Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujua kusoma na kuandika bado 'ndoto' kwa watu milioni 763 duniani

Wanafunzi wote katika madarasa ya UNESCO ya kijamii ya kujua kusoma na kuandika wanapitia masomo kwa mara ya kwanza maishani mwao.
© UNESCO/Navid Rahi
Wanafunzi wote katika madarasa ya UNESCO ya kijamii ya kujua kusoma na kuandika wanapitia masomo kwa mara ya kwanza maishani mwao.

Kujua kusoma na kuandika bado 'ndoto' kwa watu milioni 763 duniani

Utamaduni na Elimu

Hii leo ni siku ya kimataifa ya kujua kusoma na kuandika, siku ambayo inaratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO. 

Katika ujumbe wake wa siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay amesisitiza kuwa kujua kusoma na kuandika ni sawa na hati ya kusafiria ya kumwezesha mtu kuwasiliana na wenzake, na hivyo kuimarisha maelewano kati na baina ya watu. 

Sherehe za Elimu ya Watu Wazima kwenye shule ya sekondari ya juu ya wavulana ya Eastleigh jijiin Nairobi ,Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Sherehe za Elimu ya Watu Wazima kwenye shule ya sekondari ya juu ya wavulana ya Eastleigh jijiin Nairobi ,Kenya.

Maudhi ya mwaka huu 

Mwaka huu, maudhui ya siku ya kimataifa ya kujua kusoma na kuandika ni Kusongesha kujua kusoma na kuandika katika dunia iliyoko kwenye mpito:Kujenga msingi kwa jamii endelevu na zenye amani. 

UNESCO inasema licha ya maendeleo yaliyopatikana duniani kote, kujua kusoma na kuandika bado kunakabiliwa na changamoto kwani takribani vijana na watu wazima milioni 763 duniani kote hawakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika mwaka 2020. 

COVID-19 na majanga mengine yatwamisha kusoma na kuandika 

Janga la hivi karibuni la coronavirus">COVID-19 na majanga mengine yamechochea changamoto za watu kutokujua kusoma na kuandika. 

UNESCO inasema mabadiliko makubwa yanayoendelea kwa kasi duniani yamekwamisha zaidi maendeleo kwenye kuwezesha watu kujua kusoma na kuandika na kuchochea ukosefu wa usawa duniani kote. 

Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019)
© UNICEF/Frank Dejo
Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019)

Katika nchi za kipato cha chini na cha kati, kiwango cha watoto wenye umri wa miaka 10 ambao hawajui kusoma na kuandika na kuelewa kusoma sentensi rahisi imeongezeka kutoka asilimia 57 mwaka 2019 hadi asilimia 70 mwaka 2022. 

Kuelekea siku ya kimataifa ya kulinda elimu isishambuliwe, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma ujumbe wake akisema elimu ni njia ya kuwa na mustakabali bora kwa kila mtu. 

Ametoa wito kwa kila nchi kuhakikisha shule, watoto na walimu wanalindwa kila wakati, huku akisihi nchi kuridhia Azimio la Shule Salama.