Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana mmechangia kwa kiasi kubwa hatua kwa tabianchi- Guterres

Jopo la vijana la UN la ushauri kuhusu mabadiliko ya tabianchi
UN/Climate Action
Jopo la vijana la UN la ushauri kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Vijana mmechangia kwa kiasi kubwa hatua kwa tabianchi- Guterres

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa vijana wa Afrika kuhusu tabianchi ukianza leo huko Nairobi nchini Kenya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia vijana waendelee kupaza sauti zao za hatua kwa tabianchi ili kunusuru sayari dunia.

Guterres amesema hayo kupitia ujumbe wake kwa njia ya video kwa mkutano huo wa vijana unaofanyika hadi tarehe 3 mwezi huu kabla ya kuanza kwa mkutano wa viongozi wa Afrika kuhusu tabianchi tarehe 4 mwezi huu huko huko Nairobi.

“Mabadiliko ya tabianchi yametufikia na ukosefu wa haki ndio kitovu cha janga hili. Nchi za Afrika hazijachangia chochote kwenye utoaji wa hewa chafuzi, lakini ndio zinazokumbwa na kiwango kikubwa cha joto na mafuriko makubwa na ukame mkali” amesema Katibu Mkuu.

Vijana ndio taswira ya uongozi kwa tabianchi

Hata hivyo amesema ubinadamu una nguvu ya kubadili mwelekeo na “watu kama ninyi ndio mmeongoza njia. Kujizatiti na moyo wa vijana duniani kote vinahusika na hatua dhidi ya tabianchi zilizoshuhudiwa kwa kiasi kikubwa. Ninyi ndio taswira ya uongozi kwa tabianchi unavyopaswa kuwa.”

Ni kwa mantiki hiyo ametaka vijana waendelee kushinikiza kwa sababu “tunazo mbinu na teknolojia zinazohitajika kujilinda wenyewe dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuzuia kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto mbili katika kipimo cha Selsiyasi huku tukiunga mkono maendeleo endelevu.”

Viongozi wa dunia wachukue hatua

Amesema hata hivyo viongozi wa dunia wanapaswa kuchukua hatua za kasi dhidi ya tabianchi hasa wale wachafuzi wakubwa.

Halikadhalika zipatie nchi zinazoendelea zinapatiwa ufadhili wa kifedha kuweza kufanikisha kipindi cha mpito kuelekea nishati safi na wakati huo huo ahadi ya dola bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya hatua kwa tabianchi itimizwe.

Bara la Afrika linachangia asilimia 3 tu ya kiwango chote cha hewa chafuzi kinachotolewa duniain.