Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Fadhilini zaidi miradi ya kusaidia watoto kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Watoto barani Afrika ni miongoni mwa walio katika hatari zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
© UNICEF/Raphael Pouget
Watoto barani Afrika ni miongoni mwa walio katika hatari zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

UNICEF: Fadhilini zaidi miradi ya kusaidia watoto kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

"Ni dhahiri shahiri kuwa wanachama wachanga zaidi wa Bara la Afrika ambao ni watoto wa Kiafrika wanabeba mzigo mkubwa wa athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi,” amesema leo Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Lieke van de Wiel.

Kauli ya Wiel inafuatia ripoti ya UNICEF iliyotolewa leo iitwayo, Muda wa Kuchukua Hatua: Watoto wa Kiafrika wakiangaziwa katika mabadiliko ya Tabianchi, iliyofanya tathmini ya watoto kutoka nchi 49 za Afrika na kubaini watoto wa nchi 48 wako katika hatari kubwa au kubwa sana ya athari za mabadiliko ya Tabianchi. 

kuelekea ufunguzi wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi kwa Afrika jijini Nairobi Kenya ripoti hiyo ya UNICEF imezinduliwa jijini huko ambapo imefanya uchambuzi uliotathmini nchi kulingana na kiasi wanachofidiwa watoto kutokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi, kama vile vimbunga na joto kali, na vile vile uwezekano wao wa kuathiriwa na majanga hayo, kulingana na ufikiaji wao wa huduma muhimu.

Ripoti mpya inaonyesha, licha ya hatari zinazowakabili watoto ni asilimia 2.4 tu ya ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi duniani unalenga watoto suala ambapo Wiel amesema lazima libadilike

“Wao (watoto) ndio wenye uwezo mdogo wa kustahimili, kutokana na kuathirika kisaikolojia na upatikanaji duni wa huduma muhimu za kijamii. Tunahitaji kuona kundi hilo la watoto linawekewa mkazo mkubwa zaidi wa ufadhili, ili wawe na vifaa vya kukabiliana na usumbufu wa maisha unaosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi."

Kundi la watoto wakiwa nje ya shule yao katika mkoa wa Inhambane, Msumbiji, ambao uliharibiwa na kimbunga Freddy.
© UNICEF
Kundi la watoto wakiwa nje ya shule yao katika mkoa wa Inhambane, Msumbiji, ambao uliharibiwa na kimbunga Freddy.

Umoja wa Mataifa unasaidia 

Watoto wako katika hatari zaidi kuliko watu wazima kwa athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na mikazo. Watoto hawana uwezo wa kimwili kustahimili hatari kama vile mafuriko, ukame, dhoruba na mawimbi ya joto. 

Kisaikolojia huathiriwa zaidi na vitu vya sumu kama vile risasi na aina zingine za uchafuzi wa mazingira.

UNICEF na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira UNEP wanafanya kazi pamoja katika kuongezeka kwa idadi ya miradi inayoonyesha jinsi jumuiya kote barani Afrika zinavyoweza kustahimili zaidi wanapokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mfano wa miradi hiyo ni katika ukanda wa pwani ya Tanzania, UNEP inafanya kazi ili kupunguza madhara ya kuongezeka kwa kina cha bahari kwenye miundombinu kupitia kuwekeza kwenye kuta za bahari, kubadilisha maeneo yaliyochimbwa visima, kurejesha misitu ya mikoko na kujenga mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua kupitia mfumo wa ikolojia. 

Yote hayo ili kukabiliana na athari za tabianchi na kutokana na hali hiyo sasa uwezo wa jamii za pwani kustahimili kupanda kwa kina cha bahari umeongezeka na pia kumesababisha kuboreshwa kwa afya kwa wakazi kupitia upatikanaji wa maji safi na salama.

Kusoma zaidi kuhusu taarifa hii kwa kiingereza bofya hapa.