa ziara ya kimataifa ya uzinduzi na upigiaji kampeni mashindano ya VCWC2024 nchini Rwanda yanayoratibiwa kwa pamoja na UN Rwanda, serikali ya Rwanda na VCWC.

Murangwa aliweza kuhamia Uingereza na kuchezea vilabu mbalimbali na kwa mujibu wa UN Rwanda aliibuka kuwa mchechemuzi wa amani, maridhiano na uepushaji wa mauaji ya kimbari.

Murangwa alianzisha Soka kwa Matumaini, Amani na Umoja, shirika ambalo baadaye liligeuka kuwa Mfuko wa Ishami ukitumia soka kama mbinu ya maridhiano Rwanda na kwingineko na sasa ni Makamu Mwenyekiti wa VCWC akijikita na Jukwaa la Amani.

Mratibu Mkazi wa UN  nchini Rwanda ametoa wito kwa kila mtu kusimama kidete kupigia chepuo #VCWC2024 na ameshukuru serikali ya Rwanda kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.