Watu wanaojua kusoma na kuandika wameongezeka duniani lakini juhudi zaidi zahitajika:UNESCO

8 Septemba 2021

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kujua kusoma na kuandika leo Septemba 8 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO linasema kumekuwa na hatua kubwa katika miongo kadhaa iliyopita.

Takwimu za mwaka 2019 zikionesha kwamba asilimia 86 ya watu kote ulimwenguni wana uwezo wa kusoma na kuandika ikilinganishwa na asilimia 68 mwaka 1979.

Katika ujumbe wake kwa siku ya leo, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi. Audrey Azoulay ameanza na kumnukuu kiongozi na mwandishi mashuhuri kutoka Marekani, Frederick Douglass aliyesema, “pindi tu unapojua kusoma, daima utakuwa huru."

Hatahivyo Bi. Azoulay amesema hatua zilizopigwa zinatishiwa kwa mfano nchini Afghanistan, nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. 

Ameongeza kuwa kampeni kubwa zaidi ya kusoma na kuandika katika historia ya UNESCO iliendeshwa huko Kabul na majimbo ya Afghanistan, na tangu ilipoanza mnamo mwaka 2006 imewahusisha zaidi ya Waafghanistan milioni 1.2, wakiwemo wanawake 800,000. 

Elimu ya Waafghanistan wote lazima iendelee ameongeza . Mustakabali wa nchi unategemea hii  sio tu kwamba elimu ni haki ya kimsingi, pia ni kiungo muhimu katika kufanikisha maendeleo.  

Wakati huo huo, hatua katika kusoma na kuandika ulimwenguni kote zinaendelea kuzuiliwa na janga la COVID-19. Kwa maana hiyo, amesema kumekuwa na tofauti za kielimu zikichochewa zaidi na utofauti wa ufikiaji wa teknolojia za kidijitali. 

Kulingana na takwimu za UNESCO, ukosefu wa fursa ya kusoma kwa njia za kidijitali umesababisa wanafunzi milioni 500 kuachwa nyuma, kwani wameshindwa kuendelea kujifunza kusoma na kuandika, na wakati mwingine wameshindwa kuanza masomo yao. 

Mkurugenzi mkuu huyo amesema Janga la Corona limeathiri vibaya watu waliotengwa zaidi, hususan vijana na watu wazima milioni 773 kwani hawana ujuzi wa kimsingi wa kusoma na kuandika, theluthi mbili kati yao ni wanawake, na watoto milioni 617 na barubaru ambao walikuwa hawajafikia viwango vya chini vya kusoma kabla ya janga. 

Kwa hivyo amesisitiza kuwa ugonjwa wa virusi vya corona au COVID-19 umefichua umuhimu mkubwa wa elimu na hitaji la kuongeza juhudi.  

UNESCO imeonyesha kujitolea kwake katika elimu tangu mwanzo wa janga hilo kwa kuzindua Umoja wa Kimataifa wa Elimu, kwa kushirikiana na washirika 180 wanaofanya kazi katika nchi 100 tofauti.  

UNESCO pia imezindua mipango kadhaa ya kuhakikisha mwendelezo wa elimu na kuhakikisha kuwa shule zinaweza kufunguliwa salama. 

Hasa, Umoja wa Kimataifa wa Elimu, pamoja na Umoja wa Kimataifa wa Kujua kusoma na kuandika katika mfumo wa mafunzo ya maisha yote, imetekeleza mpango mkubwa wa kufundisha walimu 100,000 katika zaidi ya nchi 10 tofauti, ili waweze kutumia vizuri ujuzi wao wa kidijitali kusaidia kila mtu aweze kusoma na kuandika. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter