Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zuia mashambulizi yanayozidi kuongezeka shuleni, ahimiza Guterres

Wanawake vijana waliokimbia Afghanistan wahudhuria mafunzo Pakistan.
© UNHCR/Mercury Transformations
Wanawake vijana waliokimbia Afghanistan wahudhuria mafunzo Pakistan.

Zuia mashambulizi yanayozidi kuongezeka shuleni, ahimiza Guterres

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Kulinda Elimu dhidi ya Mashambulizi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ni muhimu kutetea "mazingira ya elimu". 

Huku kukiwa na ongezeko kubwa la mashambulizi yanayolenga shule na hospitali, na zaidi ya watoto milioni saba wakimbizi hawaendi shuleni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito leo Jumamosi kwa msukumo mpya wa kuwatetea wanafunzi na walimu walio katika mazingira magumu duniani kote. 

"Elimu sio tu haki ya msingi ya binadamu, lakini njia ya maisha bora ya baadaye kwa kila mtu, na ulimwengu wenye amani na uelewa," amesisitiza Guterres. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonesha ukweli wa kushangaza: duniani kote watoto na vijana milioni 224 wanahitaji msaada wa haraka wa elimu - ikiwa ni pamoja na milioni 72 ambao hawako shuleni kabisa - kwa sababu ya migogoro kama vile vita vya silaha. 

Mashambulizi maradufu 

Kwa mujibu wa ripoti ya kina kuhusu watoto na mizozo ya kivita iliyochapishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu, inayoonesha utafiti wa kuanzia Januari hadi Desemba 2022, kulikuwa na ongezeko la asilimia 112 la mashambulizi yaliyolenga shule na hospitali, huku maeneo hatarishi yakitambuliwa nchini Afghanistan, Ukraine, Burkina Faso. Israel, Palestina, Myanmar na Mali. 

Nchini Afghanistan, kwa mfano, Umoja wa Mataifa ulithibitisha jumla ya mashambulizi 95 dhidi ya malengo ya kiraia, ikiwa ni pamoja na 72 dhidi ya shule. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, lilisema Ijumaa kuwa kufikia mwisho wa 2022, jumla ya idadi ya wakimbizi wenye umri wa kwenda shule duniani kote iliongezeka karibu asilimia 50 kutoka milioni 10 mwaka 2021 hadi milioni 14.8, ikisukumwa zaidi na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

'Mahali pa usalama na kujifunza' 

Katibu Mkuu amezitaka nchi zote kuhakikisha ulinzi wa shule, watoto na walimu wakati wote, kupitia hatua kama vile Azimio la Shule salama na Muungano wa Kimataifa wa Kulinda Elimu dhidi ya Mashambulizi. 

Kupitia juhudi za pamoja, Bwana Guterres anaamini, shule zinaweza kuwa "mahali pa usalama na kujifunza kwa kila mtoto, bila kujali anaishi wapi".